http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928504/medRes/2219918/-/wcpd8a/-/zeina.jpg

 

Dkt Ali Shein: Zanzibar inazidi kupiga hatua katika sekta ya elimu

Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) akiwa katika hafla Jumatano, Januari 9, 2018, huko Bwefuu katika hafla ya Ufunguzi wa skuli ya msingi na Sekondari ya Bwefum Wilaya ya Magharibi B; Unguja, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Picha/HAJI MTUMWA 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  07:50

Kwa Muhtasari

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein amesema hatua ya Serikali kutangaza elimu bila malipo mwaka 1964, ililenga kuwakomboa kielimu watoto wa wanyonge wa visiwani hapo.

 

VISIWANI ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein amesema hatua ya Serikali kutangaza elimu bila malipo Septemba 23, 1964, ililenga kuwakomboa kielimu watoto wa wanyonge wa visiwani hapo.

Alisema kabla ya mapinduzi matukufu ya 1964, watoto wa kimaskini walikosa kabisa fursa ya kupata elimu, kutokana na kukosa uwezo wa kuigharamia.

Dkt Shein alisema hayo Jumatano huko Bwefuu katika hafla ya Ufunguzi wa skuli ya msingi na Sekondari ya Bwefum Wilaya ya Magharibi B; Unguja, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Alisema kabla ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na skuli chache ambapo watu wenye uwezo pekee ndio waliopata fursa ya kupeleka watoto wao kupata elimu.

Alisema katika ukanda wa maeneo ya Kiembesamaki hadi Bwefum, kulikuwa na skuli chache zilizojengwa, ikiwemo  skuli ya msingi Kombeni iliyojengwa mwaka 1935, Kiembe samaki (1943) na Bwefum mwaka 1956.

Alieleza skuli ya mwanzo ambayo ilitumika zaidi kwa watoto wa Kiafrika ilikuwa ni skuli Dole, iliyojengwa mwaka 1935, sambamba na skuli ya Uzini, Wilaya Kati Unguja.

Kupiga hatua

Alieleza kuwa Mapinduzi ya 1964, yameifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu, na kubainisha kuwa kabla ya Mapinduzi hayo kulikuwa na  skuli zisizozidi 60, wakati ambapo hivi sasa zimefikia zaidi ya 400.

Aidha alisema Zanzibar hivi sasa ina vyuo vikuu vitatu, wakati ambapo miaka 22 iliyopita hakukuwa na chuo kikuu hata kimoja.

Dkt Shein alirudia kauli yake kwa kuwataka wazazi na walezi kutokuchangia mahitaji ya kielimu kwa watoto wao, kwa vile serikali tayari imefuta michango yote katika skuli za msingi na Sekondari.

Alifafanua kwa kusema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya uchumi kuimarika kutokana na ukusanyaji bora wa kodi pamoja na misaada mbali mbali ya washirika wa maendeleo na wawekezaji wazalendo.

Akitoa mfano, alisema wakati anaingia madarakani mwaka 2010 Serikali ilikuwa ikikusanya kodi ya TSh13.5 bilioni kwa mwezi, wakati hivi sasa inakusanya wastani wa TSh65 bilioni kwa kipindi kama  hicho.

"Hii sio kazi ya mchezo ni kazi nzuri inayofanywa na taasisi zetu za kukusanya kodi,nami sitaki mchezo katika suala la ukusanyaji wa kodi, sina msalie mtume katika suala hilo," alisema Dkt Shein.

Aliwapongeza baadhi ya wafanya biashara wenye nia njema na serikali kwa kulipa kodi kwa hiari, huku akiwaasa wale wenye tabia ya kukwepa kulipa kodi.

Alisema kiwango hicho kikubwa cha ukusanyaji kodi kinathibitisha utekelezaji bora wa Ilani ya CCM, akibainisha matarajio makubwa ya kufikiwa kwa malengo kabla ya wakati uliopangwa.

Aidha, aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kusimamia na kuhoji  mwenendo wa mapato ya Serikali, pale panapotokea mashaka.

Alieleza kuwa ukusanyaji bora wa mapato ndio unaoiwezesha serikali kutekeleza malengo yake ya maendeleo, kupitia sekta mbalimbali, kama vile elimu, afya, viwanda na nyinginezo.

Elimu

Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi chache katika Bara la Afrika zinazotoa elimu bure, akiitaja Tanzania Bara kufanikiwa katika suala hilo, huku Kenya ikiwa pia inapiga hatua.

"Lakini sisi tumeanza tangu 1964 na hadi leo tunaendelea, tumezishinda nchi nyingi zenye uwezo mkubwa," alisema.

Aidha, alisema hatua hiyo imefungua fursa ya kuongezeka kwa madarasa ya skuli za msingi ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi, hatua aliyoinasibisha na kuongezeka kwa idadi ya watu nchini, ambapo kabla ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na watu wapatao 300,000 wakati hivi sasa imefikia Milioni moja na nusu.

Katika hatua nyingine, Dkt Shein alisema Serikali imepunguza kiwango cha kupokea misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo, kutoka asilimia 30.2 mwaka  2010 hadi kufikia asilimia 7.2 hivi sasa, akibainisha kiwango hicho kuzidi kupungua mwaka huu pamoja na mikopo.

Aidha, alimpongeza Rais mstaafu awamu ya tano Dkt Salmin Amour Juma kwa kupanga maeneo ya Fumba na Micheweni kuwa ya Uwekezaji, kwa lengo la kuyabadili maeneo hayo na hivyo watu wake kupata heshima kubwa.

Alisema Serikali inakusudia kuyaendeleza maeneo hayo ili kuimarisha jamii hiyo na maendeleo ya miji yake.

Aliongeza kwa kusema kuimarika kwa maeneo hayo kumewafanya wageni mbali mbali wanaozuru Zanzibar kushajiika kuyatembelea ili kujionea maendeleo makubwa yaliofikiwa.

Alieleza kuwa amefursahishwa sana na wananchi wa maeneo hayo kuridhia uwekezaji huo na hivyo kunufaika na maendeleo yanayojiri kila kukicha.

Aliwapongeza watu wa Bwefum na kuwataka kuongeza nguvu na mapenzi kwa serikali yao.

Aidha, aliipongeza Kampuni ya Union Property Developers Ltd kwa kujitolea na kujenga skuli hiyo, hivyo akawataka wana Bwefum kuthamini hatua hiyo kuwa ni neeema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aliwasihi wasizibeze na kuzikufuru neema kama hizo, pamoja na kuwataka wawekezaji hao kuendeleza misaada yao kwa maendeleo ya Zanzibar.

Akigusia kauli ya baadhi ya watu 'wasiojielewa ' ya kumhusisha na madai ya kuwadanganya wananchi kisiwani Pemba kwa kudai kuwa hakuna maendeleeo yoyote yaliofikiwa, Dkt Shein alisema kauli hiyo kamwe haiwezi kuwavunja moyo wananchi, kwa vile maendeleo yanayozungumzwa yamekuwa aykionekana na kila mwenye macho.

Aidha, aliweka bayana kuwa suala la utiaji saini mkataba wa  mafuta na gesi asili kuwa ulifanyika hadharani na kufuatiliwa na vyombo kadhaa vya habari, hivyo kupinga madai ya watu hao kuwa ulifanyika kwa siri.

"Kama ile inaitwa siri, dhihiri inaitwaje?" alihoji.

Akigusia kauli za watu hao na Muungano, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa 1964, ulikuwa ni wa hiari na kubainisha kuwa miongoni mwa wale wanaoutia dosari Muungano huo, walikuwepo Serikalini wakati ulipokuwa ukiundwa.

Aidha, Dkt Shein alisema Sherehe za Mpinduzi zitafanyika kisiwani Pemba na kuwaonya wale wote wenye lengo la kuvuruga sherehe hizo.

"Tumeamuwa kwa makusudi sherehe kuzifanya kisiiwani Pemba, tulijuwa wataumwa, sasa kama kuna yeote mwenye ubavu tutaona," alisema.

Aliwakakikishia wananchi kuwa Serikali imejiimarisha katika suala la ulinzi katika mji wa Zanzibar pamoja na kununua vifaa vipya kwa ajili ya shughuli za usalama baharinin nchini kote.

Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alimpongeza Rais kwa kutoa fursa kwa Wawekezaji wazalendo kusaidia sekta ya elimu nchini, hivyo kuibuwa chachu kwa wawekezaji wengine kusaidia sekta hiyo.

"Hii ni sadakatul jariya kubwa sana nae Mungu atamfungulia biashara zake," alisema.

Alisema Said Bakhresa ni mwekezaji mzalendo ambae amekuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kuwekeza miradi mbali mbali ya maendeleo, hivyo kutoa fursa kadhaa za ajira kwa vijana wa Kizanzibari.

Aidha, aliwapongeza wananchi wa Bwefum kwa kutoa ushirikiano mkubwa wakati ujenzi huo ukiendelea.

Alimpongeza Dkt Shein kwa jitihada kubwa anazozichukuwa katika kusimamia sekta ya elimu nchini na kubainisha kuwa hatua hiyo inatokana na kutambuwa umuhimu wa elimu kuwa ndio msingi wa maendeleo.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Dkt Idrisa Muslih Hijja akitoa maelezo ya kitaalmu kuhusiana na ujenzi huo, alisema Skuli hiyo imejengwa kwa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya Union Property Developers Ltd ya Tanzania.

Alisema kazi ya ujenzi huo ulioanza Septemba mosi, mwaka 2016 na kumalizika Desemba 2, 2018, ukitekelezwa na Kampuni ya Quality Building Contactors Ltd ya Zanzibar, kwa gharama ya zaidi ya TSh2.4 bilioni hadi kukamilika kwake.

Alisema mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa skuli hiyo ya ghorofa moja ni kusamehe Kodi ya vifaa vyote vya ujenzi.

"Serikali pia itakuwa na jukumu la kufanya matengenezo madogo madogo na kurekebisha kasoro nyengine zitakazojitokeza, ikiwa ni hatua ya kuitunza skuli hiyo", alisema.

Dkt Idrisa alisema Wizara imepanga kuigawa skuli hiyo na kuwa skuli mbili, ikiwa ni skuli ya Msingi Bwefum na Skuli ya Sekondari ya Bwefum, zitakazokuwa na utawala tofauti kwa lengo la kusaidia uongozi katika usimamizi wa skuli hizo, kuambatana na mfumo wa ugatuzi nchini.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Kampuni ya Union Property Developers Ltd kwa uamuzi na moyo wao wa kizalendo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika dhana ya kudumisha Mapinduzi.

Alitoa wito kwa viongozi wa skuli, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla, kuitunza na kuienzi skuli hiyo ili iweze kutumiwa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.