Zura yaimwagia Zawa mamilioni

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  12:32

Kwa Muhtasari

  • Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Haji Kali Haji, amesema imeipatia mkopo wa TSh500 milioni Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) ili kufunga mita za kawaida 5,000 kwa wananchi

  • Hatua hiyo ni utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia shughuli za majisafi na salama ili kuhakikisha Zawa inatoa huduma bora na endelevu kwa jamii

 

VISIWANI ZANZIBAR

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imeipatia mkopo wa TSh500 milioni Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) ili kufunga mita za kawaida 5,000 kwa wananchi.

Mbali na mkopo, pia mamlaka hiyo imepatiwa ruzuku ya TSh500 milioni ili kufanikisha mradi wa usambazaji maji katika Jimbo la Kikwajuni.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi mkuu wa Zura, Haji Kali Haji, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia shughuli za majisafi na salama ili kuhakikisha Zawa inatoa huduma bora na endelevu kwa jamii.

 

Wananchi wa Kikwajuni kufaidika

Haji alisema msaada huo utasaidia kuendeleza juhudi za kuwapatia maji wananchi wa Kikwajuni ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakihangaika kutafuta huduma hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa Zawa, Mussa Ramadhan Haji aliahidi kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwamo kutatua kero zilizopo ili wananchi wafurahie huduma bora zinazotolewa na mamlaka hiyo.