http://www.swahilihub.com/image/view/-/4586948/medRes/1990431/-/my6hlhz/-/wasilo.jpg

 

Busara ilihitajika bomba la mafuta

Dkt Medard Kalemani.

Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dkt Medard Kalemani. Picha/HISANI 

Na KELVIN MATANDIKO, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  13:01

Kwa Muhtasari

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Bandari ya Tanga kuanza Juni mosi.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

WAKATI utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania ukitarajiwa kuanza rasmi Juni mosi, Waziri wa Nishati, Dkt Merdard Kalemani amesema busara na hekima ya hali ya juu ilihitajika kufanikisha hatua ya majadiliano.

Kalenda ya kuanza utekelezaji wa mradi huo imepitishwa Januari 25 jijini Kampala, Uganda kupitia mkutano wa mawaziri wa masuala ya nishati wa nchi hizo, uliokuwa na lengo la kumalizia ‘viporo’ vya masuala yote yaliyowekwa kando katika mkutano wa Desemba 7 mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Mafanikio ya mkutano huo yametoa mwelekeo wa kutiliana saini mkataba kati ya mwekezaji na nchi husika ili kuanza rasmi utekelezaji mradi.

Mkataba huo kati ya mwekezaji na nchi husika, utaweka misingi ya utekelezaji wa mradi kwa kuangalia masuala ya kodi na mapato mengine yatokanayo na mradi, ushiriki wa Watanzania, namna ya kushughulika na migogoro na mambo mengine ya kisheria.

Akizungumza Jumanne katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Dkt Kalemani alisema ili kufikia makubaliano hayo ilihitaji busara na hekima ya kiwango cha hali ya juu kupitia vikao mbalimbali vilivyofanyika.

“Ni kazi iliyokuwa inahitaji hekima na busara ya hali ya juu, tunashukuru kazi imekamilika…. Tanzania jambo la msingi ilikuwa lazima tujipange vizuri kuangalia manufaa ya bomba hili,” alisema.

Mradi huo utakaogharimu Dola 3.5 bilioni za Marekani, kilomita 1,145 kati ya 1445 za mradi huo zitajengwa hapa nchini.