http://www.swahilihub.com/image/view/-/4577392/medRes/1983631/-/ofn3bi/-/mbajeti.jpg

 

Diplomasia ya uchumi ilivyoleta neema

Waziri Augustine Mahiga

Dkt Augustine Mahiga ni Waziri wa Mambo ya Nje, Kikanda na Kimataifa. Picha/HISANI 

Na KHALIFA SAID, Mwananchi  

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  12:40

Kwa Muhtasari

Diplomasia ya uchumi ni msisitizo wa sera ya mambo ya nje yenye mikakati, malengo, mbinu na maarifa yanayoelekeza Taifa kupata na kuvuna rasilimali na utaalamu kutoka jumuiya ya kimataifa ili kuleta na kuchochea maendeleo ya taifa husika.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

OKTOBA 7, 2016, takriban mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano, Rais John Magufuli alikutana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini hapa.

Ikiwa ilikuwa mara yake ya kwanza kukutana nao tangu achaguliwe, Rais Magufuli aliwataka mabalozi hao, pamoja na mambo mengine, kusimamia utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ili isaidie katika uwekezaji katika sekta ya viwanda.

“Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaishe watu wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo,” alisema Rais Magufuli.

Tangu aingie madarakani Magufuli ameweka wazi nia yake ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kusukuma ajenda ya viwanda. Amekuwa akisisitiza umuhimu wa ujenzi wa viwanda akiamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kumsaidia kutimiza azma hiyo.

Ni katika msingi huu Rais Magufuli, pengine kuliko rais mwingine yeyote wa Tanzania, amekuwa mstari wa mbele kuhimiza diplomasia ya uchumi akiamini inaweza kutoa mchango mkubwa katika kuupeleka mbele uchumi wa taifa.

 

Chimbuko la diplomasia ya uchumi

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt Augustine Mahiga, diplomasia ya uchumi ni msisitizo wa sera ya mambo ya nje yenye mikakati, malengo, mbinu na maarifa yanayoelekeza Taifa kupata na kuvuna rasilimali na utaalamu kutoka jumuiya ya kimataifa ili kuleta na kuchochea maendeleo ya taifa husika.

Mwaka 2001 Tanzania ilipitisha sera inayosisitiza diplomasia ya uchumi ili kuendeleza maendeleo hasa katika sekta ya uchumi. Haya yalikuwa mabadiliko makubwa ya sera ya mambo ya nje ya nchi ambayo katika miaka ya sitini na themanini malengo ya ziada katika sera ya Tanzania yalikuwa ukombozi wa bara la Afrika kutoka kwa wakoloni na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Baada ya kukamilisha hayo ndipo Tanzania iliona umuhimu wa kuwa na sera ya mambo ya nje yenye msisitizo wa diplomasia ya uchumi ili kusukuma maendeleo ya taifa.

Diplomasia ya uchumi wa viwanda inakusudiwa itoe vipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu, nishati, biashara na masoko ya bidhaa kutoka viwandani. Sambamba na mkakati huo, dhana ya diplomasia ya uchumi inategemewa kulenga sekta nyingine kama kilimo, utalii na madini ambayo kwa namna moja au nyingine yanashabihiana na viwanda.

Hali ikoje kwa sasa

Akiwa anatimiza miaka mitatu tangu achaguliwe, kuna mambo kadhaa yanayoonyesha ni kwa kiasi gani msimamo wa Rais Magufuli katika diplomasia ya uchumi imesaidia kutimiza baadhi ya malengo ya kitaifa.

Akiwasilisha taarifa ya wizara yake katika Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Dkt Mahiga alisema miongoni mwa mafanikio ya diplomasia ya uchumi ni kushawishi wawekezaji kuja nchini.

Alisema Serikali imeweza kuleta nchini ujumbe wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi kadhaa kama Ujerumani, Ufaransa, Hispania, Misri, China, India, Falme za Kiarabu, Oman na Israel. Baadhi ya wawekezaji hao tayari wameingia ubia na kampuni za Tanzania na wengine wameanza hatua mbalimbali za uwekezaji nchini.

Kwa mfano, mwezi Aprili jumuiya ya wafanyabiashara wa Ujerumani ilifungua ofisi maalumu inayoitwa AHK kwa lengo la kuratibu kwa ukaribu zaidi uwekezaji na biashara zinazofanywa na zitakazofanywa na Ujerumani nchini. Aidha, Ufaransa imefungua ofisi ya biashara kupitia kampuni ya BASF kwa lengo la kuratibu shughuli za kibiashara zitakazokuwa zikifanywa na kampuni hiyo na wabia wake, hususan katika masuala ya uzalishaji wa kemikali za viwandani.

Pia, Febuari, 2018 Dk Mahiga alikwenda Korea Kusini ambako alifungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi hiyo. Kutokana na kongamano hilo, viongozi wa Hyundai walifika nchini kufanya mazungumzo na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kwa lengo la kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vipuri vya magari. Mazungumzo hayo yanaendelea.

Katika kipindi hicho pia Serikali imekuwa mstari wa mbele kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini. Kwa mfano, mwezi Aprili Serikali iliandaa maonyesho ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania yaliyofanyika Nairobi, Kenya. Kampuni 27 kutoka Tanzania zilishiriki ili kutangaza bidhaa zao na kuvutia utalii.

Maonyesho hayo yalitoa fursa kwa wafanyabiashara kutafuta masoko ya bidhaa nchini Kenya.

Kwa kusisitiza diplomasia ya uchumi, Serikali imekubaliana na Misri kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa za nchi hizo mbili. Tayari majadiliano hayo yamekamilika na yataifanya nchi hiyo kuondoa ushuru kwa kiwango cha asilimia 100 na Tanzania iondoe kwa kiwango cha asilimia 96.89. Kiwango kilichosalia kwa Tanzania kitaondolewa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kilimo, miundombinu na utalii

Katika kipindi hiki, Serikali iliratibu upatikanaji wa mkopo nafuu wa dola 55 milioni za Kimarekani kutoka Poland ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maghala na vihenge vya kuhifadhia nafaka katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Rukwa, Songwe, Dodoma, Shinyanga, Manyara na Katavi.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Serikali pia imeratibu upatikanaji wa ufadhili wa mradi wa kituo kikubwa cha ujenzi wa kuzalisha samaki cha Zanzibar unaodhaminiwa kwa ushirika kati ya Korea Kusini kupitia Shirika la Maendeleo (Koica) pamoja na Shirika la Chakula Duniani (Fao) wenye thamani ya dola 3.2 milioni.

Kwa kushirikiana na wadau wengine, Serikali imefanikisha upatikanaji wa ufadhili wa miradi ya umwagiliaji ya Muhongo-Kagera na Bonde la Luiche-Kigoma kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait. Baada ya kukamilika kwa tathmini ya miradi hiyo Machi 2018, rasimu ya mkataba wa kuipa Tanzania mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya dola 15.3 milioni za Kimarekani ulisainiwa.

Aidha, ushirikiano wa Tanzania na China kwa kutumia jukwaa la FOCAC umeendelea kuchangia sekta ya maji na kufanikisha Zanzibar kufadhiliwa mradi wa kujenga kituo kipya cha kutibu maji eneo la Donge Mbiji wilayani Kaskazini Unguja wenye thamani ya dola5.5 milioni.

Kutokana na ombi la kujiunga na mpango wa One Belt One Road Initiative ambao una manufaa mapana katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati, reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege unaoendeshwa na Serikali ya China, Aprili 2018 nchi hiyo ilikubali ombi hilo na utaratibu wa kujiunga na mpango huo unaendelea.

Ofisi za ubalozi zinaendelea kushirikiana na wadau wengine kutangaza vivutio vya utalii na kuratibu ujio wa watalii nchini. Ripoti ya mwezi Mei ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na ripoti za balozi mbalimbali zinaonyesha kwamba idadi ya watalii nchini si tu imeongezeka, bali pia imekuza pato la sekta hiyo. Ongezeko hilo la idadi ya watalii limetajwa kuwa ni matokeo ya kasi ya kuvitangaza vivutio vya utalii inayofanywa na mamlaka za ndani na ofisi za ubalozi.

Sultan wa Oman, Oktoba 2017 alifanya ziara nchini na kuahidi kukarabati na kuhifadhi Jumba la Maajabu (Beit el Ajab) Zanzibar. Aprili, Tanzania na Oman zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya kumbukumbu na nyaraka ili kukuza utalii unaotokana na historia kati ya Oman na Zanzibar.

Sekta ya afya

Kwa kutambua kuwa hakuna maendeleo kama watu hawana afya imara, Serikali pia imetumia diplomasia ya kiuchumi kuvutia wahisani katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi.

Kwa mfano, kutokana na juhudi hizo, Serikali imeishawishi Kuwait kuanzisha mpango wa kusaidia sekta ya afya wenye thamani ya dola 500,000.

Pia mpango wa Dollar Program umewezesha upatikanaji wa vifaatiba kwa watu wenye mahitaji maalumu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.

Aidha, Kuwait imetoa dola 13.6 milioni kwa ajili ya kukarabati Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar. China imesaidia ukarabati wa Hospitali ya Abdulla Mzee (Kaskazini Pemba), wakati Mfuko wa Afya Duniani (Global Fund) unafadhili programu za kukabiliana na malaria, kifua kikuu na Ukimwi.

Diplomasia ya uchumi pia imefanikisha ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi, shahada ya kwanza, uzamili, uzamivu, uboreshaji mafunzo ya ualimu, uboreshaji mitalaa na miundombinu ya kufundishia katika vyuo vya ufundi na teknolojia; vitabu; pamoja na ujenzi wa maktaba ya kisasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).