MFUMO WA UBEPARI NI KIKWAZO CHA UHURU NA UKOMBOZI WA WENGI

Imepakiwa - Friday, December 16  2011  at 10:58

 

Ukombozi wa wengi Kenya utapatikana wakati umma tutakapotoka kwa ndoto na kurudi katika dunia halisi ya harakati za kitabaka na kujizatiti ipasavyo. Ndiyo, sasa tuna katiba ambayo ni bora zaidi kuliko ile iliyokuwa hapo awali. Lakini maisha bora kwa wengi nchini bado yako mbali. Maana katiba mpya ndani ya mfumo wa ubepari haijaweza wala haitaweza kuleta maisha bora kwa wengi. Katiba ya kibepari ilitimiza jukumu lake la kihistoria wakati ilipotumiwa kuondoa mfumo wa ukabaila na kuleta ule wa ubeperi ambao ulikuwa wa kimaendeleo kuliko mifumo ya hapo awali ya utumwa na ukabaila. Bali kutoka wakati huo katiba ya kibepari inalinda mfumo wa kitabaka wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Ninaisoma kwa makini Katiba ya Kenya. Ikisomwa kijuujuu inaonekana kuwa ya watu wote wa Kenya. Lakini ikichambuliwa kwa undani kutoka kwa msimamo wa kitabaka itadhihirika kuwa ya kulinda ubwanyenye kwa kupoza harakati za kitabaka.

Kote ulimwenguni, Kenya ikiwepo, dola la ubepari pamoja na katiba zake linaongozwa na mabepari, itikadi za kibepari na adili za kibepari. Ni la kulinda mfumo wa ubepari ambao umekuwa kikwazo cha uhuru na ukombozi wa wengi siyo to Kenya bali kote ulimwenguni. Kwani mfumo wa ubepari ni wa kitabaka, wa unyonyaji wa mtu kwa mtu, wa mwenye nguvu mpishe mnyonge msonge. Mfumo wa vyama vingi, uchaguzi na utawala wa kidemokrasi ndani ya mfumo wa ubepari ni halali bora tu usilenge kuondoa mfumo wa ubepari. Dola za kibepari hutumiwa kuwanyonya na kuwanyanyasa wafanyikazi, wakulima makabwela na wale wote wasiyo na umilikaji wa viwanda, biashara kuu, mashamba makubwa - njia kuu za uzalishaji. Ni la kuwatawala na kuwagandamiza wale wanaoishi kwa kutegemea ujira, wavujajasho, wakodeshaji nyumba, wale ambao ni mafukara ama walalahoi. Kwa ujanja wake, ambao ni pamoja na kujificha ndani ya katiba na demokrasi ya kibepari, dola la kibepari linaonekana kana kwamba liko kwa ajili ya taifa na kila raia pasina mapendeleo. Bali haijawezakana wala haitawezekana kuwa na usawa kati ya tajiri na maskini. Usawa huo unawezekana tu katika maandishi ya katiba wala siyo katika hali halisi ya maisha.

Kama kawaida ya katiba zote za kibepari, katiba ya Kenya imejaa orodha ya haki za binadamu, kama usawa katika sheria, uhuru wa kusema na kusambaza maoni, uhuru wa kutembea na kujumuika, haki ya matibabu, haki ya kujipatia riziki, haki ya kuwa na nyumba bora, haki ya elimu kwa kila raia, haki ya kuchagua au kuchaguliwa kiongozi, haki za wafanyikazi, haki za watoto, haki za wanawake, haki za walemavu na haki za wazee. Sawa, lakini wakati huohuo katiba inalinda mali ya binafsi na maadili yake ambayo ni msingi wa ubepari. Inaahidi haki na usawa kwa raia wote ndani ya mfumo wa kitabaka, jambo la kuwavisha vilemba vya ukoka wengi ambao ni mafukara na wanaolilia ukombozi.

Msingi wa katiba za kibepari ni kulinda na kuabudu haki ya mtaji na mali ya binafsi. Kwa mfano, mabepari wana haki ya kuwa na mali ya binafsi na kuikuza kwa vyovyote vile hata kwa kuwanyonya na kuwanyanyasa wafanyikazi katika viwanda, makarakana, makampuni, na popote pale penye mitaji yao. Nao mafukara eti wanahakikishiwa na katiba haki ya kuwa mabepari wakitaka. Lakini, utake usitake bila mtaji huwezi kuwa bepari. Huwezi kutoka kwa tabaka la makabwela na kuingia tabaka la mabepari ghafla bin vu ati kwa kuwa tu umeamua kufanya hivyo au kwa sababu unaruhusiwa na katiba. Ukweli ni kuwa uwezo wa mtu kutoka tabaka la mafukara kuingia tabaka la mabepari ni sawa na ule wa ngamia kupitia tundu la sindano. Tukiangazia Kenya tunaona kuwa jamaa za matajiri, zenye kudhibiti uchumi wa pesa, ardhi, biashara na mali tilatila, ni zilezile tu za kutoka kale na zamani. Zinazoongezeka ni zile za mafia wa magendo, walanguzi wa pesa na madawa ya kulevya, wafisadi na waporaji wa mali wa kila aina. Aidha, pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kupanuka nchini kila siku. Chimbuko cha umaskini si kuwa maskini hawafanyi kazi kwa bidii bali ni mfumo unaohakikisha kuwa kazi na bidii ya maskini hana fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi na akishiriki kazi yake inamfaidi tajiri badala ya yeye mwenyewe. Asili ya utajiri wa tajiri nchini si kazi na bidii ya tajiri bali umilikaji wa ardhi na njia ya uzalishaji inayomwezesha kuwanyonya wafanyikazi.

Katiba mpya imewapa wananchi wote haki za matibabu. Lakini kadiri ambapo Kenya itandelea kuwa ya ubepari, matajiri ndiyo watakaondelea kutekeleza haki hii mara nyingi zaidi kuwaliko makabwela na mafukara. Nchini leo, udaktari, mahosipitali na matibabu ni biashara kama biashara yoyote ile inayowatajirisha watu binafsi kwa kuwanyonya wagonjwa. Bila pesa ni muhali kupata matibabu yoyote, sembuse matibabu bora. Adili za udaktari, ambazo ni pamoja na kujitahidi wakati wote kuokoa maisha, hazitekelezwi katika mfumo unaoongozwa na adili ya kuchuma mali kwa vyovyote vile. Elimu pia imekuwa bidhaa kama bidhaa yoyote ile. Wenye hela ndiyo wenye uwezo wa kuwanunulia watoto wao elimu bora zaidi katika shule za binafsi nchini na ughaibuni. Elimu Kenya inatumiwa maksuudi kuzidisha na kuhifadhi utabaka na pengo kati ya matajiri na maskini.

Huku tukiangazia uchaguzi wa kitaifa mwaka wa 2012, ukweli ni kwamba wenye ukiritimba wa ardhi na uchumi wanajipanga usiku na mchana kuhakikisha uchaguzi huo utaendeleza mfumo wa ubepari. Watatumia ukabila na pesa halali na zisizo hali kuwanunua wapigaji kura. Tayari mamilioni yanatumika kila siku kuwahonga wapigaji kura kwa jina la harambee. Sasa ni juu ya watu kutoka tabaka la makabwela, tabaka la wengi, kukumbuka kuwa hawawezi kukomboleo na tabaka la matajiri. Kukataa kuwapigia wazalendo kura na kuwafanya matajiri viongozi kwa sababu za ukabalia, kula hongo, ujinga na kutowajibika ni mwiba wa kujidunga ambao haumbiwi pole.

Add a comment maoni

Share Bookmark Print

Rating

 

 

 

 

 

 

Most Popular