UCHUMI NA BIASHARA
Na PETER MWAI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 14 2012 at 19:30Kwa Mukhtasari
Waziri Shitanda asema wengi wa waliopewa kandarasi wamekuwa wakikosa kuwajibika na kushindwa kukamilisha miradi yao.
WAZIRI wa Nyumba Soita Shitanda ameonya wanakandarasi wa humu nchini kwamba hawatabembelezwa katika utoaji wa kandarasi za Serikali.
Waziri alisema wengi wa waliopewa kandarasi wamekuwa wakikosa kuwajibika na kushindwa kukamilisha miradi yao.
Alikuwa akiongea mtaani Kileleshwa wakati wa kukabidhiwa rasmi kwa nyumba 105 zilizojengwa na Shirika la Kitaifa la Nyumba (NHC) kwa gharama ya Sh800 milioni.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumetoa kandarasi kwa kampuni nne za humu nchini. Ni moja tu iliyomaliza kazi yake. Nyingine tulilazimika kuanza kutafuta watu wa kuzimaliza,” akasema Bw Shitanda.
Mradi huo wa Kileleshwa Park Appartment ulipewa kampuni ya China Wu Yi kutoka Uchina ambayo ilishirikiana na Enderman Properties.
Ujenzi ulimalizika katika kipindi cha miezi 15 pekee. Kampuni za humu nchini huchukua hadi miaka minne kumaliza ujenzi wa nyumba 200.
“Hata kama tungependa sana kukuza kampuni na wawekezaji wa humu nchini, lazima watoe huduma bora na kushindana na China Wu Yi na wengineo,” akasema waziri.
Ujenzi katika kaunti
Aliwatahadharisha wazinduke na kujiimarisha mapema akisema kuna kandarasi nyingi za ujenzi ambazo zitachipuka katika ngazi za kaunti baada ya kuanza kutekelezwa kwa ugatuzi.
“Shida iko kwenye wawekezaji wa humu nchini na hasa Waafrika. Lazima wajikakamue,” akaongeza.
Nyumba hizo za Kileleshwa zimejengwa katika ardhi ya ekari 3.55 iliyomilikiwa awali na Shirika la Reli la Kenya (KRC).
Ardhi hiyo ilikabidhiwa NHC kama sehemu ya malipo ya deni lililodaiwa na shirika hilo miaka minne iliyopita.
Wakati wa kubadilishwa kwa umiliki, ardhi ilikuwa ya thamani ya Sh80 milioni, huku deni likiwa Sh70 milioni.
Kiasi kilichokuwa juu kililipwa kama pesa taslimu.
Kesi nyingi
Katika hafla hiyo ya Jumanne, Bw Shitanda alilalama pia kuhusu kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani kupinga ujenzi wa nyumba akisema zinakwamisha maendeleo.
Alitoa mfano wa mradi wa Kibera wa ujenzi wa nyumba takriban 1,000 za bei nafuu ambao ulisimama baada ya watu kwenda mahakamani.
Miradi mingine imekwama Shauri Moto na katika barabara ya Forest Road.
Wito wake ulikaririwa na Waziri wa Maendeleo ya Maeneo Fred Gumo aliye mbunge wa Westlands ambapo mradi huo wa Kileleshwa umejengwa.
“Nawasihi waliopeleka kesi mahakamani waziondoe. Miradi inayotekelezwa na serikali si ya manufaa yake bali ni ya wananchi,” akasema.
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel