Na NORBERT AMWAYI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Wednesday, February 22 2012 at 16:58Kwa Mukhtasari
Ni wakati viongozi wetu na wananchi kutambua hatari za kupoteza rasilimali hii kama vile hewa safi, mabaki ya mimea na wanyama wa asili au hata miti ya asili ambayo iko mbioni kutoweka.
HUU ni mwaka wa kampeni za kutafuta kuchaguliwa kwa nyadhifa mbalimbali zikiwemo Urais, Ugavana, Useneta, Ubunge miongoni mwa viti vinginevyo, lakini kufikia sasa hakuna mwanasiasa ambaye ameanika wazi sera zake kuhusiana na uboreshaji wa mazingira yetu.
Ni kana kwamba wamesahau umuhimu wa mazingira kwa uchumi wa taifa na kujishughulisha tu na siasa za kuwagawanya wananchi kwa misingi ya kikabila pasi na kujali mazingara ya wanakoishi wananchi wenyewe.
Je viongozi au wanasiasa hawa wanaotafuta kuteuliwa kuongoza taifa hili wanafahamu kuwa umuhimu wa mazingira kwa uchumi wetu una mambo manne muhimu kwa maisha ya mwanadamu?
Jambo la kwanza ni kwamba Mazingira yanaipatia nchi mahitaji yote ya msingi kwa ajili ya kufanikisha masuala ya jamii na uchumi kwa ujumla. La pili ni kuwa Mazingira ndiyo makazi ya viumbe vyote-mimea, wanyama, wanadamu ambao ndio urithi usiokuwa na badala yake. Pia Mazingira ni chombo cha kuweka yale yasiyofaa na mwisho ni kwamba mazingira ni msingi ambao ndio utakuwa jawabu la kupunguza unyonge wa umaskini.
Taifa letu halijaachwa nyuma katika kukumbana na majanga ambayo yametupokonya wenzetu pamoja na mali zao, tatizo la ukame, njaa na ukosefu wa maji ni mambo ambayo yamechangiwa pakubwa na hali ya kutojali ya mwananchi mwenyewe na hata viongozi wetu.
Mengi yanaweza kuepukika
Kwani mengi ya majanga haya ni yale yanaweza kuepukika ikiwa wananchi na viongozi watashikana sako kwa bako na kuhakikisha kuwa sera za kuboresha mazingira yetu zinatekelezwa ipaswavyo.
Utakubaliana nami kuwa ni dhahiri kwamba msukumo mkubwa wa uongozi wa mazingira ni kulinda sehemu asili ya kuishi binadamu na kuoanisha upungufu uliopo kwenye mazingira katika kusaidia kufikia maamuzi yanayohusu masuala na shughuli za uchumi.
Ni wakati viongozi wetu na wananchi kutambua hatari za kupoteza rasilimali hii kama vile hewa safi, mabaki ya mimea na wanyama wa asili au hata miti ya asili ambayo iko mbioni kutoweka.
Swali ambalo nimekuwa nikijiuzila baada ya kuondoka kwake mwendazake mama Professa Wangari Maathai, mazingira yetu yatapata wapi mtetezi mwingine kama yeye?
Professa Maathai alikuwa kiongozi ambaye aliyaweka mazingira ya taifa hili mbele na nchi hii inastahili watu wengine zaidi kama yeye ili kuafikia kiwango bora cha mazingira tunayodhamiria.
Wanasiasa wa sasa wanayaweka tu mbele matakwa yao ya kibinafsi kwa kutoa ahadi ambazo hazilengi kuboresha mahitaji ya mwananchi wa kawaida. Wamesahau kuwa ni dhahiri kwamba uhifadhi na usimamizi wa mazingira duniani na kitaifa una nia ya kushinda matatizo yanayotokana na umaskini, maradhi, hali mbaya na duni ya upatikanaji wa chakula, makazi machafu, maji yasiyo salama, upatikanaji wa nishati usioridhisha na ukosefu wa ajira.
Ni wajibu wa kila mtu
Kuelewa kwa wananchi na watu binafsi juu ya faida za kuhifadhi na kusimamia mazingira ndiyo msingi wa kuendeleza rasilimali na mazingira. Hiyo inakwenda sambamba na utekelezaji wa mipango thabiti ya kuondoa umaskini kwa sababu umaskini unaendana na matumizi mabaya ya rasilimali na uharibifu wa mazingira na hivyo juhudi za kuuondoa umaskini zinahitaji ushirikiano wa jinsia zote.
Serikali itakayofuata ni sharti ifahamu kuwa jukumu la kusimamia mazingira ni wajibu wa kila mtu. Majukumu ya mashirika ya serikali ni kuwasaidia wananchi pale walipo kuelewa hali zao kujisaidia na kuwajibika kuendesha maisha yao. Kitu cha muhimu ni kutayarisha sera, kutunga sheria na mifumo ya kusimamia, pamoja na kuimarisha mipango ya elimu. Zaidi ya hayo, serikali itawajibika kutoa msaada wakati unaofaa na kutoa taarifa sahihi zinazohusu usimamizi wa mazingira.
Kuna sera ambazo zimependekezwa na zinaweza kufanikisha haya ikiwa zitafuatiliwa. Kwa mfano serikali ijayo haina haja kuhakikisha udumishaji, usalama na matumizi sawa ya rasilimali kwa mahitaji ya msingi ya sasa na ya vizazi vijavyo bila kuharibu mazingira au kuhatarisha afya na usalama. Kuzuia na kudhibiti uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambayo ndiyo husaidia mfumo wa uhai wetu. Kuhifadhi na kuendeleza urithi wetu na ule unaotengenezwa na binadamu, ikiwa ni pamoja na maisha ya viumbe wa aina mbalimbali na vya pekee nchini.
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel