Na WAANDISHI WETU, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  12:48

Kwa Muhtasari

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepinga polisi kumfungulia mashtaka ya kuandamana bila kibali mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma.

 

DAR/ TARIME

TAARIFA iliyotolewa Alhamisi na Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, imeelezea kustushwa kukamatwa na kupigwa kwa mwandishi huyo wakati akiwa kazini wilayani Tarime.

Tuma, mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko na wafuasi 14 wa chama hicho walikamatwa juzi kwa tuhuma za kufanya mkutano usio halali. Licha ya kuachiwa jana, walitakiwa kuripoti leo.

Mwanahabari huyo alikuwa akipiga picha katika mkutano wa Chadema uliokuwa ukifanyika katika Kata ya Turwa wilayani humo.

“Mashtaka hayo yafutwe mara moja, polisi wanapaswa kutambua na kuthamini kazi ya uandishi wa habari sawa na wao wanavyofanya kazi ya ulinzi na usalama kwani uandishi ni kazi sawa na kazi nyingine,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

“Tunawasihi polisi kumwachia huru mara moja. Tuma amekamatwa katika mazingira halali ya mwandishi kufanya kazi.”

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa kifungu cha (7)(1)cha Sheria ya Huduma ya Habari (MSA) ya mwaka 2016 kinatambua taaluma ya uandishi habari na kinampa mwandishi haki na wajibu wa kukusanya, kuchakata na kuchapisha taarifa mbalimbali bila kizuizi. “Viongozi waandamizi wa polisi mara kadhaa wamewaahidi waandishi wa habari kuwa wanaheshimu uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wanapokuwa kazini, ila kwa mshangao tumeona Tuma akikamatwa, kupigwa kinyama huko Tarime,” imesema taarifa hiyo.

Kitambulisho cha kazi

Mbali na TEF, Chama cha Waandishi wa Habari za Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (Ojadact), kimesikitishwa na tukio hilo kikieleza kuwa wakati Tuma akikamatwa alikuwa na kitambulisho cha kazi anayoifanya.

Mwenyekiti wa chama hicho, Edwin Soko kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa alisema mbali na kutaka Tuma achiwe, pia wanashauri vyombo vya habari kuwaandalia waandishi vikoti maalumu vinavyowatambulisha wawapo kazini.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema, “nimepigiwa simu nyingi na media (vyombo vya habari) nyingi na waandishi wa habari wakiwamo wa Tarime wakiomba nimwachie lakini polisi tumekataa, huyu amekamatwa akiwa kwenye mkusanyiko uliozuiwa.”

 

Imeandikwa na Kalunde Jamal (Dar), Waitara Meng’anyi na Dinna Maningo (Tarime)