http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

Kinara maonesho ya mavazi aunga mkono kauli ya JPM

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na JAMES MAGAI, Mwananchi jmagai@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  11:53

Kwa Muhtasari

Mwasisi wa fani ya maonesho ya mitindo ya mavazi nchini, Farida Matata amekoleza kauli na msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu mavazi ya staha.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

MWASISI wa fani ya maonesho ya mitindo ya mavazi nchini, Farida Matata amekoleza kauli na msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu mavazi ya staha.

Akizungumzia nafasi ya sanaa hiyo, alipofanya ziara katika ofisi ndogo za gazeti hili, Mtaa wa Samora, Harbour View Tower, mwanzilishi huyo wa maonesho ya mavazi, maarufu Farida Fashion Show, alisema sanaa ya mitindo imepotoshwa na baadhi ya wasanii.

“Nimemsikia hata Rais (John Magufuli) amesema, kizazi cha leo kimepotosha suala la mavazi. Nadhani jamii haina elimu ya kutosha kuhusu mavazi na sioni ‘fashion show’ nyingi siku hizi. Tuvae nguo kulingana na hali na mahali,” alisema Farida.

Mwanzilishi huyo wa maonesho ya mitindo ya mavazi ambaye kwa sasa anaishi Uingereza, alisema anatarajia kufanya onesho la mfano ili kutoa elimu ya mavazi.

Alisema mavazi yana kanuni za uvaaji ambazo zinaelekeza vazi gani livaliwe wakati gani na mahali gani na alisisitiza lazima mitindo ya mavazi ifuate mila na utamaduni wa nchi.

“Wakati mimi nilipokuwa nikionesha mitindo ya mavazi nilikuwa nikitoa elimu, nikielekeza kila aina ya mtindo wa nguo kuwa zina mahali na wakati wake wa kuzivaa,” alisema mwasisi huyo.

Akihutubia mkutano wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Magufuli alielezea kukerwa na namna wasanii hususan wa muziki wa kizazi kipya wanavyovaa mavazi yaliyopoteza maadili.