http://www.swahilihub.com/image/view/-/2539202/medRes/887146/-/la74wh/-/mizani_haki.jpg

 

Majaji wa Zanzibar washauriwa kuzingatia sheria, kanuni

Mizani ya haki

Mizani ya haki. Picha/MTANDAO 

Na HAJI MTUMWA

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  09:36

Kwa Muhtasari

Jaji Mkuu wa Zanzibar amewashauri majaji kuangalia sheria na kanuni ambazo ndizo mwongozo wa kufikia utoaji haki mahakamani.

 

ZANZIBAR

JAJI Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amewataka majaji kutoangalia sura za washtakiwa wakati wa kutoa hukumu.

Badala yake waangalie sheria na kanuni ambazo ndizo mwongozo wa kufikia utoaji haki mahakamani.

Akizungumza wakati wa ziara yake akitembelea mahakama mbalimbali Unguja, Jaji Makungu alisema utumishi uliotukuka katika uendeshaji kesi mahakamani ni kufuata na kutekeleza sheria ipasavyo.

Alisema hatua hiyo ni wazi kuwa itaweza kuondoa lawama za wananchi ambao wanaonekana kukosa imani na kutoamini hukumu zinazotolewa wakiona kama kuna kasoro katika kufikia utoaji uamuzi katika mahakama mbalimbali nchini.   

“Ni vyema katika Idara ya Mahakama  kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuona idara yetu ambayo ni muhimu na tegemeo katika kutoa haki izidi kupata sifa nzuri kwa wananchi,” alisema Makungu.

Nidhamu

Naye Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mohamed Ali Mohamed, aliwataka watendaji kuzingatia nidhamu ambayo ni ngao katika kuongeza uwajibikaji kazini.

Awali, Hakimu wa Mahakama ya Mwanakwerekwe , Mohamed Amour Haji alisema kwa kuwa kazi zao ni muhimu kwa jamii na Taifa watahakikisha watatenda haki kwa wote ili kuondoa malalamiko ambayo yanasababisha wananchi kukosa imani na chombo  hicho cha kutoa haki.