http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842618/medRes/2164326/-/536u5kz/-/masauni.jpg

 

Mabomu yarindima Waziri akihutubia Njombe

Hamad Yusuf Masauni

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Yusuf Masauni. Picha/MWANANCHI 

Na GODFREY KAHANGO na HERIETH MAKWETTA, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  10:03

Kwa Muhtasari

Mjini Njombe kumetokea mauaji ya kikatili kabisa ambapo watoto wapatao 10 ni wahanga wa kisa hiki.

 

NJOMBE, Tanzania

POLISI mjini Njombe, Jumanne walitumia mabomu ya kutoa machozi karibu na eneo ambalo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alikuwa akihutubia wananchi wakati askari hao walipokuwa wakimuokoa mtu aliyeshukiwa kutaka kuteka mtoto aliyekuwa akitoka shuleni.

Katika kipindi cha mwezi mmoja, watoto wapatao 10 wamechinjwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Njombe na wauaji kunyofoa baadhi ya viungo vyao na kutelekeza miili, matukio ambayo yanahusishwa na imani za kishirikiana na visasi.

Mabomu hayo ya Jumanne yalisababisha kuvurugika kwa mkutano wa waziri huyo kwa muda na hali ilipotulia na Masauni kuanza kuzungumza, alimtaka Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Rashid Ngonyani kueleza sababu za kupigwa kwa mabomu hayo.

Akieleza, Ngonyani alisema kulitokea wizi wa pikipiki na mshukiwa alikuwa akifukuzwa na madereva wengine wa pikipiki hivyo na wananchi waliamua kumkimbiza mtuhumiwa huyo huyo jambo ambalo polisi waliliona na kuingilia kati.

Hata hivyo, kamanda huyo alipingwa na wananchi waliopaza sauti wakisema si kweli. Kelele zilizopozidi, Masauni aliwapa nafasi kuele-za kilichotokea.

Alphonce Ndulu na wenzake zaidi ya wanne walisema kilicho-zungumzwa na Kamanda Ngonyani kilikuwa ni kupotosha ukweli. Alisema walipata taarifa kutoka kwa ndugu zao walioko eneo la Mgendela kwamba kuna mtu ameonekana kumbeba mtoto.

Alisema mtu huyo alipoulizwa kama ni mtoto huyo ni wake, alishindwa kutoa jibu sahihi na kumuachia kisha kuanza kutimua mbio.

“Mke wangu amenieleza wakati anatoka shuleni kumchukua mtoto, alimuona mtu mmoja amembeba mtoto ambaye sio wake ambaye alikuwa akilia sana. Baada ya kuulizwa kama ni mwanaye alimuacha na kuanza kukimbia. Watu wa bodaboda ndio wakaanza kumfukuza, ila ajabu askari wakaanza kutupiga mabomu,” alisema Ndulu.

Baada ya maelezo hayo, Masauni alisema hata yeye aliitilia shaka kauli ya Kamanda Ngonyani kwa kuwa wakati mabomu yakipigwa, alipewa taarifa na kaimu mkuu wa kituo cha Polisi Njombe, Kashoraeli Munuo kwamba kuna mtu alikuwa anataka kumteka mtoto na wananchi wakawa wanamfukuza.

“Haiwezekani kaimu OCD aseme hivi huku kaimu RPC naye aseme hivi. Hili jambo halikubaliki tena mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani tena hadharani! Mimi sitakubali kuvuliwa nguo. Ambaye si mkweli kwenye hili tukio nitajua cha kufanya,” alisema Masauni na kushangiliwa na mamia ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Turbo, Njombe.

Katika mkutano huo, wananchi hao walimweleza Masauni kuwa hali bado ni tete kwenye wilaya hiyo kutokana na mauaji ya watoto.

Mmoja wa wananchi hao, Yohana Mgaya alisema ili kukomesha matukio hayo, mtu wa kwanza ni mwananchi mwenyewe kuwa mlinzi kuanzia familia hadi kwenye jumuiya na kushauri kurejeshwa kwa mfumo wa uongozi wa balozi wa nyumba 10.

“Mfumo wa uongozi wa balozi wa nyumba 10 uimarishwe zaidi, kwani huyo atakuwa ni mtu muhimu kujua kila nyumba na watu wake na hata kama kuna mgeni, basi balozi huyu lazima apewe taarifa. lakini msako mkali uendelee kufanyika kwenye nyumba za kulala wageni,” alisema.

Mkazi wa Mji Mwema, Deo Kayombo alisema watu wengi wanaoshukiwa kwa matukio hayo ni vijana ambao wamekimbilia imani za kishirikina kutafuta utajiri kutokana na uvivu wa kufanya kazi halali za kujitafutia kipato.

Kauli ya Serikali

Akitoa msimamo wa Serikali, Masauni alisema macho yote ya Serikali yapo Njombe hivi sasa na tayari imeanza kuchukua hatua ikiwamo ya kuongeza nguvu ya vyombo vya dola.

“Tumeweka mikakati ya kukomesha mauaji haya ya kinyama na kishenzi, lakini ushauri uliotolewa hapa wa kuimarisha mfumo wa uongozi wa balozi wa nyumba 10 ni mzuri na itafanyika hivyo tu,” alisema Masauni. “Pia niwaombe wananchi endeleeni kutoa ushirikiano kwa vyombo vyenu vya dola, tunajua kama mlivyolalamika hapa kwamba hakuna usiri kutoka kwa askari. Kweli hili linavunja nguvu ya wananchi, ila niwahakikishie hatutawanyamazia hawa watu pindi wanapobainika.”

Wakati Masauni akieleza hayo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri alisema Jumanne kuwa matukio hayo katika eneo lake la utawala yanawafanya wananchi kukosa amani.

“Kuteka watoto ni tukio linaloondoa usalama, watu wakikosa amani hakuna usalama.”