http://www.swahilihub.com/image/view/-/3787860/medRes/1545730/-/9psrn4z/-/tesaa.jpg

 

Maisha ya miaka miwili ijayo yatapunguza makali miaka mitatu iliyopita TZ

John Magufuli

Rais John Magufuli akiendesha basi la mradi wa Mabasi Yaendeyo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam Januari 25, 2016 baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya miundombinu na utoaji huduma wa mabasi hayo. Picha/EMMANUEL HERMAN 

Na MWANDISHI WETU, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 31  2019 at  11:28

Kwa Muhtasari

Rais John Magufuli aliingia madarakani Novemba mwaka 2015.

 

IMETIMIA miaka mitatu na ushee tangu Rais John Magufuli alipoingia madarakani Novemba mwaka 2015, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huo.

Tangu aingie madarakani katika miaka yake mitatu, amefanya mengi makubwa yanayopigiwa mfano ndani na nje ya nchi ikiwamo ununuzi wa ndege sita za Serikali huku nyingine mbili zikiwa mbioni kuingizwa nchini. Amefanikisha kukamilika kwa barabara za juu eneo la Tazara ambalo awali lilikuwa na kero kubwa ya foleni iliyokuwa ikiwagharimu wengi kwa ama kuchelewa kufika waendako au kutumia muda mwingi ili kuwahi shughuli zao.

Pia, Rais Magufuli amefanikisha kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa barabara kutoka Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani, ambazo sasa zitakuwa sita lengo likiwa ni kuondoa msongamano.

Hata hivyo, katika miaka mitatu hiyo kumeshuhudiwa pia misimamo mbalimbali ya Serikali ambayo utekelezaji wake ulikuwa mwiba mchungu kwa wananchi.

Hapa tunakuletea mambo manne ambayo katika miaka mitatu iliyopita yalionekana kuwa mwiba mchungu, lakini sasa hali imebadilika ambapo wananchi wataondokana na kilichokuwa kikitafsiriwa ni ‘maumivu’ na kupata ahueni.

 

Bomoabomoa

Ilianza kwa wakazi wa mabondeni. Wale waliokuwa na makazi au kuishi eneo la Bonde la Msimbazi, Dar es Salaam wanakumbuka mambo yalivyokuwa. Walivunjiwa nyumba zao kwa kuwa walijenga eneo lisilo sahihi bila kulipwa fidia na kupewa onyo kwa atakayethubutu kurudi alikoondolewa.

Bomoabomoa ikawafuata waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara, maeneo mbalimbali nchini hususani katika miji mikubwa kama Dar es Salaam wengi walilia.

Waliojenga katika hifadhi ya barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo, walivunjiwa kupisha upanuzi na ujenzi wa barabara. Bomoabomoa hiyo haikuchagua, hata ofisi za Serikali zilizokuwa na majengo makubwa, ya kisasa kama zile za wizara ya maji, Tanesco na Tanroards Mkoa wa Dar es Salaam zilizokuwa Ubungo nazo zilikwenda na maji. Nyumba za walala hoi na hata za ibada nazo hazikusalimika.

Baada ya yote hayo, hatimaye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hakutakuwa na bomoabomoa kauli ambayo ni faraja baada ya miaka mitatu iliyopita kushuhudia wengi wakivunjiwa na kusababisha maumivu.

Lukuvi akiwa ziarani Simanjiro mkoani Manyara, mapema mwezi huu, alisema Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela.

Alisema Rais Magufuli ametoa fursa kwa wananchi wote masikini waishio mijini waliojenga bila ya kufuata mipango miji na hawana hatimiliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi yao na wasibomolewe nyumba zao kwa kuwa haikuwa makosa yao kujenga maeneo hayo.

Zaidi ya hilo matumaini ya kutumia barabara hasa kwa wakazi wa Kimara na wale wanaosafiri mikoani ni kubwa na kinachotarajiwa hapo ni kutokuwapo kwa foleni katika eneo hilo.

 

Suala la Ma-RC, Ma-DC kuwaweka watu ndani

Rais Magufuli amewahi kusikika mara kadhaa akiwaagiza wakuu wa wilaya (ma-DC) na wakuu wa mikoa (ma-RC) kutomchekea yeyote kati ya wale wanaowasimia au wananchi wanapoonekana kutaka kukwamisha maendeleo ya jamii ya nchi.

Kauli hiyo ilipokewa vyema na wakuu wengi wa wilaya na mikoa ambao wameonekana kuwa wakali katika maeneo yao hususani kwa watu wanaokuwa kikwazo kufikia maendeleo ya wilaya au mkoa husika

Hata hivyo, wapo baadhi ambao ama walielewa tofauti au kwa hulka zao waliamua kuzidisha kipimo agizo la kusimamia maendeleo na kutumia rungu la kisheria walilonalo la kuweza kumuweka mahabusu mtu yeyote ndani ya eneo lao na kuwaweka ndani wanasiasa au viongozi wenzao.

Ipo mifano mingi juu ya hilo ikiwamo iliyotokea mkoani Kilimanjaro ambako baadhi ya wakuu wa wilaya walifikia hatua ya kuwaweka ndani wakuu wa idara na katibu wa CCM wa wilaya.

Hilo lililalamikiwa mno, walianza wananchi, wakaja viongozi wakiwamo wanasiasa, mawaziri na juzi Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akatoa yake kukemea tabia hiyo.

Mwishowe Rais Magufuli akapigilia msumari kwa kutaka busara itumike kwa viongozi hao badala ya kutumia mwanya walionao kisheria kuwasweka watu ndani, watumie hekima kutafuta suluhu ili kuongeza kasi ya uchapaji kazi.

Rais Magufuli wakati akiwaapisha viongozi aliowateua mapema wiki hii, Ikulu jijini Dar es Salaam, juzi, alisema wakuu wa wilaya hawapaswi kutumia vibaya sheria ya kuweka watu ndani bila ya kuwapeleka mahakamani.

 

Vijiji vilivyoingilia hifadhi kutoondolewa

Jambo hili halikuanzia katika awamu ya tano, lakini tangu ilipoingia madarakani iliendelea kusimamia sheria inayotaka wananchi kutoingilia maeneo ya hifadhi za taifa. Operesheni mbalimbali zimefanyika kuwaondoa wavamizi katika mapori ya akiba ambako walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali kama makazi, kuchunga mifugo, kilimo na shughuli nyingine.

Ziliendeshwa operesheni kuwaondoa wavamizi katika mapori ya Kimisi na Burigi kwa upande wa mkoa wa Kagera, pia ilifanyika hivyo katika mikoa mingine ukiwamo wa Tabora.

Hata hivyo, Januari 15, mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu wa wizara ya maliasili na utalii walioongozwa na waziri wake, Dkt Khamisi Kigwangalla ambapo aliagiza kutoondolewa kwa vijiji vyote 366 vilivyobainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi, badala yake wizara husika zianze kufanya mchakato wa kuvirasimisha.

Alisema ili kukamilisha jambo hilo wizara ya maliasili na utalii inapaswa kuangalia upya uwekaji mipaka ya hifadhi na makazi kwa kutumia busara ili kuwaondoa wananchi katika maeneo ambayo hawana ulazima wa kuondolewa.

Rais Magufuli alisema hafurahii kuona wafugaji wakifukuzwa, hivyo akaagiza kuangalia kama kuna eneo ambalo awali lilikuwa ni kwa ajili ya wanyama lakini halitumiki, sheria ibadilishwe, limegwe na kuligawa kwa wafugaji.

 

Ombi la kukutana na viongozi

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu na Rais Magufuli kuibuka mshindi, kuingia Ikulu, wananchi, viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini na siasa waliomba kukutana naye ili kupata fursa ya kujadiliana naye mambo mbalimbali kwa ajili ya mustakabali wa Taifa.

Huenda waliokuwa wakiomba jambo hilo walizoea utamaduni uliokuwa ukitumika na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipokuwa Ikulu ambapo alitoa fursa ya kukutana na makundi mbalimbali likiwamo la wanasiasa.

Hata hivyo, Rais Magufuli licha ya kukutana na makundi mengine mengi, kusikiliza mawazo yao na kujadili mambo ya maendeleo, lakini hajawahi kufanya hivyo kwa wanasiasa (kama kundi) ijapokuwa wapo mmoja mmoja waliowahi kupata fursa hiyo akiwamo Mbunge wa Vunjo, James Mbatia.

Baada ya miaka mitatu, hatimaye Rais Magufuli Januari 23, mwaka huu alikutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini Ikulu, Dar es Salaam ambapo walipata fursa ya kuzungumza na kujadili mambo ya maendeleo wakiwasilisha kero zinazolalamikiwa na Watanzania ikiwamo ya kutopata fursa ya kupaza sauti.

Rais Magufuli aliwasikiliza na kujibu hoja zilizokuwa na majibu ya moja kwa moja huku nyingine akitoa maagizo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa azishughulikie ikiwamo ile ya kuliangalia suala la kamari katika jamii.

Wengi walipongeza na kufurahia uamuzi wa Rais kukutana na kundi hilo muhimu huku pia wakiamini ni mwelekeo mzuri na kwamba huenda sasa akatoa nafasi kama hiyo kwa wanasiasa.

Kubadilika kwa mwelekeo wa mambo manne hayo kunaashiria kufunguka kwa fursa na kubadilika kwa mambo yaliyokuwa yakionekana vikwazo ambapo sasa wakati Rais Magufuli akielekea kukamilisha muhula wake wa kwanza wa urais, ndani ya miaka miwili ijayo mambo yatazidi kunoga na Watanzania kusahau ‘ugumu’ walioupitia miaka mitatu iliyopita.

Licha ya mambo manne hayo kuonekana kubadili mwelekeo, lakini yapo mengine yanayoendelea kutekelezwa kwa kasi ileile tangu aingine madarakani likiwamo la kuwalinda wafanyabiashara wadogo (machinga) ambao Serikali ya awamu ya tano imekuwa ya neema kubwa kwao.

Mbali na Rais mwenyewe kusimama imara kuhakikisha hawabughudhiwi na kupewa fursa ya kufanya biashara zao maeneo mbalimbali ya mijini yakiwamo yale ambayo huko nyuma walikuwa wakitimuliwa, sasa Serikali imekuja na mkakati wa kuwaongezea usalama wa shughuli zao kwa kuwaandalia vitambulisho maalumu wanavyolipia TSh20,000 kwa kila kimoja ili kuwatambua.