http://www.swahilihub.com/image/view/-/4395920/medRes/1940659/-/3een2w/-/banu.jpg

 

Suala la Basilla Mwanukuzi na mambo ya Miss Tanzania

Basila Mwanukuzi

Basila Mwanukuzi kwa sasa ndiye mratibu wa Shindano la Miss Tanzania. Picha.MAKTABA 

Na MWANASPOTI

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  13:35

Kwa Muhtasari

Mara ya kwanza, mashindano haya yalipigwa marufuku mwaka 1968 na Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanu (Tanu Youth League).

 

JUZI kati hapa, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, DK Harrison Mwakyembe aliyapiga marufuku mashindano ya Miss Tanzania.

Lakini ngoja nikupe hii.

Mara ya kwanza, mashindano haya yalipigwa marufuku mwaka 1968 na Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanu (Tanu Youth League) lakini si kwa sababu ya zawadi.

Tanu iliyapiga marufuku kwa kuwa si ya kimaadili ya Tanzania, wasichana walivaa nguo fupi ndiyo walioshiriki na miaka hiyo, haikutakiwa. Si mashindano ya mamisi tu, klabu za usiku zilifungwa, madisko yote ni kwa ajili ya kujenga utamaduni wa Mtanzania.

Achana na habari hiyo, mwaka 1994, ngoma ikaanza upya. Mashindano yalizinduliwa pale Whitesands Hotel na mrembo wa kwanza tangu kufufuliwa alikuwa Aina Maeda.
Mwaka uliofuatia akaja, Emily Adolf, 1996 (Shose Sinare), 1997 (Happiness Magesse), 1998 (Basila Mwanukuzi) ikaendelea hiyo.

Ile ya ndani kabisa

Iko hivi. Kama unadhani tukio la kudhulumiwa zawadi katika shindano la Miss Tanzania, lilitokea kwa Miss Tanzania mwaka 2016/17, Diana Edward, utakuwa unajidanganya.

Matukio kama hayo ndiyo yaliyosababisha Septemba 25 mwaka jana, Serikali kupitia waziri wake, Dkt Mwakyembe kuyapiga marufuku mashindano hayo.

Dkt Mwakyembe katika kuyafungulia alitoa masharti kwa atakayekuwa tayari kuyaandaa mashindano hayo kuhakikisha zawadi wanazoahidi kuwapa washindi zinawekwa kabisa ofisini kwake.

Tukio hilo pia kwa taarifa yako lilishamtokea Basila Mwanukuzi ambaye kwa sasa ndiye mratibu wa Shindano la Miss Tanzania baada ya kutangazwa Februari mwaka huo na kampuni ya 'Lino International Agency’ iliyokuwa ikiandaa mashindano hayo kwa miaka zaidi ya kumi.

Mkurugenzi wa Lino, Hashim Lundenga, alipotangaza uamuzi huo, moja ya maneno aliyoyasema ni kudai uamuzi huo umetokana na malengo yao ya kutaka mashindino hayo kusimamiwa na damu changa kwa lengo la kuleta chachu katika tasnia ya urembo nchini.
Dalili mbaya kwa Lino zilianza kuonekana tangu mwaka 2014 kulipotokea sintofahamu ya mshindi wa shindano la Miss Tanzania ambapo ushindi alipewa Sitti Mtemvu na baadaye kubainika hakupaswa kupewa kutokana na kudanganya umri wake na shindano hilo kuanza kupoteza mvuto kwa wadau wa masuala ya urembo.

Mitandaoni

Sakata hiyo ilikuwa gumzo nchini hadi kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadaye mrembo huyo alikubali kulivua taji hilo na kukabidhiwa mshindi wa pili Lilian Kamazima.

Hata hivyo, katika kupania kulirudisha shindano hilo kwa nguvu zote, Aprili 7, 2018, Basila kupitia kampuni yake ya ‘The Look’ ilizindua shindano hilo hafla ilifanyika ukumbi wa makumbusho Jijini Dar es Saalam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa Dk. Mwakyembe.

Katika hafla hiyo, mojawapo ya mambo aliyopania Basilla ni kurudisha heshima ya shindano hilo na suala zima la kupatikana kwa zawadi kwa washindi watakaoibuka kidedea kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.

Ili kudhibiti hili anasema ameanza na kufuta shindano la Miss Vitongoji ambapo huko haswa ndiko kuna ubabaishaji mkubwa na kama mtu hatafanikiwa kupata udhamini zawadi inakuwa shida na wakati mwingine hata kuahirisha shindano wakati warembo wanakuwa tayari wameshatumia gharama nyingi katika kujiandaa na hivyo kuwakatisha tamaa.

Badala yake anasema shindano hilo litaanzia ngazi ya mkoa na kisha Taifa, ambapo Dar es Salaam tofauti na mikoa mingine yenyewe itakuwa na mikoa mitano ambayo ni Wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, Kigamboni na Ubungo.
“Kama mnavyojua niliwahi pia kuwa Miss Tanzania na nilibabaishwa katika kupata zawadi yangu mpaka pale mama yangu alipoingilia kati, sasa ninaahidi kulisimamia jambo hili kwa nguvu zote,” alisema Mwanukuzi.

Serikali yaahidi mazito

Katika hotuba yake, Waziri Mwakyembe aliwahi kuwaza kutaka kulifuta kabisa.

Hata hivyo anasema wamekaa na Basilla na kuzungumza naye, wameona mwelekeo wa yeye kutaka kulirudishia heshima yake.

Pia katika serikali kuweka mkono wake, Waziri huyo anasema watamsadia kutafuta wadhamini pale atakapokwama ikiwemo kuzishirikisha taasisi za serikali.
Wakati kwa upande wa Mamiss, anasema angependa kuona wakishamaliza shindano hilo wanapata ajira moja kwa moja kama lilivyo lengo mojawapo la uanzishwaji wa shindano hilo ambapo anaahidi kuongea na Shirika la Ndege Tanzania(ATCL) badala ya kutafuta warembo mtaani wawachuke wanaotoka Miss Tanzania.

“Binafsi naona warembo wanaoshiriki shindano la Miss Tanzania wana kila sababu ya kuajiriwa katika shirika hilo ukizingatia kwamba wana miondoko ambayo inatakiwa kwa wahudumu wa ndege pia waliojiendeleza zaidi kielimu. Kinachotakiwa ni kwenda kufanyiwa mafunzo ya miezi mitatu au minne katika chuo chetu cha usafirishaji (NIT) na kuajiriwa, kwani tunataka kuona mashindano haya yanakuwa chanzo cha ajira na hatuoni haja ya kuajiri watu wengine wakati watoto wetu wapo,” anasema.

Wasikie warembo wenyewe

Katika uzinduzi huo wadau mbalimbali waliweza kutoa maoni yao akiwemo mbunifu wa mavazi, Ally Rehmtullah aliyefanya kazi na waratibu wa mashindano hayo kwa miaka minane sasa kwa kuwavalisha washiriki, anasema anatarajia kuona vitu vikubwa zaidi na warembo bora.

Rehmtullah anasema mambo ambayo angependa yafanyiwe kazi ni pamoja na kuwepo kwa uratibu mzuri ikiwemo suala zima la shughuli kuanza kwa muda, kwani miaka ya hivi karibuni utaratibu huo haukuwa mzuri kiasi cha kukera watu.

Mdau mwingine ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2016, Diana Edward anasema katika uzinduzi huo ameona dalili nzuri ikiwemo suala zima la wadhamini.