http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759154/medRes/2109561/-/pixivk/-/kiudune.jpg

 

Masheha wapewa mtihani usajili wa vitammbulisho vya Mzanzibari

Ayoub Mohammed Mahmoud

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud. Picha/MAKTABA 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  12:53

Kwa Muhtasari

Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar watoa mafunzo kwa masheha

 

VISIWANI ZANZIBAR

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka masheha kuwahamasisha wananchi kujisajili ili kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari kutoka Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar.

Mahmoud alisema kwamba lengo la kujisajili ni kuhakikisha taarifa za wananchi zinapatikana na kuwekwa katika mfumo maalumu utakaokuwa rahisi kwenye matumizi ya kijamii na kiserikali.

Mahmoud alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa masheha kuhusu usajili wa vitambulisho, yanayotolewa na ofisi ya wakala huo, huko Rahaleo Mjini Unguja.

Alisema mfumo wa usajili kwa njia ya teknolojia una umuhimu mkubwa katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo masheha wana nafasi ya kusimamia shughuli hiyo.

Mahmoud alisema kwamba lengo la kutolewa elimu hiyo kwa masheha ni kuondoa migongano baina yao na wananchi wakati kazi hiyo ikiendeshwa katika shehia zao.

Haki ya kila mwananchi

Mwanasheria kutoka Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii Zanzibar, Hamid Haji Machano alisema kwamba kwa mujibu wa taratibu za kisheria kila mwananchi ana haki ya kusajiliwa katika shughuli hiyo.

Alisema kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana ofisi yao imeona kuna umuhimu mkubwa wa kuwapatia masheha mafunzo hayo ili wapate elimu sahihi kuhusu usajili huo na malengo ya Serikali.

Sheha wa Shehia ya Mlandege, Nassor Mohamed alisema hawana tatizo lolote kuhusu uhamasishaji wananchi kushiriki usajili huo.

Alisema kuwa mara nyingi matatizo hutokea wakati wananchi wanapoingiza masuala ya kisiasa katika shughuli mbalimbali.