Mradi wabainisha michezo ni mbinu mbadala kupunguza utoro shuleni

Na IMANI MAKONGORO

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  13:41

Kwa Muhtasari

Serikali imekwenda mbali zaidi na kukiri kuwa katika shule 43 ambazo ziko kwenye mradi wa PAQE unaoratibiwa na Shirika la “Right to Play” utafiti unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi ambao waliacha shule wamerejea baada ya kuwapo kwa vipindi vya michezo.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

KAMA bado uko katika zama za kufikiria michezo ni afya na mshikamano basi pole kwani Serikali kupitiia Ofisi ya Rais Tamisemi imekiri kuwa michezo shuleni imesaida kuwarejesha darasani wanafunzi watoro.

Serikali imekwenda mbali zaidi na kukiri kuwa katika shule 43 ambazo ziko kwenye mradi wa PAQE unaoratibiwa na Shirika la “Right to Play” utafiti unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi ambao waliacha shule wamerejea baada ya kuwapo kwa vipindi vya michezo.

Akizungumza katika semina ya wadau wa michezo na elimu iliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Shirika la ‘Right to Play', Katibu wa Tamisemi Idara ya Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bernadetha Thomas alikiri kuwa michezo ni nguzo mojawapo muhimu ya kufundisha shuleni.

“Hakuna ubishi kuwa kupitia njia ya michezo watoto wamejengewa uwezo nzuri darasani lakini pia tafiti mbalimbali zinaonyesha utoro shuleni umepungua na hata wale walioacha shule kwa asilimia kubwa wamerejea darasani kutokana na mradi wa PAQE,” alisema.

MEneja wa mradi wa ‘Right to Play’ Tanzania, Maria Mongi, alisema mradi huo ulilenga kuwasaidia wanafunzi kuwa karibu na walimu wao kupitia michezo inayosema kuwa ‘mtoto akicheza dunia inafanikiwa’.

“Tulichokifanya ni kuangalia changamoto za watoto. Hivyo tukaanzisha utaratibu wa kuwaweka karibu na walimu kupitia michezo na tuliunda timu za shule ambao watoto walishindana katika michezo mbalimbali kama riadha, kikapu, wavu, netiboli na michezo mingine mingi.”

Kwa kweli mafanikio yalionekana kwani kuna watoto ambao waliacha shule lakini baada ya kuanzishwa kwa mradi huu walirudi shuleni na wanaendelea na masomo yao.

Wamekuwa wakifanya vizuri kitaaluma pia.

Mkurugenzi wa ‘Right to Play’ Tanzania, Josephine Mukakalisa alisema mradi wa PAQE unafanyika kwenye shule 93 nchini ambazo 66 ni za Mkoa wa Mara, 12 za Dar es Salaam na zinazobaki ni za Morogoro na Pwani.