http://www.swahilihub.com/image/view/-/4680862/medRes/2057323/-/r1fcbmz/-/inaka.jpg

 

Mswada wa vyama vya siasa wapita wabunge wa CCM na upinzani wakivutana

Jenista Mhagama

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) nchini Tanzania, Bi Jenista Mhagama. Picha/MWANANCHI 

Na SHARON SAUWA, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  09:49

Kwa Muhtasari

  • Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 uliwasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliyeuita kuwa ni kiboko

  • Kabla ya kupitishwa, uliibuka mvutano mkali kati ya wabunge wa upinzani na CCM

 

DODOMA, Tanzania

MSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 ulipitishwa Jumanne bungeni, Dodoma.

Kabla ya kupitishwa kwa mswada huo uliowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliyeuita kuwa ni kiboko, kuliibuka mvutano mkali kati ya wabunge wa upinzani na CCM.

Baada ya kupitishwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema, “Kilichobaki tutaupeleka kwa Mheshimiwa Rais ili akiridhia ausaini uwe sheria.”

Awali, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipendekeza kurekebishwa au kufutwa kwa maeneo saba makubwa huku Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ukiwataka wabunge kuukwamisha.

Mswada huo umepita huku Taasisi sita za kiraia zikiongozwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), zikiwa zimetoa onyo kuwa hakuna mtu aliye salama endapo utapitishwa.

Taasisi hizo zinajumuisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Centre for Strategic Litigation na Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza).

Waziri Mhagama alisema pamoja na mambo mengine, mswada unalenga kumpa uwezo Msajili wa kuhakiki chama cha siasa wakati wowote. “Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili,” alisema.

Hata hivyo, Ester Bulaya akisoma maoni ya kambi ya upinzani alisema kifungu kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya chama kitapunguza uhuru wa vyama kufanya chaguzi bila shinikizo.

Alisema kifungu kingine ni kinachotoa masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia hakikutilia maanani kuwa vyama vya siasa vina uhusiano wa kiitikadi na vyama rafiki kutoka nje ya nchi.

Bulaya ambaye ni mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) alisema Katiba inatoa masharti ya mtu anayetaka kugombea urais na umakamu wa Rais wa Tanzania kwamba anatakiwa kuwa raia kwa kuzaliwa lakini masharti hayo hayakuwekwa kwa wazazi wake.

“Kambi ya upinzani inahoji kwa nini mtu anayegombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa Taifa hili wazazi wake hawawekewi masharti ya uraia na Katiba iweje mtu anayetaka kusajili chama cha siasa awekewe masharti hayo?” alihoji.

 

Mvutano ulivyokuwa

Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, akichangia muswada huo alisema katika ibara ya 8 c ya muswada huo kuna uvunjwaji wa Katiba.

Alisema muswada huo unataka kufutwa kwa chama ambacho kitashindwa kuwa na kumbukumbu ya wanachama wake wakati Katiba imeeleza mazingira ambayo yanaweza kukifanya chama kufutwa.

Mdee aliungwa mkono Mbunge wa Tanga Mjini (CUF) Mussa Mbarouk aliyewataka wenzake wa CCM kutambua kuwa ipo siku nao watakuwa chama cha upinzani na kwamba sheria hiyo itawahusu.

Hata hivyo, Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema muswada huo ndio muarobaini wa kuondoa uhasama unaotokana na vyama vya siasa, “Ilifika hatua vijana wetu badala ya kutulinda wanageuka kuwa wana mgambo au Al Qaeda, tunakwenda katika uchaguzi vijana wanamwagiana tindikali, wanakatana masikio, migongo. Hii sheria inakwenda kuondoa hawa Mungiki,” alisema.

Mbunge wa Madaba (CCM) Joseph Mhagama aliwataka wabunge wa upinzani kuacha upotoshaji juu ya muswada huo akisema unalenga kuweka uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa vyama vya siasa.

 

Kufutwa, kurekebishwa

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wake, Mohamed Mchengerwa alipendekeza kurekebishwa au kufutwa kwa maeneo saba makubwa ambayo aliyataja kuwa ni masharti ya kuzuia ufadhili holela kutoka nje ya nchi kwa vyama vya siasa na umuhimu wa kutumia Mfuko wa Baraza la Vyama vya Siasa.

Mengine ni uainishaji mzuri wa majukumu ya Msajili tofauti na ilivyo katika sheria ya sasa na pamoja na kuainisha jukumu la usimamizi wa chaguzi ndani ya vyama vya siasa. Pia alizungumzia, zuio la vyama vya siasa kuwa na vikundi vya ulinzi akitaka vipate haki ya ulinzi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Alitaja uainishaji wa masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika katiba za vyama vya siasa ikiwemo mgawanyo mzuri wa kufanya maamuzi kwa vyombo mahususi ndani ya vyama husika na uainishaji mzuri wa masharti ya vyama kuungana na kuunda ushirika pamoja.

Pia alitaja maeneo yote ambayo yamekinzana na msingi ya Katiba ya nchi sheria ya vyama vya siasa au sheria nyingine za nchi.