Muundo wa ukusanyaji kodi ubadilishwe

Haji Semboja

Profesa Haji Semboja. Picha/MAKTABA 

Na PROFESA HAJI SEMBOJA

Imepakiwa - Thursday, July 13  2017 at  11:46

Kwa Mukhtasari

Taarifa ya makusanyo ya Serikali iliyotolewa na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) juzi imebainisha sababu nyingine ya kutekelezwa kwa theluthi moja tu ya bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

TAARIFA ya makusanyo ya Serikali iliyotolewa na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) juzi imebainisha sababu nyingine ya kutekelezwa kwa theluthi moja tu ya bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha.

Kwa mwaka mzima ulioisha Juni 2017, TRA imekusanya TSh14.4 trilioni ikiwa ni pungufu ya Sh700 za lengo Sh15.1 trilioni. Pamoja na kutofikiwa kwa lengo, TRA imesema makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 7.6 jambo ambalo linaelezwa kama si la kujivunia.

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Haji Semboja amesema makusanyo hayo yanaakisi vyanzo vinavyowategemea watu wachache.

Amesema kiasi kilichopanda ni kioo cha uchumi wenye wigo mdogo wa ulipaji kodi kwa kuwa takriban asilimia 70 ya Watanzania walipop vijijini hawalipi kodi licha ya kipato wanachotengeneza.

Katika ripoti yake kwa umma iliyotolewa juzi na TRA ilisema mapato ya kodi yaliongezeka kutoka Sh13.3 hadi 14.4 trilioni mwaka 2016/17.

“Kuna haja ya kubadili muundo wa ukusanyaji wa kodi kwa kuwa sehemu kubwa ya uchumi haijarasimishwa,” alisema Profesa Semboja.

Kwenye muswada wa fedha uliopitishwa bungeni hivi karibuni sheria imependekeza kurasimishwa kwa wafanyabiashara ndogondogo kuanza kulipa kodi kwa taasisi za kijamii (NGO’s) na wachimbaji wadogo wa madini.

Kwa sasa mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ni asilimia 13 ya Pato la Taifa (GDP) yanatokana kati ya asilimia nne na tano ya watu na taasisi zinazoekeleza wajibu huo huku wananchi wengi wakilipa lile Ongezeko la Thamani (VAT)

“Ukusanyaji wa kodi unatakiwa ifikie asilimia 18 ya GDP. Wazalishaji na wawekezaji wengi hawalipi,” alisema.

Kuhusu kutotekelezwa kwa bajeti kwa kiasi kilichotarajiwa kumeathiri miradi mingi ya maendeleo. Taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango ilieleza kuwa hali hiyo ilitokana na kuchelewa kwa fedha zilizoahidiwa na wahisani na Serikali kutokopa kutoka taasisi za kimataifa.

Kutofikiwa kwa lengo la TRA kunadhihirisha upungufu wa fedha za kufanikisha bajeti iliyopita.

Mbunge wa Vwawa(Chadema) David Silinde alisema takwimu zilizotolewa na TRA ni za jumla kwa sababu hazijaainisha vyanzo vilivyochangia mapato hayo.

Alikumbusha kwamba miaka miwili iliyopita TRA imepewa vyanzo vilivyokuwa chini ya Halmashauri ikiwamo kodi ya maendeleo na makusanyo ya mashirika ya umma.

“Kama vyanzo hivi visingeigizwa basi kiwango hicho kisingefikiwa.TRA hawajapanua wigo wa ukusanyajiwa mapato. Chanzo pekee kilichoboreshwa ni kodi ya mafuta,” alisema Silinde ambaye ni Naibu Waziri Kivuli wa Fedha.

Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipitisha bajeti ya Sh29.5 trilioni lakini ni asilimia 80 tu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani uliofanikishwa. Kwenye bajeti ya Sh31.7 trilioni kwa mwaka huu, TRA inakusudia kukusanya Sh17.1 trilioni.