Polisi wakanusha kushikilia mashoga Zanzibar

Na MUHAMMED KHAMIS, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  11:32

Kwa Muhtasari

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassan Suleiman amesema vijana 10 wanaoshikiliwa na jeshi la polisi ni kutokana na kutuhumiwa kwa uhalifu na si ushoga.

 

VISIWANI ZANZIBAR

BAADA ya kuenea taarifa za kukamatwa watu 10 katika shehia ya Pongwe wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja kwa madai ya kujihusisha na matendo ya ushoga, Jeshi la Polisi limekanusha taarifa hizo.

Akizungumza Alhamisi na Mwananchi, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman alisema vijana 10 wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni kutokana na kutuhumiwa kwa uhalifu na si ushoga.

Alisema polisi hawana ushahidi wowote hadi sasa ambao unaweza kuthibitisha vijana hao kuwa wanajihusisha na vitendo vya ushoga kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Kamanda Suleiman alisema vijana hao wamekamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Pongwe kuwa wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo polisi walikwenda na kufanikiwa kuwakamata 10 ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya Unguja na baadhi walifanikiwa kukimbia.

Alisema hadi sasa wanawashikilia vijana hao kwa ajili ya kuwahoji na iwapo watabainika kuwa na tuhuma zozote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao.

Kuhusu iwapo jeshi hilo litataka kujiridhisha na madai ya baadhi ya watu wakiwahusisha na vitendo vya ushoga, Kamanda Suleiman alisema polisi hawafanyi kazi kwa matakwa ya watu bali kwa mujibu wa sheria.

“Hatutakuwa tayari kuwapima kwa lengo la kutambua wanafanya matendo ya ushoga au hawafanyi wakati tuhuma dhidi yao zilikuwa ni kufanya vitendo vya uhalifu inakuaje tufanye mengine yasiyokuwa kwenye tuhuma zao?’’ alihoji.

Dalili za ushoga

Aidha, kamanda huyo alisema wakati jeshi hilo lilikwenda kwenye maeneo ya fukwe za Pongwe ambazo vijana hao na wenzao walikuwapo, hawakuona dalili za kufanya matendo yoyote yale ya ushoga kama inavodaiwa na baadhi ya watu visiwani hapa.

Aliitaka jamii kuepuka kusambaza taarifa zisizokuwa sahihi kwani licha ya kuwachafua wahusika lakini pia zinaichafua Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa vijana ambaye alifanikiwa kutoka kwenye mtego huo wa polisi kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema hawakwenda kwenye fukwe za kijiji hicho kwa ajili ya kufanya uhalifu kama inavyodaiwa.

“Ngoja niseme ukweli tulikwenda kama kujifurahisha kule Pongwe na wenzetu ambao wanashikiliwa lakini tukiwa tunaendelea kuogelea ghafla tulishangaa tunavamiwa na polisi bila ya sisi kujua lolote lile linaloendelea,’’ alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrisa Kitwana aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapowaona watu wasio wa kawaida kwenye maeneo yao ili kudhibiti vitendo vya uhalifu.