http://www.swahilihub.com/image/view/-/4911580/medRes/1748042/-/p9w0eaz/-/lissu.jpg

 

Sakata ya matibabu ya Lissu yaibuka upya

Tundu Lissu

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu. Picha/AFP 

Na WAANDISHI WETU, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  10:59

Kwa Muhtasari

Tundu Lissu asema alistahili kulipiwa ada za matibabu na bunge la kitaifa.

 

DODOMA/DAR

UNAWEZA kusema sakata ya gharama za matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, imeibuka upya baada ya Alhamisi Spika Job Ndugai kusema Bunge limemlipa stahiki zake zinazofikia TSh250 milioni, huku mbunge huyo akisema mhimili huo wa dola haujawahi kutoa hata senti moja ya kugharimia matibabu yake.

Ndugai ametoa kauli hiyo kipindi ambacho Lissu anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma.

Tangu wakati huo mbunge huyo, familia yake pamoja na chama chake - Chadema wamekuwa wakiulalamikia uongozi wa Bunge kutogharimia matibabu.

Lakini jana baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni, Spika Ndugai alisema hadi mwishoni mwa Desemba mwaka jana, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu ya mbunge huyo.

Alisema kwa jumla hadi sasa Lissu amelipwa Sh250 milioni kutoka bungeni.

“Siku za mwanzo sikutaka kujibu maana niliamini kumjibu mtu aliyelala kitandani siyo vizuri kwani kuna vitu huenda vingekuwa vimempita, lakini sasa naamini ni mzima hadi anafanya ziara nje. Nalisema hili akijibu nakuja na mkeka hapa,” alisema Ndugai.

Kulalama

Alisema mbunge huyo amekuwa akilalamika kila wakati kuwa Bunge halimjali kitu ambacho hakina ukweli ndani yake na hakuna madai kama hayo.

Hata hivyo, Lissu akizungumza na Mwananchi alisema, “Kama Bunge limetoa senti hata moja ya matibabu yangu (Spika) aweke huo mkeka, na hizo (Sh43 milioni ni) fedha za michango ya wabunge si ya Bunge ni michango ya hiari.”

Alisema, “Pesa pekee ninayolipwa ni mshahara na posho zangu za kila mwezi kama mbunge tu. Hizo wanalipwa wabunge wote hata yeye (Ndugai) akiwa India alikuwa analipwa, walioko bungeni au walioko matibabuni.”