Sakata la Madini lapeleka msururu wa vigogo Takukuru, uchunguzi waanza Mwadui

Na ELIAS MSUYA na MUSA JUMA

Imepakiwa - Tuesday, September 12  2017 at  16:29

Kwa Mukhtasari

Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) inawahoji vigogo wa Serikali wakiwemo walikokuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti huku polisi ikitua katika mgodi wa almasi uliopo Mwadui.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) inawahoji vigogo wa Serikali wakiwemo walikokuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti huku polisi ikitua katika mgodi wa almasi uliopo Mwadui.

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata imeeleza kuwa miongoni mwa vigogo waliohojiwa na Takukuru kwa vipindi tofauti mpaka jana ni mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na William Ngeleja..

Akizungumza kwa simu na gazeti la Mwananchi mnamo Jumatatu, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Valentino Mlowola japo hakuwataja mawaziri hao wastaafu, alikiri vigogo kadhaa kuhojiwa.

Mlowala alisema kuwa mbali na ripoti za kamati teule za Bunge zilizochuguza mwenendo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa Madini ya aina ya almasi na Tanzanite zilizowasilishwa kwa Rais Magufuli kuwataja Profesa Muhingo na Ngeleja na pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani kuhusika kwa namna moja au nyingine katika masuala ya kiutendaji yaliyokwenda kinyume na mikataba.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema Profesa Abdulkadir Mruma aliyetajwa katika ripoti hiyo kuwa ni mmoja wa wahusika alikuwa amepandikizwa kwa maadui ili kubua taarifa ya namna nchi inavyoibiwa.

Profesa Mduma ndiye aliyeongoza kamati ya kwanza ya Rais ya kuchunguza mchanga wa Madini ambayo pamoja na mambo mengine ilimtaja Profesa Muhongo kuhusika na upotevu wa mapato wa Madini na hivyo kutakiwa kujiuzulu mwezi Mei 24.

Makinikia

Ngeleja ambaye pia alikuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Awamu ya Nne ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alitajwa katika kashfa kadhaa za madini ikiwamo ya mchanga wenye madini maarufu kama makinikia.
Mbali na kashfa hiyo, vilevile alitajwa katika kashfa ya Teggeta Escrow ambao hata hivyo hivi karibuni alirejesha Sh 40 milioni ziizotolewa na mfanyabiashara maarufu James Rugemalira.
Mawaziri wengine wastaafu wa Nishati na Madini katika Awamu ya Tatu na ya Nne waliotajwa katika kashfa ya madini na Kamati ya Rais ikiwemo ile ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro ni pamoja na Daniel Yona, Abdallah Kigoda (marehemu) na Nizar Karamagi. Wengine waliotajwa ni waliokuwa wamasheria wakuu wa Serikali Andrew Chenge na Johnson Manyika.
Vilevile wako aliyekuwa Mkurugenzi wa Mikataba Felix Mrema na aliyekuwa Makamishna wa Madini wa Wizara ya NIshati na Madini Mary Ndosi na Dk Dalali Kafumu, Mwanasheria Jaji Julius Malaba na baadhi ya maofisa wa TRA.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya biashara za madini za almasi na Tanzanite wiki iliyopita Rais Magufuli aliagiza viongozi wote waliotajwa katika ripoti hiyo kujiuzulu mara moja kupisha uchunguzi.

Pia aliagiza vyombo vya ulizi na usalama kuwakamata wote waliotajwa huku akiwataja Watanzania kuwa na uzalendo.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro alisema Jeshi la Polisi limeanza kuifanyia kazi ripoti hizo walizokabidhiwa na Rais Magufuli kuhusu masualla ya wizi, ufisadi, uzembe pamoja na rushwa zilizosababisha nchi kupata hasara kutokana na biashara ya madini.
Alisema, “Wale wote waliotajwa kwenye ule uchunguzi wa biashara ya madini ni vizuri sana wakajisalimisha wao wenyewe kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ili waweze kuhijiwa na uchunguzi ufanyike hlafu tuweze kufahamu wanahusika kwa kiasi gani na wasisubiri kukamatwa.”