http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759186/medRes/2109554/-/1lvkqx/-/viise.jpg

 

‘Vijana shiriki kutoa uamuzi’

Issa Haji Ussi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Visiwani Zanzibar, Issa Haji Ussi ‘Gavu’. Picha/MAKTABA 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  13:03

Kwa Muhtasari

Vijana visiwani Zanzibar wametakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa uamuzi kwenye masuala ya kisiasa na kijamii ili Zanzibar ipige hatua katika maendeleo yanayoletwa na watu wake.

 

VISIWANI ZANZIBAR

VIJANA visiwani hapa wametakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa uamuzi kwenye masuala ya kisiasa na kijamii ili Zanzibar ipige hatua katika maendeleo yanayoletwa na watu wake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ alitoa kauli hiyo wakati akifungua mdahalo kuhusu ushirikishwaji wa vijana katika kutoa uamuzi kwenye masuala ya kisiasa na jamii.

Mdahalo huo wa siku moja uliwashirikisha vijana kutoka Wilaya ya Mjini Kati, masheha na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Ussi alisema ni jambo la busara kwa vijana kuwa tayari na kujiamini katika kutoa uamuzi ili kuiwezesha Serikali kuchukua maoni yao na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Alisema kwa kuwa vijana ni nguzo ya Taifa, ni vyema kila taasisi ikawashirikisha kutoa uamuzi utakaoleta faida katika maendeleo.

“Kiongozi hawezi kuongoza peke yake lazima asikilize uamuzi kutoka kwa wenziwe wakiwamo vijana, hivyo ni vyema kila mmoja wetu kulifahamu hilo na kulifanyia kazi ili uamuzi wa makundi hayo (vijana) yafanyiwe kazi,” alisema Gavu.

Aliwataka vijana waliopata fursa ya kushiriki mdahalo huo kuyatumia vyema mafunzo kutoka kwa viongozi wakiwamo masheha na wawakilishi ili baadaye wawe na uongozi uliotukuka.

Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Mohamed Said Mohamed alisema ili malengo yaliyokusudiwa yawe na nguvu zaidi, lazima vijana wawe kitu kimoja katika utoaji uamuzi kuanzia katika mabaraza yao.

Sheha wa Shehia ya Sogea, Abdullah Mohammed aliwataka vijana kuaminiana, kushirikiana na kupendana ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta maendeleo.