http://www.swahilihub.com/image/view/-/4844224/medRes/2165306/-/ljms7i/-/ikia.jpg

 

Wabunge wa CCM waichachamalia Serikali

Mussa Zungu

Mbunge wa CCM, Mussa Zungu (Ilala). Picha/MWANANCHI 

Na SHARON SAUWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  14:02

Kwa Muhtasari

Wabunge wa CCM, Mussa Zungu (Ilala) na Hussein Bashe (Nzega Mjini) wametumia nafasi yao bungeni, kuishukia Serikali na wataalamu kwa kushindwa kuweka mazingira rafiki ya kibiashara hali inayosababisha wafanyabiashara kukimbia nchini Tanzania.

 

DODOMA, Tanzania

WABUNGE wa CCM, Mussa Zungu (Ilala) na Hussein Bashe (Nzega Mjini) Alhamisi walitumia nafasi yao bungeni, kuishukia Serikali na wataalamu kwa kushindwa kuweka mazingira rafiki ya kibiashara hali inayosababisha wafanyabiashara kukimbia nchini.

Wabunge hao wamesema kipindi hiki wafanyabiashara karibu wengi wamekuwa wakilalamikia mazingira ya kodi kuwa kubwa hali inayowafanya kutoitumia Bandari ya Dar es Salaam na wengine wakidaiwa kufunga biashara zao.

Wawili hao waliyasema hayo walipokuwa wakichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20.

Zungu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge alisema biashara katika maeneo ya bandari na maeneo mengine siyo rafiki kwa wasafirishaji na waingizaji wa bidhaa nchini.

Alisema gharama ya kutoa kontena moja lenye ukubwa wa futi 20 bandarini nchini Kenya ni Dola 80 za Marekani, wakati awali ilikuwa Dola 103.

Alisema gharama za kuingiza kontena lenye ukubwa huo nchini ni Dola 170 za Marekani, hali aliyodai kuwawia ngumu waingizaji wa bidhaa na kujikuta wakivutika kutumia Bandari ya Kenya.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam inayotegemewa nchini, gharama za utunzaji kwa usafirishaji ni Dola 100 za Marekani, lakini Kenya ni Dola 60.

“Hivyo ni lazima watu wengi watahamia katika bandari yenye unafuu, namuomba waziri aendelee kuchukua ushauri wa namna gani anaweza kupunguza kodi na kodi za ‘importation’ ishuke ziwe rafiki kwa wafanyabiashara,” alisema Zungu.

Pia, alimshauri Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango kuangalia tozo na kwamba, uzalishaji katika viwanda vya vinywaji baridi umeshuka kwa sababu gharama ni kubwa na wananchi hawawezi kumudu kununua.

Alisema kwa kupunguza tozo katika bidhaa hizo, mauzo yatakuwa makubwa na uzalishaji utaongezeka hivyo Serikali haitapoteza kitu.

“Wafanyabiashara wengi sasa mheshimiwa mwenyekiti wanakimbia kwenda nchi nyingine. Lazima tuwavutie wawekezaji kwa kuwa na tariff (ushuru) nzuri zenye urafiki,” alisema.

Zungu aliungwa mkono na Bashe aliyesema tatizo ni kubwa serikalini au kwa mawaziri na wataalamu ambao alidai kuwa wamekataa kufikiri ama wameamua kutegeana.

Alisema licha ya Serikali kuchukua hatua nzuri ya kutengeneza andiko la mpango wa kuboresha mazingira ya biashara, kwa nini hawapeleki sheria za kodi bungeni zikafanyiwa marekebisho.

“Kwa nini tunaandaa kwa haraka Muswada wa Vyama vya Siasa tunaacha za kodi ambazo zinahusiana na uchumi? Kwa nini, kipaumbele chetu ni kipi?” alihoji Bashe.

Alisema anatarajia kuona mabadiliko ya kodi na sheria kwa 2019/20, katika maeneo yalikuwapo katika taarifa ya andiko la mpango wa kuboresha mazingira ya biashara.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Lucy Mayenga alisema Taifa limejinasibu linakwenda katika uchumi wa viwanda, lakini kuna tatizo la uratibu wa pamoja baina ya wizara zote zinazohusika.

Alihoji kama Serikali inakaa na kufanyia kazi matatizo ambayo yanawafanya kutofikia malengo ya kuwa katika uchumi wa viwanda.

Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi alisema kuchelewa kutoa uamuzi sahihi na wakati, ndiko kunaiporomosha Tanzania kwenye ripoti ya mazingira ya ufanyaji wa biashara duniani.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema kuna tatizo kwenye mauzo ya nje ya nchi na kwa mujibu wa taarifa ya wizara, bidhaa zilizouzwa nje ya nchi mwaka 2016 zina thamani ya Sh9.8 bilioni, lakini sasa bidhaa zilizouzwa nje ya nchi ni za Sh1 bilioni.

 

Waitara aibua kizaazaa

Pamoja na wabunge hao kuishukia Serikali, Mbunge wa Ukonga (CCM) Mwita Waitara akichangia mpango huo, aliwataja wabunge wa upinzani akiwamo kiongozi wake wa zamani wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuwa wamejipanga kuvuruga mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea.

Aliwataja wabunge aliodai wamekaa kikao kuwa ni Mbowe, aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na mbunge mwingine ambaye hakumtaja jina.

Zitto alisimama kuomba utaratibu huku wabunge wa upinzani wakipiga kelele, lakini Spika Job Ndugai alinyamaza kimya na kumuacha Zitto akiwa amesimama huku Mwita aliyekuwa mbunge wa Chadema kabla ya kutimkia CCM, akiendelea kuchangia licha ya kelele zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wabunge wa upinzani zikiomba kuhusu utaratibu.

“Kama kuna wafanyabiashara ambao hawafuati utaratibu, wanakwepa kodi, wakikamatwa wanasema hawana imani. Wahalifu lazima washughulikiwe, hata Mwalimu Nyerere alifanya hivyo,” alisema Waitara aliyekuwa akishangiliwa na wabunge wa CCM.

Baada ya kumaliza kuchangia, Zitto alipewa ruhusa na kusema kanuni ya 64 inazuia wabunge kutotoa kauli za uongo bungeni, kutozungumzia jambo ambalo halipo kwenye mjadala, hatatumia lugha ya kuudhi ama inayodhalilisha wengine.

Zitto alisema Waitara anapaswa kulithibitishia Bunge kuwa wabunge aliowataja, walikaa wapi na lini kwenye hicho kinachoitwa kuvuruga shughuli za Bunge.

Hata hivyo, Spika Ndugai aliamua kuyafuta maneno akili yako inabadilika kwa sababu

yanadhalilisha na yamekwenda kinyume na alipoanzia na kisha kumruhusu mbunge mwingine kuchangia.