Wanafunzi 100 hatarini

Na MUHAMMED KHAMIS, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  11:25

Kwa Muhtasari

Zaidi ya wanafunzi 100 wa diploma wa chuo cha sayansi na teknolojia cha Karume visiwani hapa wapo hatarini kushindwa kuhitimu masomo yao na kuendelea na shahada ya kwanza kutokana na kukosa usajili kwenye mfumo wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).

 

UNGUJA

ZAIDI ya wanafunzi 100 wa diploma wa chuo cha sayansi na teknolojia cha Karume visiwani hapa wapo hatarini kushindwa kuhitimu masomo yao na kuendelea na shahada ya kwanza kutokana na kukosa usajili kwenye mfumo wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).

Wanafunzi hao wanaosoma fani mbalimbali wamesema wakati wanaomba kujiunga na chuo hicho walielezwa lazima kuwa na ufaulu wa masomo manne kwa kiwango cha D tofauti na wanavyoambiwa sasa kuwa hawana vigezo kwani zinatakiwa D tano.

Mmoja wa wanafunzi hao, Kauthar Yussuf alisema kwa sasa hawajui hatima yao ya kuhitimu itakuaje.

Mwingine, Silima Ali Mashauri alisema, “Kama tulikosa vigezo vya kusajiliwa tangu awali tungeelezwa lakini siyo sasa tupo mwaka wa mwisho tunaambiwa hatuna vigezo.’’

Akizungumza na Mwananchi, Rais wa Serikali ya wananfunzi chuoni hapo, Hakim Abdullah Mohammed alisema tatizo hilo ameshaliwasilisha rasmi katika uongozi wa chuo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Uongozi wakata kulizungumzia

Hata hivyo, uongozi wa chuo hicho umekataa katakata kuzungumzia suala hilo.

Kwa sharti la kutotajwa jina lake, ofisa wa ngazi za juu wa Nacte visiwani hapa alisema utaratibu haujabadilika na kwamba kinachoendelea katika chuo hicho hajui ni kitu gani.

Alipoulizwa naibu waziri wizara ya elimu na mafunzo ya amali, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema wizara hiyo imepata taarifa hiyo ingawa sio kwa kina na kwamba wanafuatilia kujua tatizo hasa ni nini. Hata hivyo, alisema viongozi wa Nacte wapo Zanzibar kwa ajili ya kikao chao na kwamba anaamini jambo hilo litapatiwa ufumbuzi.