http://www.swahilihub.com/image/view/-/4758978/medRes/2109422/-/fsuohuz/-/ukubiswa.jpg

 

Wataalamu wa Afya wataja mbinu kuzuia ugonjwa hatari wa Sepsis, Serikali yatahadharisha

Mpoki Ulisubisya

Katibu Mkuu Wizara ya Afya nchini Tanzania, Mpoki Ulisubisya. Picha/MAKTABA 

Na FORTUNE FRANCIS, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  11:41

Kwa Muhtasari

Wakati tafiti zikionyesha kuwa asilimia 32 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na maambukizi ya bakteria kwenye damu kitaalamu Sepsis, wataalamu wa afya, wamezitaja njia za kujikinga na ugonjwa huo.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

WAKATI tafiti zikionyesha kuwa asilimia 32 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na maambukizi ya bakteria kwenye damu kitaalamu Sepsis, wataalamu wa afya, wamezitaja njia za kujikinga na ugonjwa huo.

Njia hizo ni pamoja na kuzingatia usafi, kufunga vidonda, kunawa mikono, kuoga mara kwa mara na kupata kwa wakati tiba ya maambukizi ya bakteria kwenye mkojo (UTI).

Akizungumza Alhamisi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mpoki Ulisubisya alitoa tahadhari kuhusu ugonjwa huo akisema kwa sasa asilimia 32 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na maambukizi ya bakteria kwenye damu yaani Sepsis.

“Pamoja na kuwa bakteria hawa wanasababisha vifo kwa watoto wachanga pia asilimia nane ya vifo vya kinamama waliotoka kujifungua,” alisema Dkt Mpoki.

Dkt Ulisubisya alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha zaidi ya watu milioni 30 duniani kote wanapata Sepsis na wengine milioni sita hupoteza maisha kila mwaka.

“Ugonjwa huu unaweza kumshambulia mama aliyejifungua, watoto wachanga, wazee na wenye umri mkubwa lakini hata wenye magonjwa yanayopunguza kinga ya mwili kama Ukimwi, Kisukari na kuongezeka kwa usugu wa dawa za kuua vijidudu vya magonjwa,” alisema.

Alisema madhara ya ugonjwa huo ni makubwa na yanahatarisha maisha ya watoto wachanga na kinamama waliojifungua ndani ya katika kipindi cha siku 42.

Alisema madhara ya ugonjwa huo ni pamoja na kuganda kwa damu, kuzuia kupeleka hewa safi (oxygen) mwilini, kufeli kwa ogani muhimu kama figo hali inayoweza kusababisha kifo kwa asilimia 50.

Homa kali

Akizungumzia namna ya kujikinga na ugonjwa huo, Daktari wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IhI), Fred Haraka alisema ni muhimu jamii ikaelimishwa kuhusu kwenda hospitali haraka pindi mtoto au mama aliyejifungua anapopata homa kali.

“Kama ni kidonda, kifungwe kwa usafi na kitunzwe ili kisiingie bakteria, usafi ni suala muhimu na muhimu zaidi ni kupata huduma za afya haraka,” alisema.

Dkt Haraka alitaja vyanzo vya Sepsis kuwa ni bakteria kuingia kwenye damu, bakteria kuingia kwenye kidonda na kwenda kwenye mfumo wa damu, bakteria kwenye sikio na mama aliyejifungua kupata maambukizi hayo kutokana na majeraha ya kujifungua.

“Huu ni ugonjwa hatari, damu haitakiwi kuwa na maambukizi ya bakteria, madhara yake ni mtu kupata mshtuko au ogani za mwili kufeli,” alisema.

Alisema watoto wachanga wenye umri wa kuanzia siku moja hadi miezi mitatu, huathiriwa kwa urahisi na bakteria kutokana na kinga yao ya mwili kuwa ndogo.