http://www.swahilihub.com/image/view/-/4703176/medRes/2072807/-/t1ooyq/-/shein.jpg

 

Wataalamu wa uchumi Falme za Kiarabu watua Zanzibar

Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein. Picha/MWANANCHI 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  14:21

Kwa Muhtasari

Wananchi waombwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu hao ambao wana lengo zuri Zanzibar

 

VISIWANI ZANZIBAR

WATAALAMU 16 wa uchumi kutoka Falme za Kiarabu (UAE) wapo visiwani hapa kuangalia miradi saba ya maendeleo watakayoitekeleza baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein na uongozi wa Falme hizo.

Akizungumza wakati akiwapokea katika Uwanja wa Ndege Zanzibar, Mshauri wa Rais, Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia alisema wageni hao watakuwa visiwani hapa kwa siku tatu.

Alisema ujio wao unatokana na ziara aliyoifanya Dkt Shein mwanzoni mwa mwaka 2018.

Balozi Ramia alisema wataalamu hao watafanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kukagua miradi ya Hospitali ya Wete, Barabara ya Chake hadi Wete, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Barabara ya Fumba hadi uwanja wa ndege, Hospitali ya Binguni pamoja na matengenezo ya Nyumba za Mji Mkongwe.

“Niwaombe sana wananchi, tuwape ushirikiano wataalamu hao ambao wana lengo zuri kwetu ambalo likifanikiwa kama linavyotarajiwa ni wazi Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo,” alisema Balozi Ramia.

Kiongozi wa ujumbe huo, Dkt Najla Alkaabi alisema kuwa wao kufika Zanzibar kunatokana na uongozi wa Serikali ya UAE kuridhia maombi ya Dkt Shein kuhusu uungwaji mkono katika miradi yake mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia wananchi.