http://www.swahilihub.com/image/view/-/3978682/medRes/1677525/-/l3hdogz/-/kja.jpg

 

Historia fupi ya Kiswahili

Kamusi ya Kiswahili

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongoza wajumbe wa Bakita wakiingia kwenye Ukumbi wa Bunge Juni 19, 2017. Mbele yake yuko Mussa Azan Zungu akiwa Mwenyekiti wa kikao cha Bunge. Picha/GAZETI LA MWANANCHI 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Tuesday, January 23  2018 at  09:20

Kwa Muhtasari

Mambo yaliyosaidia kuenea kwa Kiswahili ni pamoja na biashara, dini, ukoloni na harakati za ukombozi wa kupata uhuru.

 

Kitovu cha Kiswahili (Swahili Hub)

Historia fupi ya Kiswahili

LUGHA ya Kiswahili ni lugha ya Kibantu na chimbuko lake ni upwa wa Afrika Mashariki. Hata hivyo lugha hii haikuishia upwa wa Afrika Mashariki tu, bali ilisambaa katika maeneo mbalimbali ya bara hili.

Mambo yaliyosaidia kuenea kwake ni pamoja na biashara, dini, ukoloni na harakati za ukombozi wa kupata uhuru.

Misafara ya biashara

Wanahistoria wanaeleza kwamba lugha ya Kiswahili ilianza kuenezwa na wenyeji na baadaye na wafanyabiashara.

Wenyeji walibadilishana bidhaa mbalimbali kwa makabila ya jirani. Baadaye walifuatwa na wafanyabiashara wa Kiarabu waliokuwa wanataka bidhaa za pembe za ndovu na pia watumwa.

Kwa kweli misafara ya kwenda bara kutoka pwani ilifanywa na wapagazi Waafrika wakifuatana na Waarabu waliosafiri kwenda bara ya Tanganyika na Kenya waliotumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano na wenyeji wa bara.

Misafara hii ilifika maeneo mbalimbali ya bara hadi kufikia Mashariki ya Kongo maeneo ya Goma na Kivu ambako kunazungumzwa lahaja pekee inayojulikana kama Kingwana.

Dini za kigeni

Uenezaji wa dini za kigeni pia ulichukua nafasi yake muhimu sana ya kukieneza Kiswahili. Waarabu walipoleta dini yao ya Kiislamu waliwashawishi wenyeji kusilimu.

Walilazimika kujifunza Kiswahili ili waweze kuhubiri mafundisho na fasili ya Kurani kwa Kiswahili ikiwa ni lugha iliyoeleweka na wengi. Mashehe na maulama walianzisha matumizi ya maandishi ya Kiswahili kwa kutumia alfabeti za Kiarabu.

Nao Wamisionari walipofika Afrika Mashariki hawakutaka sana kutumia Kiswahil kwa sababu waliinasibisha lugha hii na dini ya Kiislamu. Walipendelea kutumia lugha za kienyeji lakini waligundua kuwa wangenufaika zaidi kama wangetumia Kiswahili.

Kwa nia hiyo, wakawa wanachangia katika kikieneza Kiswahili. Hivyo wakaanzisha alfabeti za Kirumi ambazo zinatumika hadi sasa.

Kipindi cha ukoloni

Wakoloni walikuwa na mchango mkubwa sana wa kukikuza na kukiendeleza Kiswahili na kuanzia na ukoloni wa Kiarabu. Kiswahili kilitumika katika kutafsiri, ufasili na kufafanua aya mbalimbali za Korani.

Waliofuata ni wakoloni wa Kijerumani ambao walikuta lugha ya Kiswahili imeanza kukubalika katika shughuli za kibiashara na za kiutawala.

Walianzisha shule kwa ajili ya wafanyakazi wa ngazi za chini kama makarani na matarishi. Madarasa ya chini ya shule za Tanganyika na Zanzibar yalifundishwa kwa Kiswahili.

Wakoloni waliofuata walikuwa ni Waingereza ambao walifanya kazi kubwa ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili kupata watumishi na wasaidizi wengine wa ngazi za chini.

Mwaka 1925 Gavana wa Tanganyika aliitisha kikao cha viongozi wa elimu katika nchi zote za Afrika Mashariki kujadili suala la matumizi ya lugha ya Kiafrika kwa nchi zote. Wajumbe wote walikubali na kupendekeza kuwa lugha iwe ni ya Kibantu na Lugha iliyofikiwa ni Kiswahili.

Mwaka 1928 ilionekana kuwa kwa kuwa Kiswahili kina lahaja nyingi, lahaja ya Kiunguja ilichaguliwa kuwa ni lahaja mwafaka kwani ilikuwa imeenea katika sehemu kubwa ya nchi hizi na ndiyo iliyoanza kusanifiwa na kuwa lahaja rasmi ya mawasiliano.

Ili kufanikisha azma hiyo, shughuli zote za ukuzaji na usanifishaji wa lahaja ya Kiunguja, iliundwa Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki na katibu wake wa kwanza alikuwa hayati Frederick Johnson.

Kamati hii ilianza kufanya utafiti wa lahaja za Kiswahili. Walianzia na lahaja za Kimvita, Kipemba, Kimtang’ata, Kijomvu, Kingare na Cifundi. Vitabu wakaanza kuandikwa  kuhusu vipengele mbalimbali vya lahaja hizo.

Iliundwa taasisi yenye jukumu la kuendeleza Kiswahili kwa lengo la kuchapisha vitabu na kutoa ushauri kuhusu masuala ya uandishi.

Taasisi hii ilijulikana kama Shirika la Uchapishaji vitabu la Afrika Mashariki (EALB). Iliwahamasisha waandishi chipukizi na pia kutoa muhuri wa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada.

Baadaye Kiswahili kikaanza kufundishwa ili kitumike katika masuala ya maendeleo.

Usanifishaji

Usanifishaji wa Kiswahili ulianzishwa enzi za ukoloni mwaka 1930 na kutelekezwa na Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ambayo ilifikia hatima yake mwaka 1964 ilipoundwa Taasisi ya Ukuzaji wa Kiswahili (TUKI) chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hatua hii ilichukuliwa baada ya kila nchi katika Afrika Mashariki kupata uhuru na hivyo kuwa na sera tofauti.  

Tanzania:

Kiswahili nchini Tanzania ni lugha rasmi na lugha ya Taifa. Ni lugha ya utambulisho kwa Mtanzania na inatumika kama lugha ya kuimarisha uelewano, ushirikiano na umoja wa kitaifa.

Katika kuiendeleza, juhudi za usanifishaji zimefanyika kwa kuwatumia wataalamu wa fasihi na isimu, wadau wengine na wachapishaji vitabu. Vyombo mbalimbali viliundwa kama Bakita, Bakiza, Takiluki, Taasisi ya Elimu, Uwavita na Ukuta. Pia vyuo vikuu mbalimbali vya Bara na Visiwani vilianza kusomesha Kiswahili kuanzia shahada ya kwanza, ya uzamili na uzamivu.

Kenya:

Kiswahili nchini Kenya ni lugha rasmi na pia ni lugha ya Taifa. Mnamo mwezi Agosti, 1969 Rais wa Kenya Mzee jomo Kenyatta alitoa kauli kwamba Kiswahili kinafaa kutumika kama lugha rasmi ya Kenya na mwaka 1975 Lugha ya Kiswahili ikaanza kutumika katika Bunge la Kenya.

Serikali ya Kenya ikaanzisha somo la Kiswahili katika Idara ya Lugha za Kiafrika na Isimu  ya Chuo Kikuu cha Nairobi. Kuanzia miaka ya themanini mwishoni, takriban vyuo vikuu vyote vilivyoanzishwa na Serikali vinafundisha masomo ya Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili.

Pengine hatua muhimu iliyochukuliwa na Serikali ya Kenya ni kuwa kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari  analazimika kuchukua somo la Kiswahili kama somo la lazima.

Uandishi

Kiswahili ni lugha yenye historia ndefu ya uandishi hasa katika pwani ya Kenya. Maandishi yalijikita katika fani hasa ya mashairi na tenzi. Wako mabingwa wabobezi wa Kiswahili walioanza na utunzi wa mashairi katika pwani ya Kenya walioishi Lamu, Pate na Mombasa. Walikuwapo kina Fumo Liyongo, Muyaka bin Haji, Alamin Mazrui na Abdulatif Abdallah na wengine kadhaa.

Kiswahili kilienea bara hasa mijini na kutumika kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na  shule za sekondari.

Uganda:

Nchini Uganda Kiswahili kilipelekwa huko na wafanyabiashara kutoka pwani. Tangu mwanzo lugha ya Kiswahii ilipigwa vita na watawala wa jadi kama Kabaka na pia na wamisionari waliokilinganisha Kiswahili na Uislamu na pia kukiona kama ni lugha ya wadhalilishaji. Hata hiyo kinatumika katika majeshi kama Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi.

Katika elimu, Kiswahili kinafundishwa katika shule chache za msingi na sekondari na katika vyuo vikuu kama Makerere, Mbarara, nk. Kiswahili kimo katika mipango ya kuimarishwa ili kiweze kutumika kama lugha ya mawasiliano ya ndani na nje ya nchi.

Kimataifa:

Inafahamika kuwa wazungumzaji wa Kiswahili wanazidi kuongezeka. Kiswahili kinazungumzwa katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati, Visiwa vya Comoro, Kaskazini ya Msumbiji na kusini mwa Somalia.

Ziko redio, runinga, mitandao ya kijamii na tovuti ambazo zinatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Redio na Runinga nchini Uingereza, Ufaransa,  Marekani, India, Korea Kusini, Sweden, Finland, Norway, Ujerumani, China na Japan hutangaza kwa Kiswahili. Vyuo vikuu katika baadhi ya nchi hizo pia kufundisha Kiswahili.

Kitovu cha Kiswahili:

Kwa kuzingatia umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa nchi, kanda na kimataifa, Kampuni ya Nation Media Group ilibuni mradi wa kukiendeleza Kiswahili  ili kiweze kuimarika katika matumizi yake ya fasihi na isimu kwenye elimu, siasa, uchumi, utamaduni na teknolojia.

Mradi huu ulioanzishwa nchini Kenya mwaka 2012, chini ya usimamizi wa Kampuni ya Nation Media Group na mwaka 2016 makao makuu yake yalihamishiwa katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Kiswahili ya Mwananchi na Mwanaspoti.

Madhumuni

Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa na wananchi wengi wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.  Kutokana na umuhimu wake, Kiswahili kimechaguliwa kuwa ni lugha ya Taifa ya Tanzania na Kenya na pia ni lugha rasmi katika nchi hizi na pia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki  pia Umoja wa Afrika.

Nation Media Group