Na JENITHA WALTER
Imepakiwa - Tuesday, April 24 2018 at 12:43Kwa Muhtasari
Kauli hutokana na mchakato wa unyambuzi; yaani urefushaji wa vitenzi.
KAULI katika lugha ya Kiswahili hutokana na mchakato wa unyambuzi wa vitenzi. Vitenzi ni miongoni mwa aina za maneno ambavyo hutumika kuelezea tendo fulani mfano kivumishi, kielezi, kihusishi, kihisishi na kiunganishi. Zifuatazo ni kauli za vitenzi:
Kauli ya kutendeka; kauli hii huonesha uwezekano wa tendo kufanyika. Mfano:
Chezeka
Mechi kati ya Simba na Yanga itachezeka kesho jioni katika Uwanja wa Taifa.
Pigika
Mwizi yule alipigika kiasi ambacho hakuweza kuiona kesho yake, alifariki dunia.
Someka
Fujo nyingi za wanafunzi zilisababisha kutosomeka kwa kipindi cha pili.
Lishika
Haikuwezekana George kulishika bila kumbinya mdomo na kumshika miguu kwa nguvu.
Zalika
Baada ya kufunga uzazi kwa miaka miwili hatimaye mtoto wa watu alizalika.
Zoleka
Japokuwakulikuwa na mvua, majani yote yalizoleka.
Kauli ya kutendesha; kauli hii huhusisha mambo mawili ambayo ni lazima yatokee. Kwanza, kuwe na mtu au watu wanaofanya jambo fulani. Mtu huyo au watu hao sio lazima watende mfano somesha. Kumsomesha mtu sio lazima na wewe usome au uwe umesoma.
Pili, pawe na watu wanaofanya jambo fulani. Watu hao ni lazima wafanye hilo tendo. Mfano kama unalimisha, watu hao ni lazima walime.
Limisha
Baba amelimisha shamba la ekari tatu lililopo karibu na mto Ruvu.
Somesha
Mwalimu mkuu alimsomesha mwanae wa kwanza sekondari ya mtu binafsi.
Kalisha
Mama alimkalisha mtoto kwenye kochi ili asimsumbue akiwa anapika chakula.
Zalisha
Mkunga kutoka Moshi alimzalisha dada nyumbani.
Liza
Kukosa tuzo za mwanafunzi bora, kulimliza Janeti.
Kauli ya kutendea: Kauli hii huelezea hali ya mtendaji kufanya jambo.
Somea
Kaka alisomea kitabu kikuukuu sana (kilichochakaa).
Imbia
Sara aliimbia sauti ya juu sana hadi tukashindwa kuitikia wimbo.
Chezea
Wanafunzi walichezea zana za mwalimu za kufundishia.
Pakia
Mjomba alipakia vyombo vyote kwenye lori.
Kauli ya kutendwa; hutumika kuelezea mtu au kitu kinachofanyiwa jambo fulani.
Chezwa
Baada ya kupatiwa mafunzo kwa muda mrefu, wali walichezwa ngoma.
Pigwa
Mwizi alipigwa bila huruma japo wengine walitaka apelekwe polisi.
Zalishwa
Mwanahamisi alizalishwa watoto wanne akiwa nyumbani kwao.
Zoleshwa
Baada ya kutapika kwa sababu ya kunywa pombe nyingi alizoleshwa matapishi yote.
Kauli ya kutendana; hutumika kuonesha pande mbili zikiwa zinafanya jambo fulani.
Limiana
Baada ya kumaliza kulimiana shamba walikubaliana kila mmoja atafute soko lake.
Andikiana
Walipotambua miandiko yao inafanana, waliandikiana nukuu za kila somo.
Ogeshana
Mapacha wale waliogeshana kwenye beseni moja lililokuwa na maji ya uvuguvugu.
Zalilishana
Mtu na mke mwenzake walizalilishana kwa kutukanana hadharani.
Semeana
Alipomtaja kuwa alidokoa nyama, walisemeana mambo yote waliyoyafanya harusini.
Kauli ya kutendewa: Kauli nii ni matokeo ya michakato ya kauli mbili kuungana. Kauli hizo ni kauli ya kutendea na kauli ya kutendwa.
Chezewa
Aisha kwa kuwa hakuwa na msimamo katika uhusiano, alichezewa na wanaume wengi.
Pigiwa
Juma alipigiwa ngoma yake kwa kuwa alikuwa anaumwa.
Zalishiwa
Matajiri wote huzalishiwa mali na maskini.
Somewa
Juma alisomewa kitabu cha hadithi na James.
Kauli ya kutendua; ni kauli ambayo hutumika kuonesha jambo ambalo limefanyika kinyume.
Pangua
Dada alipangua viti vyote vilivyokuwa karibu na meza ya chakula.
Fungua
Mwizi alifungua mlango taratibu akidhani kwamba ndani hakukuwa na mtu.
Zibua
Mzee Juma ni hodari kwa kuzibua vyoo.
Vua
Mwajua alivua gauni lake refu alilovaa mchana na kuvaa fupi baada ya wageni kuondoka.