http://www.swahilihub.com/image/view/-/4754450/medRes/2106537/-/631yli/-/sahani.jpg

 

Kipolo kimenishinda

Sahani yenye mchanganyiko wa vyakula   

Na Stanley Dastan Letema

Imepakiwa - Tuesday, September 11  2018 at  16:19

Kwa Muhtasari

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi

 

Nafungua domo langu, haya kuyaweka wazi,

Nakinena kisa changu, kilichonitoa chozi,

Ingawa ninamachungu, namuachia mwenyezi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Kuvunjika kwa pakacha, nafuu kwa mchukuzi,

Kipolo kimeshachacha, hata kukila siwezi,

Niweke nini machacha, kuunogesha mchuzi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Chakula nilikipika, nikashindwa kuhifazi,

Nilishindwa kusindika, nilizidiwa na kazi,

Nakihisi kinanuka, niriziki yake nzi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Njaa inanisokota, nazunguka kama chizi,

Mateso ninayopata, najiona mpuuzi,

Kila ninachokipata, naona ganda la ndizi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Vyakula vya kibandani, kwangu mimi siviwezi,

Kwa yale mapishi duni, nahisi kuna malazi,

Ninakufa kisabuni, simuoni mtetezi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Nilipiga moyo konde, nitadoea kwa Suzi,

Nikayakuta makande, yamesheheni mchuzi,

Nikayala kiafande, ingawa sina mapenzi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Nilikupenda kipolo, hilo ulijua wazi,

Nilishikwa na kiholo, nilipomkuta nzi,

Ninaogopa uhalo, kukurudia siwezi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Mzee amenambia, mlachake sio mwizi,

Sasa nimeshatambua, sitoludia ushenzi,

Kikiiva napakua, sitokiletea pozi.

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

Nimeshafika kikomo, kunena yangu majonzi,

Furaha yake mdomo, kula kilicho mapenzi,

Akili za mbili kimo, dafu nilijua nazi,

Kipolo nakikumbuka, japo kukila siwezi.

 

0788227605/ 0679893903 Segerea- Dar es salaam