Konsonanti, vigezo bainifu vya konsonanti

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, December 5  2018 at  10:03

Kwa Muhtasari

Konsonanti ni sauti ambazo hutamkwa kwa kuzuiwa kwa mkondo wa hewa kutoka mapafuni kwenda nje.

 

KWA mujibu wa Massamba et al (2004), konsonanti ni sauti ambazo hutamkwa kwa kuzuiwa kwa mkondo wa hewa kutoka mapafuni kwenda nje kupitia ama chemba ya kinywa au chemba ya pua.

Kumbuka katika makala iliyotangulia maelezo yametolewa kwamba baadhi ya watu husema chemba ya huku wengine wakisema chemba cha.

Konsonanti hubainishwa kwa kutumia vigezo (sifa) vikuu vinne vifuatavyo:

 

i. Jinsi au namna ya matamshi (manner of articulation)

ii. Mahala pa matamshi (place of articulation)

iii. Mkondo wa hewa (air stream)

iv. Hali ya vyuzi au kanda sauti (state of glottis)

 

 

Mahala pa matamshi

Sifa ya mahala pa matamshi huhusu alasauti zinazohusika katika utamkaji wa sauti. Katika utamkaji huwa kuna alasauti (ala sogezi) ambazo hujongea na kusogea katika ala nyingine (alatuli) ili kwamba sauti fulani zifanyike kutokna na kugusana kwa ala hizo.

Hivyo basi ala hizo zinazogusana ndizo husababisha kutokea kwa sauti za lugha. Hivyo basi mahala pale sauti fulani inapotokea baada ya alasauti kugusana ndipo huitwa mahala pa matamshi. 

Mahala pa matamshi, kama tulivyoeleza hapo awali, ni sifa inayorejelea viungo vinavyohusika na utamkaji. Viungo hivyo ni kama, midomo, midomo na meno, meno, ufizi, kaakaa gumu, kaa kaa laini, kilimi, koo na koromeo.

 

Ala hizi zinafafanuliwa kwa kina jinsi ifuatavyo:

 

Midomo (Sauti za midomo).

Sauti za midomo hutokana na hewa inayotoka katika mapafu kupitia chemba ya kinywa au ya pua kutatizwa au kuzuiliwa na midomo yote miwili. 

Mdomo wa juu huelekeana na mdomo juu ili sauti fulani zitokee. Sauti ambazo hutokea kwa kutokana na sifa hii ni kama vile : [m], [p], [b],[ɱ], [w], [ᵝ]

 

Midomo meno (Sauti za midomo meno)

Sauti hizi huhusisha meno ya juu yakishirikiana na meno ya chini na mdomo wa chini. Mdomo wa chini huwa unasogea na kubanwa na meno ya juu na ya chini kisha hewa inayotoka katika mapafu huruhusiwa kupenya kwa shida katikati na kutengeneza sauti kama  [f], [v], na /ɱ/.

Meno (sauti za meno)

Sauti za meno hutamkwa wakati ambapo ncha ya ulimi inasogea na kubanwa na meno ya juu na

ya chini. Mifano ya sauti hizi ni kama vile [θ], na [ð]

 

 

Marejeo

Whiteley, W.H., (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen and Company Limited.

Chiraghdin, S., Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.