Lugha ya Kiswahili katika magazeti

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Tuesday, April 24  2018 at  13:20

Kwa Mukhtasari

Hivi sasa maelekezo ya mwongozo kuhusu matumizi ya lugha fasaha ya Kiswahili kwenye magazeti kwa wanahabari yaliyotolewa mengi yamezingatiwa lakini bado kuna makosa yanatojitokeza ambayo yanaendelea kuandikwa.

 

KWA kipindi kirefu nimekaa kimya baada ya kutoa mwongozo kuhusu matumizi ya lugha fasaha ya Kiswahili kwenye magazeti kwa wanahabari. Mwongozo huu ni ule uliotayarishwa na kamati maalumu ya Kiswahili ya Kampuni ya Mwanachi Communications Limited na kupitishwa na uongozi wa Idara ya Uhariri ya Kampuni ya Nation Media Group nchini Kenya.

Mwongozo huu umeyatarishwa kwa lengo la kuwasaidia wanahabari kwa maana ya waandishi wa habari na watangazaji katika redio na runinga. Baadhi ya mada zilizoainishwa ni miundo, maumbo, maana na matamshi sahihi ya lugha ya Kiswahili kwakuzingatia athari za lugha za makabila na pia athari za lugha za kigeni kama Kiarabu na Kiingereza.

Hivi sasa maelekezo yaliyotolewa mengi yamezingatiwa lakini bado kuna makosa yanatojitokeza ambayo yanaendelea kuandikwa.

Napenda kunukuu sentensi zilizoandikwa katika gazeti moja la hapa nchini Tanzania lililochapishwa Alhamisi, Aprili, 19, 2018. Kwa mfano imeandikwa:

-        Ali Kiba amekodisha Ukumbi wa Diamond Jubilee unaokadiriwa kuchukua watu 500.

Sentensi hii ina maana kuwa Ali Kiba ameuchukua ukumbi huo kwa shughuli zake binafsi kutoka kwa wamiliki wa ukumbi huo.

Ingekuwa sahihi kama mwandishi angeandika, “Ali Kiba amekodi Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa shughuli zake binafsi. Mwenye ukumbi ndiye aliyemkodisha Ali Kiba ukumbi huo.

-        Bado kamisheni haijakifunga kituo cha kuwaweka wahanga wa mvua hizo.

Maana mhanga ni mtu anayejitolea kwa hiari yake na kuwa tayari kumwaga damu yake au kuhatarisha maisha yake kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuwa tayari kuua au kupigania maslahi ama yake au ya mtu mwingine, kikundi, jamii, nchi yake au kufanya uharibifu mkubwa wa mali za watu ili atekeleze dhamira mbaya ya kufanya maangamizi aghalabu kwenye halaiki ya watu.

Maelezo haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kutoka katika Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Pili iliyotayarishwa na Baraza la Kiswahili (Bakita) kwa kushirikiana na Kampuni ya Longhorn Toleo la mwaka 2016 na Chapisho la 2017.

Kwa hiyo kituo kilikuwa cha kuwaweka waathirika wa mvua hizo na wala sio wahanga. Hawa wameathirika kwa maana ya watu waliopata madhara ama kwa kujeruhiwa au kuumizwa.   

-         Majengo yalijengwa kinyume cha sheria.

Kwa usahihi tunapaswa kuandika “Majengo yalijengwa kinyume na sheria”.Maana yake ni kwamba ujenzi ulifanywa bila kufuata sheria kwa hiyo ni kunyume na sheria iliyopo.

-                 Lakini Machi 2013 jumba la gharofa 16 liliporomoka wilayani Ilala. Kwa mujibu wa kanuni za sarufi ya Kiswahili sanifu, neno lakini linatumika kama kielezi yaani linaashiria kasoro, upungufu, hitilafu, nk. Kwa kawaida haifai kutumia neno lakini kwa kuanza sentensi au aya katika uandishi. Nenoakini linatumika kuunganisha vifungu vya maneno.  Kwa mfano angeandika, “Alishindwa kuoa lakini alikosa fedha za kulipia mahari.

-        Na kuwashirikisha wataaalimu wa Idara na Taasisi mbalimbali suala hilo lingeweza kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Kwa kawaida tunatumia neno na kama kiunganishi na wala hatuwezi kulitumia kuanza aya ya sentensi na neno na.

-        Kifedha wataalamu hutizama hali halisi ya uchumi.

Kiini cha neno hutizama ni tazama. Kutazama ni kuangalia kitu au mtu. Hata hivyo mwandisi alikosea tahajia ya neno hili. Kwa usahihi ilitakiwa kuandika tazama na sio tizama. Ni kosa kuandika tizama ijapokuwa watu wengi wamezoea kutumia tizama badala ya tazama. 

-        Mapato ya kodi peke yake haitoshi kugharamia bajeti ya nchi husika.

Neno kugharamia ni kitenzi linalotokana na neno gharama ambalo ni nomino. Maana ya gharama ni thamani ya bidhaa au huduma. Pia malipo ya huduma, matumizi aghalabu makubwa ya fedha. Kitenzi chake ni  gharimu kwa maana ya kutoa kiasi fulani cha malipo au kutiwa matatizoni.

Kama tukilinyambua neno gharimu tunapata  gharimia na siyo gharamia kwani hatuwezi kunyambua nomino bali ni kitenzi tu kinachoweza kunyambuliwa.

-Viongozi wa Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Monduli walitembelea eneo la mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo kwa siku tatu mfululizo. Pia kuna kichwa cha habari kilichoandikwa,

“Wakazi wakwama juu ya miti kwa siku kadhaa kufuatia mafuriko.”

Imekuwa ni mazoea kwa watu wengi kutumia neno hili kufuatia badala ya kutokana na. Hata majirani zetu wanatumia sana neno hili kwenye redio, runinga na magazeti yao bila kufahamu kuwa wanakosea. Maana ya kufuatia ni kuambatana kwa kwenda nyuma ya mtu mwingine. Hata hivyo, maana iliyokusudiwa hapa ni kutokana na.

Kutokana na mafuriko, wananchi wameshindwa kuishi kwenye makazi yao na kujificha kwenye miti. Wananchi hawa hawakufuata mafuriko na kukimbia na kukwea miti bali walikimbia makazi yao kutokana na mafuriko.

Nashauri waandishi na pia wahariri wawe makini wanapofanya kazi zao na killa mara warejee kwenye kamusi za Kiswahili.