http://www.swahilihub.com/image/view/-/4392590/medRes/1938396/-/j5oreiz/-/maina.jpg

 

Lugha ya Kiswahili katika magazeti

Stephen Maina

Bw Stephen Maina. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Monday, June 25  2018 at  16:20

Kwa Muhtasari

Sahihi ni ‘ugonjwa’ na halipo neno ‘gonjwa’ kwa maana ugonjwa mkubwa.

 

KWA kipindi cha miaka takriban miaka 88 kuanzia mwaka 1930 ilipoundwa Kamati ya Lugha ya Kiswahili ikiwa na lengo la kusanifisha lugha ya Kiswahili kwa ajili ya matumizi katika shughuli mbalimbali za mawasiliano rasmi, juhudi nyingi za kukiendeleza zimefanyika. Tangu mwanzo, kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa lugha  ni kuona kwamba matumizi ya lahaja takriban 16 za Kiswahili zilizoainishwa, ni lahaja moja tu ndiyo iliyokubaliwa kuwa ni msingi wa usanifishaji. Lahaja ya Kiunguja ndiyo iliyoainishwa kuwa ndio iwe msingi wa usanifishaji kutokana na sababu kadhaa. Sababu ya kwanza ni kutokana na kuenea kwake katika eneo kubwa la Afrika Mashariki na Kati kutokana na njia mbalimbali.

Kuenea kwa lugha ya Kiswahili kulifanywa na wafanya biashara waliotoka pwani na kwenda bara wakifuata pembe za ndovu, madini na pia watumwa.  Wafanyabiashara hawa waliandamana na wenyeji wa pwani waliotumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Wengine waliochangia ueneaji wa lugha ya Kiswahili ni wamisionari waliotumia lugha ya Kiswahili katika kueneza neno la Mungu kwa kutumia mahubiri, machapisho na elimu.

Wamisionari walichapisha vitabu wa kufundishia na kujijifunzia ikiwa ni pamoja na kamusi, vitabu vya sarufi pamoja na vijarida. Lengo lilikuwa ni kuboresha uenezaji wa Kiswahili sanifu kinachoweza kutumika katika eneo kubwa kwa ulinganifu ulio sawa.

Juhudi zao ziliendelezwa na Wakoloni ambao walitaka kuwa na watumishi wenye uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa lengo la kuwasaidia kazi za utawala.

Magazeti yaliyoanzishwa enzi za ukoloni mbali na kueneza harakati za utawala wao, yalikuwa na azma ya kukieneza na kukiimarisha Kiswahili katika nyanja zake zote.

Inasikitisha kuona kuwa juhudi zao bado hajijazaa matunda yaliyotarajiwa kwani idadi kubwa ya wananchi hasa wasomi wamekuwa ni vinara wa kukipotosha Kiswahili wakati wa mawasiliano rasmi. Kwa mfano ukisoma katika maandishi ya Kiswahili kama vile nyaraka mbalimbali, vitabu na magazeti utagundua makosa mengi ya kisarufi kama matumizi mabovu ya maneno, maendelezo ya maneno yasiyo sahihi, mpangilio wa maneno kwenye sentensi na pia matumizi mabovu ya alama za uandishi kama nukta, mkato, semikoloni, koloni, alama za mshangao na hasa matumizi ya herufi kubwa.

Katika mapitio ya maandishi kwenye magazeti ya Kiswahili kama Mwananchi, Nipashe, Mtanzania nk. kwa upande wa Tanzania pia Taifa Leo, gazeti pekee la Kiswahili linalochapishwa na Kampuni ya Nation Media Group nchini Kenya, mbali ya yale ya udaku na burudani kuna makosa ya aina mbalimbali yaliyoonekana. Nitatoa mifano michache. Vichwa vya habari kwenye makala kwa baadhi ya miundo ifuatayo ilionekana ambayo ni matokeo ya kazi isiyoridhisha ya wahariri kama ‘sub editor’:

“Upigaji mabilioni serikalini waibuka.” Ukitaka kuelewa kilichoandikwa ni muhimu usome makala yote ndipo upate maana iliyokusudiwa. Maana yake ni kuwa wizi mkubwa wa mabilioni umegunduliwa serikalini. 

“Tahadhari na gonjwa lililoibuka.”

Ni dhahiri kuwa ugonjwa wa Ebola umetokea katika nchi jirani ya DR Kongo na kuwafanya viongozi wa Serikali hasa wa Wizara ya Afya kutaharuki. Wametoa tahadhari kwa wananchi kuwa waangalifu. Pamoja na kwamba Ebola ni ugonjwa wa hatari haina maana kwamba tuna haki ya kuharibu lugha ya Kiswahili wakati wa kuuelezea. Neno gonjwa si sahihi. Sahihi ni ‘ugonjwa’ na halipo neno ‘gonjwa’ kwa maana ugonjwa mkubwa.

“PM aagiza wanaume kupima miezi sita”. Maana ya sentensi hii ni kuwa Waziri Mkuu ameagiza wanaume wote wapime virusi vya Ukimwi ndani ya miezi sita. Nao wabunge wakaitikia wito huo wakiwa bungeni jijini Dodoma. Si sahihi kutumia kifupisho cha Prime Minister (PM) badala ya Waziri Mkuu. Wasomaji wengi hawana uelewa na kifupisho PM. Pili, haikubaliki kutumia vifupisho vya lugha ya Kiingereza katika maandish ya Kiswahili.

“Homa ya Bonde la Ufa ni hatari, usiwapo mzaha.”

Neno lenye mushkeli hapa ni ‘usiwapo’. Neno sahihi ni ‘usiwepo’. Baadhi ya waandishi huchanganya maneno ‘wapo na wepo’ bila kuyatofautisha. Kwa muktadha huu, neno sahihi ni wasiwepo badala ya wasiwapo.

Kuna baadhi ya waandishi wanashindwa pia kutumia kwa usahihi neno wimbo na badala yake hutumia mimbo na wakati mwingine hulitumia vibaya kwenye sentensi. Vilevile wingi wa neno wimbo ni nyimbo na kimatumizi tunaandika, “Nyimbo zangu zimevuja badala ya kuandika ‘nyimbo yangu imevuja’ kama ilivyoandikwa  kwenye gazeti moja maarufu jana likimnukuu mbunge mmoja akizungumza. Alisema, “Nyimbo yangu imevuja lakini jana Basata wameufungia wimbo wangu.” 

Haya ni matumizi mabaya ya kisarufi ambayo hayakubaliki hasa yanapotolewa na watu maarufu kama wabunge.