Sifa za kimsingi zinazoitofautisha lugha ya binadamu na aina nyingine za mawasiliano

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, November 19  2018 at  06:38

Kwa Muhtasari

Sifa au tabia za kimsingi zinazoitofautisha lugha ya mwanadamu na aina nyingine za mawasiliano zitumiwazo na wanyama ni pamoja na unasibu, na uzalikaji au ubunifu.

 

KUNA sifa au tabia za kimsingi zinazoitofautisha lugha ya mwanadamu na aina nyingine za mawasiliano zitumiwazo na wanyama. Sifa hizo ni kama zifuatazo:

Unasibu

Jinsi tulivyofafanua, unasibu wa lugha ya binadamu unajikita katika vigezo vifuatavyo:

Binadamu hazaliwi na lugha, anakutana nayo kwa unasibu tu.

Hakuna uhusiano wa moja kwa moja au wa asili kati ya kitaja (neno kama umbo la kiisimu) na kitajwa (kitu au umbo linalomaanishwa au maana).

Uhusiano wake ni wa unasibu na unatokana na makubaliano ya watumiaji wa lugha fulani.

Hata makubaliano haya ya kwamba kitu kiitwe au dhana fulani iitwe na kuelezwa kwa namna fulani ni ya nasibu tu.

Kila jamii lugha ina namna yake ya kuufasili na kuuelezea ulimwengu kwa lugha yake ambayo inatofautiana na jamii lugha nyingine.

Uzalikaji au Ubunifu

Uzalikaji katika lugha ya binadamu unajidhihirisha katika mambo yafuatayo:

Uwezo wa mwanadamu kubuni na kuunganisha maneno na miundo mbalimbali ya tungo bila kikomo.

Uwezo wa mwanadamu kutunga na kuzielewa tungo mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile ambazo hajawahi kuzisikia wala kuzitunga.

Uwezo wa mwanadamu kuelewa tungo zilizotungwa na watu wengine na kufahamu maana ya kisemantiki na ile ya kipragmatiki.

Uwezo wa mwanadamu kuzielewa tungo sahihi na zile zisizo sahihi.

Hivyo, uwezo huu unatofautiana na aina nyingine za mawasiliano zinayotumiwa na wanyama wengine.

Uambukizaji wa utamaduni

Lugha ya mwanadamu ina uwezo wa kuambukiza utamaduni kutoka katika kizazi kimoja kwenda kizazi kingine au kutoka katika jamii lugha moja kwenda katika jamii lugha nyingine.

Ni muhimu kufahamu kwamba, uwezo huu wa kuambukiza maarifa ya lugha hufanyika kwa njia ya kusoma au kujifunza na sio kurithi. Kwa mfano, mtu anaweza kurithi maumbile kutoka kwa wazazi wake, mathalani aina ya nywele, aina ya macho, lakini mtu hawezi kurithi lugha.

Lugha inamfikia kwa kuambukizwa katika jamii lugha anayokulia. Aidha ni vyema kukumbuka kwamba ingawa mwanadamu anazaliwa na ule uwezo (kitengo cha lugha) wa kujifunza lugha kama anavyoeleza mwanaisimu Noam Chomsky, lakini hazaliwi na lugha. Hii ndiyo sababu mwanadamu anaweza kujifunza lugha yoyote ile na kwa wakati wowote maadamu yupo katika mazingira na hali ya kawaida na saidizi.

 

Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe:

marya.wangari@gmail.com