http://www.swahilihub.com/image/view/-/3320734/medRes/1393871/-/107lsh2/-/EAC+FLAG.jpg

 

Mustakabali wa maendeleo ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Picha/ HISANI 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22  2017 at  15:13

Kwa Mukhtasari

WAKATI wa kipindi cha kupigania uhuru nchini Tanganyika na kwa kiasi kikubwa Kenya, Kiswahili ndiyo lugha iliyotumiwa kuwaunganisha wakazi wa mataifa hayo.

 

Harakati za siasa zilipoanza kupamba moto nchini Tanganyika, lugha ya Kiswahili ilikuwa 'silaha’ madhubuti iliyotegemewa na chama cha Tanganyika African Association (TAA) kupigania ukombozi.

Isitoshe, Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilipoanzishwa rasmi 1954, viongozi wake walilazimika kutumia Kiswahili mikoani na wilayani kuwashawishi wananchi kujiunga na harakati za ukombozi.

Ni sehemu chache sana ambapo lugha za kikabila zilitumiwa na kuhitaji mkalimani wa Kiswahili. Kwa maana hiyo, Kiswahili kilikuwa ni alama ya umoja, uzalendo na uhuru.

Hapa Kenya wakati wa utawala wa Uingereza, Kiswahili kilitumika katika baadhi ya shule za msingi hasa maeneo ya Pwani. Kiswahili kilitumiwa sana wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Wakoloni wa Uingereza walipobaini kuwa Kiswahili kinatumiwa kama nguzo ya umoja wa Wakenya, walianza kukipiga vita na kushauri lugha za makabila zitumiwe kufundishia katika shule za msingi kwa lengo la kuvunja umoja wa Wakenya.

Viongozi wa KANU na hasa Hayati Mzee Jomo Kenyetta alitumia sana Kiswahili wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Kenya.

Kwa upande wa Uganda, Kiswahili kilipigwa vita na wamishionari na pia watawala wa Baganda wakidai kuwa ilikuwa lugha iliyotumiwa sana na wafanyabiashara hasa Waarabu na hivyo ikahusishwa na dini ya Kiislamu na biashara ya watumwa. Pamoja na pingamizi zilizokuwapo, Kiswahili kiliendelea kutumiwa na majeshi (ya ulinzi na polisi).

Baada ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru (Tanganyika 1961, Uganda 1962, Kenya 1963 na Zanzibar 1964 baada ya mapinduzi), kila nchi ikawa na kipaumbele chake katika sera ya lugha.

Nchini Kenya na Tanganyika, Kiswahili kilitumiwa kujenga umoja na kilifanywa lugha ya taifa katika nchi hizi mbili.

Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya kufundishia masomo yote katika shule za msingi na pia kuwa somo la lazima kuanzia darasa la kwanza hadi la saba nchini Tanganyika.

Kwa upande wa sekondari, Kiswahili kilitumiwa kama somo la kutahiniwa kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne na kwa Kidato cha Tano na Sita likawa somo la hiari.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanganyika katika kukiendeleza na kukikuza Kiswahili ni kwa kuanzisha asasi kadhaa ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa TUKI inajulikana kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).

Aidha, ilianzishwa Idara ya Kiswahili kwa ajili ya kufundisha fasihi na isimu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuundwa kupitia kwa Sheria ya Bunge, 1970, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (1975), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) mnamo 1976, Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) nchini Zanzibar kwa minajili ya kufundisha, kukuza na kuendeleza Kiswahili na pia lugha za kigeni kama vile Kiarabu, Kifaransa, Kireno, Kijerumani na Kiingereza na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) mnamo 1977.

Nchini Kenya, Kiswahili kilipata msukumo mkubwa baada ya Rais Jomo Kenyetta kutoa kauli kuwa Kiswahili kinafaa kuwa lugha ya taifa na kuwa baadaye kingekuwa lugha ya mawasiliano katika Bunge.

Mnamo 1975, Kiswahili kilianza kutumiwa katika Bunge la Kenya. Ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Bunge la Kenya ilimtuma mtaalamu wake kuja Tanzania kuonana na viongozi wa BAKITA ili kushauriana kuhusu istilahi zilizosanifiwa na kukubaliwa kuwa istilahi rasmi za BAKITA na kuwianisha orodha hiyo na ya Kenya.

Inafahamika kuwa vyuo vikuu vyote vya serikali nchini Kenya vilivyoanzishwa miaka ya 1980 vinafundisha somo la Kiswahili kwa kutumia Kiswahili. Mifano hai ni Chuo Kikuu cha Nairobi, baadaye Chuo Kikuu cha Kenyatta na cha Moi. Kwa utaratibu huu, idadi ya wahitimu wa Kiswahili wa kiwango cha digrii ya kwanza nchini Kenya ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wahitimu wa Kiswahili kutoka Tanzania.

Kuna wanafunzi wa Kiswahili nchini Kenya walioungana na wenzao wa Tanzania na kuanzisha chama cha kukuza Kiswahili katika vyuo vikuu (CHAWAKAMA). Chama hiki kinawaunganisha wanafunzi wote wa Kiswahili wanaosoma katika vyuo vikuu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Huandaa semina na warsha za Kiswahili kila mwaka na hukutana katika nchi wanachama kwa mzunguko.

Suala linalotokana na mfumo wa elimu ya Kenya wa 8-4-4 unawalazimisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kusoma Kiswahili kama somo la lazima linalotahiniwa katika viwango vya taifa. Hatua hii iliwafanya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini Kenya kuona umuhimu wa lugha ya Kiswahili.

Kiswahili ni lugha muhimu katika masuala ya siasa, elimu, uchumi na utamaduni. Kwa maana hiyo, kina nafasi kubwa katika kupaisha maendeleo ya Afrika Mashariki. Tumeona kuwa Kiswahili kinawaunganisha watu na kuwaletea umoja. Hakuna lugha nyingine ambayo imeenea zaidi katika sehemu kubwa ya Afrika Mashariki kuliko Kiswahili.