Maenezi ya Kiswahili ikiwemo Kingozi kama asili ya Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, November 27  2018 at  11:11

Kwa Muhtasari

  • Madai yapo kuwa Kiswahili cha asili kilitokana na Kingozi au lugha ya Wangozi
  • Katika mapokezi mengi ya zamani, maneno ngozi, ngozini, na Wangozi hutokea kwa wingi. Asili ya kuitwa Wangozi ni kwa kuwa walikuwa wakipima mashamba kwa kanda ya ngozi

 

TUKIO lililoharakisha uhamaji ni mashambulizi ya kabila la Wagalla.

Uhamiaji kutoka Shungwaya ulitokea kwa mikondo na nyakati tofauti.

Baadhi ya Wabantu walielekea upande wa Magharibi, huku wengine wakienda Kusini.

Kikundi kinachounda makabila ya Gikuyu, Wameru,Waembu na Wakamba walifuata Mto Tana na kuanzisha makaazi katika eneo linalouzunguka Mlima Kirinyaga au Mlima Kenya kama unavyojulikana leo hii.

Wasegeju nao walielekea Kusini na kukalia eneo baina ya pwani na milima yaUsambara. Kikundi kinachojiita Wataita kilianzisha makazi kwenye milima ya Taita karibu na Mlima Kilimanjaro.

Kikundi kinachounda makabila ya Mijikenda kiliteremka Kusini kikifuata ukanda wa mwambao kama kilomita 40 upana kuelekea bara.

Hatimaye kikundi hiki kilianzisha maskani baina ya mji wa Malindi na Kusini ya Mombasa. Kikundi kingine, kilichounda kabila la Wapokomo kilielekea Kusini ya Mto Tana na kuanzisha makazi kati ya mito Tana na Galana au Athi. Kikundi kiitwacho Wangozi kilianzisha makaazi sehemu mbalimbali za ufuowa bahari kuanzia Kismayu (Kusini mwa Somalia) mpaka Sofala kule Msumbiji.

Wengine walivuka bahari na kuishi katika visiwa vya Lamu, Pate,Faza, Pemba, Unguja, Ngazija na Bukini.

Kupima mashamba

Waswahili wanadai kuwa Kiswahili cha asili kilitokana na Kingozi au lugha ya Wangozi. Katika mapokezi mengi ya zamani, maneno ngozi, ngozini, na Wangozi hutokea kwa wingi. Asili ya kuitwa Wangozi ni kwa kuwa walikuwa wakipima mashamba kwa kanda ya ngozi.

Aidha, walikuwa wakiishi katika mji wa zamani ulioitwa Ngozi. Mapokezi ya Bwana Abdallah Barua ni kuwa mashairi ya Hamziya ni Kingozi cha kati ya Kivumba na Kingozi cha mwisho. Kingozi cha kwanza hakipo tena.

Kingozi chasemekana kilianza kaskazini katika penya za visiwa vyaMagunyani, Pate, Faza na Lamu na kushukia mpaka mipaka ya Mto Tana.Waarabu walipofika upwa wa Afrika Mashariki katika karne ya 10 BK,waliwakuta Wangozi waliokuwa wamestawi kijamii na kibiashara.

Walizikuta lahaja za lugha zilizokuwa zinafanana wakaziita swahil, yaani lugha za pwani au watu wa pwani. Baadaye, neno hili lilitoholewa kuwa Swahili. Lugha ya wenyeji wa pwani ilianza kuitwa Kiwashili.

 

 

 

Marejeo:

Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, pp.248-52.

Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178.