Maingiliano ya biashara katika kusambaa kwa Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, November 27  2018 at  11:22

Kwa Muhtasari

Mtagusano miongoni mwa wafanyabiashara na wateja wa bidhaa na huduma ulikuwa na mchango mkubwa katika kusambaa kwa Kiswahili.

 

KUTANGAMANA kwa kibiashara na kijamii kati ya wenyeji wa pwani na wageni yaliendelea kwa karne nyingi.

Maingiliano hayo yalileta athari kubwa kwa lugha na utamaduni wa Waswahili. Kwa mfano, Waswahili wengi walisilimu na kuwa Waislamu.

Aidha, idadi kubwa ya maneno ya Kiarabu yaliingizwa katika lugha ya Kiswahili. Uchunguzi wa isimu historia na isimu linganishi uliofanywa na Malcolm Guthrie mwaka wa 1948 unaonyesha kuwa Kiswahili kina uhusiano na lugha nyingine za Kibantu hasa tunapotazama mashina na mizizi ya maneno meng ikutoka lugha mbalimnali za Kibantu.

Maneno ya asili kama vile kichwa,mkono, maji, njia na majina ya wanyama katika lugha hizi yanahusiana, na hivyo kubainisha kuwa yalitoka kitovu kimoja. Jambo lingine ni kuwa Kiswahili kina irabu (vokali) tano kama zilivyo lugha nyingi za Kibantu. Irabu hizi ni a, e, i, o, u.

Hali kadhalika, muundo wa msamiati wa Kiswahili kimsingi huchukua konsonanti – irabu (KI). Kwa mfano; karatasi, baba, kamata. Hata hivyo, konsonanti mbili, tatu au nne zinaweza kufuatana. Kwa mfano; pwani, nywele, mchwa.

Mpangilio wa nomino za Kiswahili huleta uwiano wa kisarufi na huitwa ngeliza nomino. Hujitokeza katika lugha nyingine za Kibantu. Mfano wa mpangilio wa nomino hizi ni ngeli ya A-WA, KI-VI, U-I, LI-YA. Nomino hizi zinapotumiwa katika lugha ya Kiswahili huwa na uwiano na vitenzi. Jambo hili pia hutokea katika lugha nyingine za Kibantu, na kudhihirisha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kibantu.

Dhana kwamba Kiswahili kilitokana na Kingozi

Katika maoni ya fasihi simulizi, asili ya Kiswahili ni Kingozi. Mashairi ya Hamziya yaliyoandikwa katika Karne ya 18 yaliandikwa kwa Kingozi.

Kingozi kilikuwa kikizungumzwa sehemu iliyoitwa Uswahili; upande wa visiwa vya Magunyoni (Pate, Lamu, Faza) hadi bara kupakana na Mto Tana.

Asili ya neno Kiswahili inasemekana ilitokana na kijana wa Kingozi aliyeulizwa na wageni kutoka Uarabuni kuwa wao ni kina nani, naye akajibu kuwa ‘’Sisi ndio wenye siwa hili.’’Yaani wenyeji wa kisiwa hiki. Kutegemea wakati na matamshi, jina hili lilibadilika na kuwa Waswahili.

 

 

Marejeo:

Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, pp.248-52.

Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178