Bado kuna makosa mengi katika machapisho ya Kiswahili

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Tuesday, October 31  2017 at  13:24

Kwa Muhtasari

Ni ukweli usiopingika kwamba kusahau ni jambo la kawaida na hivyo hatuna budi kukumbushana.

 

NI ukweli usiopingika kwamba kusahau ni jambo la kawaida na hivyo hatuna budi kukumbushana.

Pia ni jambo lisilopingika kwa mwanataaluma yeyote hujifunza mambo mapya hasa katika enzi hii ya sayansi na teknolojia.

Kwa hiyo maelezo na ufafanuzi ninayotoa ni kwa manufaa ya kila mmoja wetu.

Kwa kuanzia angalia sentensi zifuatazo:

“Tatizo la uhaba wa madawati limetamalaki kiasi cha kuhatarisha mustakabali wa elimu.”

Pengine mwandishi alilisikia neno ‘kutamalaki’ na kuanza kulitumia bila kuwa makini. Maana ya kutamalaki ni kuwa na mamlaka ya kitu fulani, kumiliki, kutawala. Kwa maana hiyo tatizo la uhaba wa madawati haliwezi kutawala au kumiliki kitu. Hivyo, suala la madawati ni tatizo la muda mrefu linalohatarisha mustakabali wa elimu nchini.

“Lakini muda uliopangwa kwa ajili ya vikao vya kamati uliisha jana”.

Neno lakini ni kiunganishi ambacho huunganisha vifungu vya maneno kama vishazi au virai. Kwa maana hiyo kiunganishi hakianzi kwenye sentensi kama ilivyo hapo juu.

Waandishi wengi wa Kiswahili wamezoea sana mtindo huu wa kuanza sentensi kwa kutumia neno ‘lakini’. Hili ni kosa.

Kwa usahihi ingefaa kama mwandishi angeanza kwa kutumia maneno kama ’hata hivyo’. Sentensi ingesomeka,

“Hata hivyo, muda uliopangwa kwa ajili ya vikao vya kamati uliisha jana.”

“Dkt Ave Maria Semakafu aliwakatisha wanawake waliokuwa wanaimba Wimbo wa Taifa kwenye mkutano wa mtandao wa Wanawake na Katiba uliofanyika mjini Dodoma kwa madai kuwa wamekosea kuuimba.”

Msomaji wa kawaida hataweza kuelewa kama kuna tatizo ila mtaalamu wa lugha akisoma kwa jicho la kiuchunguzi atabaini kuwa matumizi ya neno kukatisha yametumika kimakosa. Neno sahihi ambalo angetumia ni kukatiza badala ya kukatisha. Kukatiza maana yake ni kuingilia kati jambo kama mazungumzo, kusimamisha shughuli bila kuimaliza au kupita njia ya mkato. Kwa upande wa sentensi hiyo hapo juu maana yake ni kuingilia kati kitendo cha kuimba.

“Leo nawaletea ‘desert’ ambayo kwa Kiswahili ni kitinda mlo.”

Haipo haja ya kuandika neno la Kiingereza halafu unatoa kisawe chake kwa Kiswahili. Kwa maana hiyo neno ‘desert’ halikuandikwa mahali pake. Liko neno jingine tena ambalo lina maana ya ‘desert’ nalo ni ‘pudding’. Kwa Kiswahili tunalo neno linalojulikana kama ‘kitinda mlo” yaani kinacholiwa cha mwisho kwenye mlo. Kwa ufasaha ingeandikwa.

“Leo nawaletea kitinda mlo.”

“Jingine muhimu ni chakula kinachoganda juu ya ulimi. Wengi hujaribu kukiondoa kwa kutumia mswaki.”

Mwanzo wa sentensi una kasoro kwani ingeanza na nomino badala ya neno jingine. Angeanza kuandika ‘jambo’ jingine. Kosa la msingi ni upatanishi wa kisarufi. Ikiwa tumetumia ‘chakula kilichoganda’ ingefaa isomeke,

“Jambo jingine muhimu ni chakula kinachoganda juu ya ulimi. Wengi hujaribu kukiondoa kwa kutumia mswaki.”

“Uzagaaji wa silaha ni tatizo ambalo serikali inapaswa kulitafutia dawa sasa.”

Ijapokuwa neno uzagaaji linaweza kutumika, ni bora zaidi kama ingekuwa ‘kuzagaa kwa silaha…’ Kwa hiyo isomeke,

“Kuzagaa kwa silaha ni tatizo ambalo serikali inapaswa kulitafutia dawa sasa.”

“Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi ni mjumbe wa Chama cha Riadha Tanzania (RT).

Ili kuiboresha sentensi hii isiwe na utata tungeweza kuandika,

“Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha   Riadha Tanzania (RT).

“Ndege  ilikuwa imedunguliwa kwa kugongwa na kitu kizito.”

Kwa kawaida ndege inatunguliwa kwa maana ya kupigwa aghalabu na risasi au kitu kinachoruka angani na kukiangusha.  Kwa mfano wanajeshi wametungua ndege ya maadui. Kwa hiyo kudungua si Kiswahili fasaha. Ama kwa neno gongwa na kitu kizito si sahihi kwani kugonga ni kukutanisha kitu kimoja na kingine kwa kuvikutanisha. Inavyoeleweka ni kuwa ndege ilipigwa na kitu kizito. Kwa hiyo isomeke,

“Ndege ilikuwa imetunguliwa kwa kupigwa na kitu kizito.”

Stephen Maina

Nambari za Simu: 0754 861664 / 0716 694240