http://www.swahilihub.com/image/view/-/4844174/medRes/2117300/-/5pxuip/-/chepeo.jpg

 

Mapambo, maana na madhumuni ya kuyavalia

Chepeo

Picha ya mnamo Septemba 20, 2018 ya Bw Antony Mwangi ni muoshaji na mpigaji pasi chepeo mtaani Githurai 45, Kiambu. Picha/SAMMY WAWERU 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  13:20

Kwa Muhtasari

Mapambo huwa na umuhimu mkubwa kwa mtu anayejali mwonekano wake.

 

MAPAMBO yanaweza kuelezewa kama vitu vinavyovaliwa na watu kuongeza uzuri au urembo na kuwafanya wavutie machoni pa watu wengine.

Mapambo pia yanaweza kufafanuliwa kama vitu vya nakshi ambavyo huvaliwa mwilini au hata kwenye nguo alizovaa mtu. Mapambo hutumika kuashiria vitu vyovyote vinavyotumika kumpamba mtu.

Mapambo hutumiwa hasa na wasichana, wanawake au wanamitindo waliobobea katika tasnia ya fashoni laikini pia kuna mapambo yanayovaliwa na wanaume.

 

Malengo ya kuvalia mapambo

Mapambo huvaliwa kwa madhumuni mbalimbali jinsi ifuatavyo:

 1. Kuonyesha hadhi ya mtu kama vile tajiri mwenye uwezo wa kujipamba kwa vito vya thamani.
 2. Kumfanya mtu kuonekana wa kuvutia zaidi machoni pa watu
 3. Katika baadhi ya jamii, mapambo fulani hutumika kumkinga mtu kutokana na uchawi
 4. Mapambo hutumika kumtambulisha mtu kwa kuonyesha ni mmoja wa kikundi fulani cha jamii au dini

 

Kuna aina tele za mapambo yanayovaliwa katika sehemu mbalimbali za mwili kama vile usoni, mikononi, kwenye kiuno, miguuni na kadhalika.

Ifuatayo ni orodha ya aina mbalimbali ya mapambo pamoja na sehemu za mwili yanakovaliwa.

Kichwani – taji au shela

Usoni – chale/tojo/gema/nembo/taruma, ndonya, jebu/ukaya, kigwe, barakoa, wanja

Shingoni – mkufu, kidani, ushanga, tai

Puani – kipini, kishaufu/kikero/hazama/shemere

Sikio – kipuli/bali/herini, mapete, pingo

Mikononi – bangili, pete, hina, wanja, usinga, nembo, kikuku, kekee, pochi, Jaribosi

Kiunoni – masombo/kibwebwe, mshipi, kogo

Miguuni – furungu, hina, milia, udodi, njuga, wanja

Mapambo haya yanaweza kufafanuliwa jinsi ifuatavyo:

 1. wanja - ni rangi nyeusi ya majimaji au ungaunga inayotumika na wanawake kupaka machoni, usoni, mikononi na hata miguuni.
 2. rangi ya midomo - ni rangi inayopakwa kwenye midomo na wanawake.
 3. ukaya au jebu – ni nguo au kitambaa kinachovaliwa kukinga sehemu ya mdomo hasa na wanawake Waislamu.
 4. taji  - ni kofia inayovaliwa na wafalme, watawala au washindi kuashiria cheo chao au ushindi wao.
 5. saa - kifaa cha kupimia wakati kinachovaliwa mkononi kama pambo.
 6. poda - ni rangi nyeupe, laini itumiwayo na wanawake kujipaka.
 7. nywele bandia - ni nywele za kununua zinazovaliwa na kina dada ili kujiongezea urembo.

Marejeo:

Swahili English dictionary

Kamusi ya TUKI