Matawi mbalimbali ya Isimu Pweke katika Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  07:56

Kwa Muhtasari

Tunaendeleza mada ya isimu kwa kuchambua kwa kina istilahi na matawi mbalimbali ya tawi la isimu pweke.

 

KATIKA makala iliyotangulia, tulianzisha uchambuzi wa mada kuhusu isimu pamoja na matawi yake mbalimbali.

Hii leo tutaendeleza mada hii kwa kuchambua kwa kina istilahi na matawi mbalimbali ya tawi la isimu pweke.

Jinsi tulivyotaja awali, tawi la isimu pweke limegawika katika vitengo vidogovidogo ambavyo tutavyainisha kwa njia ifuatavyo:

FONETIKI

Hiki ni kipengele cha isimu pweke kinachoshughulikia vitamkwa katika lugha. Inaweza pia kufafanuliwa kama taaluma ambayo hutafiti, huchanganua na kutoa ufafanuzi kuhusu utamkaji na usikivu wa sauti zote kama zinavyoweza kutamkwa katika kinywa cha binadamu, pasipo kujali iwapo sauti hizo ni za lugha gani.

Kipashio cha msingi katika taaluma hii hujulikana kama fonimu.

Fonimu

Hizi ni sauti zinazotokea katika nafasi au mazingira yale yale na kubadili maana aliyokusudia msemaji husika. Kwa mfano, mzungumzaji wa Kiswahili akisikia maneno sindano na shindano yakitamkwa ataelewa mara moja kuwa maneno hayo yana maana tofauti kabisa.

Ataelewa kuwa sindano ni kifaa cha kushonea au kudungia ilhali shindano ikiwa ni aina ya mchezo unaochezwa ili kupata mshindi.

Tofauti katika maneno haya inatokana na sauti /s/ na /sh/ zinazotokea mwanzo wa maneno. Kwa hivyo, katika mfano huu /s/ na /sh/ kila moja ni fonimu.

 

Alofoni

Ni fonimu inayotokea katika mazingira ya kiisimu ya fonimu nyingine bila ya kubadilisha maana. Wakati mwingine sauti zinaweza kubadilisha nafasi lakini bila kubadili maana ya maneno. Kwa mfano, wazungumzaji wazungumzaji wa Kiswahili wenye matatizo ya lafudhi huweza kusema:

mbalambala – badala ya barabara

lafiki – badala ya rafiki

yuu – badala ya juu

azabu – badala ya adhabu

rishiti – badala ya risiti lakini maana hazibadiliki.

 

Sauti hizi ni sura mbili za fonimu moja au ukipenda ni alofoni za fonimu moja.

Alama za fonimu huonyeshwa kwa kupitia ishara ya mistari miwili mathalan /b/ huku alofoni zikionyeshwa kwa kutumia mabano ya mraba kama vile [z].

 

Fonimu imegawika katika vitengo viwili ambavyo ni irabu na konsonanti. Aidha, fonetiki inasheheni matawi manne madogo madogo ambayo ni:

  1. Fonetiki matamshi
  2. Fonetiki akustika
  3. Fonetiki masikizi
  4. Fonetiki tiba matamshi

 

 

Marejeo

Whiteley, H. (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen and Company Limited.

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M., (1977) Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.