Matawi ya Fonetiki, Ala za sauti za Lugha

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  12:09

Kwa Muhtasari

Fonetiki ni taaluma ya kisayansi inayochunguza sauti za lugha ya mwanadamu bila kujiegemeza kwa lugha yoyote mahususi.

 

IMEENDELEA

 

3. Fonetiki Masikizi

Kwa mujibu wa Massamba, et al (2007), hili ni tawi linalojishughulisha na jinsi utambuzi wa sauti mbalimbali za lugha unavyofanywa na uhusiano uliopo baina ya neva za sikio, neva masikizi (hizi ni neva zinazohusika na usikiaji wa sauti) na ubongo.

Tawi hili huchunguza jinsi sauti zinavyosikika na kufasiliwa katika akili ya msikilizaji. Sikio la msikilizaji linapaswa kufasili sauti za lugha sawa sawa ili kuzitenga.

Hivyo basi, fonetiki masikizi ndilo tawi maalumu linalochunguza mchakato huu. 

 

4. Fonetiki Tiba-Matamshi

Tawi hili ni jipya zaidi kuliko hayo mengine. Tawi hili hujishughulisha na matatizo yanayoambatana na usemaji au utamkaji wa sauti na jinsi ya kuyatatua.

 

ALASAUTI

Ili kuelewa vyema sauti za lugha ni muhimu kujifahamisha na kuchunguza kwa kina alasauti za lugha.

Sauti hutamkwa wakati viungo mbalimbali vinavyohusika na utamkaji vinaathiri mkondo wa hewa inayoingia na kutoka mapafuni kupitia chemba ya kinywa au chemba ya mdomo (kinywa).

Viungo mbalimbali vinavyohusiana na utoaji wa sauti za lugha huitwa alasauti. Alasauti hizi zinajumuisha viungo vifuatavyo:

  1. Mapafu

  2. Koo

  3. Kongomeo

  4. Ulimi

  5. Paa la kinywa (kaa kaa gumu)

  6. Kaa kaalaini

  7. Ufizi

  8. Meno

  9. Midomo

  10. Pua

Kimsingi, kazi za ala za sauti sio kutoa sauti pekee, bali ni kuhimili uhai wa mwanadamu.

Ala za sauti hizi hata hivyo hushirikiana kwa namna mbalimbali kutoa sauti za lugha. Kama tulivyoeleza awali, viungo hivi pamoja na kuwa vinasaidia kutoa sauti, kazi yake ya msingi sio hiyo, bali kuna kazi za kibaiolojia ambazo viungo hivi vinafanya na vimeumbwa kwa ajili yake.

Hata hivyo sio kusema kwamba kazi ya utoaji wa sauti ni ya ziada. La hasha! Kwa kuwa mawasiliano kwa binadamu ni kitu muhimu basi viungo hivyo vinaongeza kazi nyingine na kuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa vinawezesha utoaji wa sauti za lugha.

Katika uzalishaji wa sauti, hewa inayotakiwa kwa utoaji wa sauti za lugha hutokea kwenye mapafu.

Misuli ya mapafu husukuma hewa mpaka katika chemba ya kinywa au pua kwa kupitia bomba la hewa linaloitwa koromeo.

Marejeo

Maddo, U., Thiong’o, D., (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.

Tumbo Masobo, Z.N., Chiduo, F.K.F. (2007). Kiswahili Katika Elimu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).

Mogambi, H., (2008). KCSE Golden Tips Kiswahili. Nairobi: Macmillan Kenya