http://www.swahilihub.com/image/view/-/3783476/medRes/1542363/-/g69s8p/-/goua.jpg

 

Matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali nchini

Mabati-Cornell

Idrissa Haji Abdallah, mshindi wa kwanza katika utanzu wa riwaya (aliyevaa kanzu na koti jeusi). Kushotoni mwake ni Hussein Wamaywa, mshindi wa pili wa utanzu wa riwaya na Ahmed Hussein Ahmed, kutoka Kenya, aliyesimama baina ya Mama Salma Kikwete na Abdilatiff Abdalla, ni mshindi wa kwanza katika utanzu wa ushairi. Picha/HISANI 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Thursday, February 9  2017 at  12:49

Kwa Mukhtasari

Wananchi wa nchi za Afrika Mashariki wana bahati kubwa ya kuwa na lugha ya Kiswahili ambayo imefikia katika hatua kubwa ya maendeleo.

 

RAIA wa nchi za Afrika Mashariki wana bahati kubwa ya kuwa na lugha ya Kiswahili ambayo imefikia katika hatua kubwa ya maendeleo.

Lugha hii imekamilika katika nyanja zake zote.

Nyanja hizi ni katika fani za isimu na fasihi.

Wataalamu wa kigeni kama vile Madan, A.C. aliyeandika Kamusi ya Swahili- English Dictionary mwaka 1903, Frederick Johnson aliyeandika Kamusi ya A standard Swahili-English na English Swahili Dictionary 1930, Bloomfield, P, M. aliyeandika Sarufi ya Kiswahili mwaka 1931) wengine wengi walituwekea misingi imara ya kiisimu ambayo pamoja na dosari zilizopo imetufikisha hapa tulipo.

Huu ni ushahidi tosha kuwa lugha ya Kiswahili imeendelea ikilinganishwa na lugha nyingine kubwa za Kiafrika kama Kihausa, Kiigbo na Kiwolof za Afrika Magharibi; Kizulu, Kishona za Afrika Kusini na lugha nyingine za Kiafrika zenye idadi kubwa ya wazungumzaji.

Pamoja na kuandika kamusi hizi baadhi yao walianza kuisanifu lugha ya Kiswahili kwa kuweka misingi ya kisarufi.

Utawala wa Kiingereza walianza kuisanifu lugha ya Kiswahili tangu miaka ya 1930 walipokutana ili kuhakikisha kuwa nchi za Uganda, Kenya na Tanganyika zinashirikishwa kwa kuunganishwa na kuwa na kamati moja ya kuisanifu lugha ya Kiswahili na kuwa na wawakilishi kutoka katika nchi hizo.

 

Utafiti

Wataalamu wazawa waliobobea katika sarufi ya Kiswahili nao wamejikita katika utafiti na uandishi kama Nkwera F.M.  (Sarufi na Fasihi ya Kiswahili kwa shule za sekondari na vyuo -1978), Kapinga, M.C. Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu- 1983), Massamba, D.P.B. Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu – 1999) na wengine walianza kujikita katika taaluma za fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia.

Wamejitahidi kufanya utafiti na kuongezea pale wageni walipoachia.

Matokeo yake ni kwamba wamewahamasisha wataalamu wa fani nyingine kuanza kuandika kwa Kiswahili ili kueneza taaluma zao kwa wasomaji wazawa wasiokuwa na ujuzi wa lugha ya Kiingereza.

Wako baadhi ya wataalamu waliojitahidi kuandika taaluma zao kwa Kiswahili ambao wanafaa kuigwa.

Huu ni mfano wa kuigwa kwani wametekeleza yale ambayo yalionekana hayawezi kutekelezwa. Wataalaumu hawa wamediriki kuandika vitabu vya kitaaluma kwa Kiswahili kama biashara, hisabati, kemia, fizikia, historia, jiografia na kadhalika.

Msaada mwingine waliopata ni kutumia istilahi zilizosanifiwa.

Istilahi hizi zilizoandaliwa wakati wa enzi za ukoloni hadi tulipopata uhuru wakati kila nchi ilipoamua kuwa na sera yake ya lugha.

Kwa upande wa Tanzania juhudi hizi ziliendelezwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na hatimaye kuunda Baraza la Kswahili laTaifa (Bakita) lililoundwa mwaka 1967. 

Tangu mwaka 1967 Bakita limekuwa likisanifu istilahi lakini matunda ya kazi hii kwa kipindi cha hiki karibuni hayajaleta mafanikio ya kuridhisha kutokana na ukata. Ilitarajiwa kuwa istilahi hizi zilizoandikwa zingetumika kukieneza Kiswahili kwa kuandika vitabu, majarida, makala na matini. Hilo halifanyiki.  Sababu yake ni kwamba hakuna msukumo wowote unaotoka kwa viongozi wa Chama na Serikali kwa kutunga sera na sharia zinazohusu matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

 

Vitendo

Jambo la kushangaza zaidi ni kwa viongozi hutoa kauli za kuunga mkono lugha ya Kiswahili lakini kivitendo hakuna chochote. Kwa kweli hakuna utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi wetu.

Inasikitisha kuona kuwa tangu miaka ya 70 suala la kuiendeleza lugha ya Kiswahili limekuwa zikisuasua. Waandishi hawajapata motisha wa kuandika vitabu vya taaluma kwa sababu haipo sera wala sheria inayoelekeza Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia.

Kwa hiyo wanaojitahidi kuandika kwa Kiswahili maandishi yao yanakosa sera iliyo wazi inayotoa mwelekeo kwa wananchi kuhusu lugha. Juhudi za viongozi wakuu ambao waasisi wa nchi wameonyesha uzalendo na mapenzi makuu ya Kiswahili ni kama Mwalimu J.K. Nyerere na Rashid Mfaume Kawawa.

Walihimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano, mawasiliano kwa simu and barua, kwa kuandika nyaraka mbalimbali na kwa kutoa matamshi yao. Viongozi wa sasa nao waunge mfano huu. Hatua hii itasaidia kukiendeleza Kiswahili katika uandishi wa vitabu vya kiada na ziada, matini na pia vielelezo vingine vya kufundishia.

Katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imetaja wazi nafasi ya Kiswahili katika mfumo mzima wa elimu.

Baada ya sera hii kutolewa, kinachotakiwa kufanyika ni kuandaa mipango thabiti ya utekelezaji ambayo itazingatia mambo yafuatayo:

Kwanza ni upatikanaji wa vitabu.

Vitabu vinaweza kupatikana kwa kuwahimiza wataalamu wazawa kuandika vitabu. Kwa kuwa zipo istilahi za kutosha za masomo mbalimbali na kwa kuwa Bakita wanaedelea kusanifisha istilahi za masomo mbalimbali, pawepo na ushirikiano kati ya Bakita na waandishi wa vitabu na majarida na Taasisi ya Elimu wanaotayarisha miongozo  ya mada za kufundishia. Jambo la msingi ni kuandika vitabu na majarida kwa kufuata mpangilio maalumu wa kuanzia kidato cha kwanza masomo ya sanaa kama uraia, historia na jiografia halafu kuendelea na masomo ya sayansi na hisabati.

Mbali na vitabu, eneo jingine muhimu ni kuajiri walimu weledi wa kutosha. Walimu waliopo wapigwe msasa kwa njia ya semina na warsha kulingana na mabadiliko a mitalaa. Idadi yao iongezwe kulingana na ongezeko la usajili wa wanafunzi wapya. Nao walimu tarajali watasomeshwa kulingana na mitalaa kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania. Wakaguzi na wakufunzi wa vyuo nao waelimishwe ili waende na wakati. Kutakuwapo na kipindi cha hekaheka za kusoma kwa watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufunndi kwa kuanzia na walimu walio kazini, wakufunzi wa vyuo, wakaguzi na walimu tarajali.

Njia ya tatu ni kutafsiri vitabu na makala za kitaaluma kama ilivyo katika uandishi wa vitabu. Ni jambo muhimu kufuata taratibu zote za kutafsiri mara inapoamuliwa aina ya vitabu vya kutafsiriwa kwa mfano kupata kibali cha mchapishaji ambaye naye atawasiliana na mwandishi wa kitabu.  (Itaendelea)

 

Simu ya kiganjani: 0754861664