http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842552/medRes/2164303/-/bplfvg/-/zanio.jpg

 

Mavazi

Sahara Abdi

Sahara Abdi, 28, akiwa amevalia baibui katika hii picha ya Februari 20, 2018; ndiye mwasisi wa Northern Voice Trust. Picha/HISANI 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  13:37

Kwa Muhtasari

Baibui ni vazi refu ambalo mara nyingi huwa la rangi nyeusi na huvaliwa na wanawake aghalabu wa mwambao juu ya nguo za kawaida, hasa wanapotoka nje ya nyumba.

 

NENO vazi linatokana na kitenzi kuvaa. Hivyo mavazi ni nguo zinazovaliwa na watu kwa minajili ya kufunika mwili au sehemu za mwili.

Mavazi huvaliwa kwa sababu tofauti tofauti jinsi ifuatavyo:

  1. Kukinga mwili dhidi ya hali hasi ya anga mathalan baridi, jua kali ikiwemo madhara mengine ya mazingira yanayoweza kuathiri vibaya afya ya nwili.
  2. Kuwasilisha ujumbe kwa watu wengine kwa kutambulisha mtu fulani na kundi mathalan kabila, jeshi, dini, timu jeshi na kadhalika au tabaka kama vile nguo ghali za matajiri au uraibu fulani kwa mfano unapopendelea nembo fulani.

 

Jambo la msingi ni kwamba mavazi hutegemea hali ya anga au mazingira ya mwanajamii.

Kwa mfano katika maeneo yenye joto,  mavazi huwa mepesi huku mahali kwenye baridi penye watu huvalia mavazi mazito zaidi.

Aidha, ni muhimu kufahamu kwamba kila utamaduni una aina yake mahsusi ya mavazi pamoja na mapambo.

Tamaduni mbalimbali zimepokea mavazi kutoka nje na kubadilisha mitindo yao kadri na mpito wa wakati.

Mavazi yanaweza kuwa ya aina nyingi mathalan sufi, ngozi, kitambaa, plastiki, na kadhalika.

Vilevile mavazi yanaweza kutofautishwa kwa misingi ya kijinsia, umri, kazi na majira.

Hii ni kumaanisha mavazi yanaweza kuwa ya ama wanaume au wanawake, mavazi ya watu wazima au watoto, mavazi ya kikazi au nyumbani, mavazi ya siku za kawaida au sikukuu.

Mavazi pia yanaweza kutofautisha kama ya sehemu ya juu au chini mwilini, mavazi ya sehemu mbalimbali za mwili mavazi ya nje nay a ndani mathalan chupi, shati, kaptura, rinda sokisi na kadhalika.

Kwa mintarafu hiyo, ni vyema kufahamu kwamba kuna aina anuai ya mavazi jinsi ifuatavyo:

Mavazi mbalimbali

1. Rinda - kanzu ya kike pana iliyokatwa kiunoni.

2. Kikoi - hufungwa kiunoni na kuteremka hadi miguuni.

3. Baibui - vazi jeusi linalovaliwa juu ya nguo nyingine.

4. Ubinda - hupitishwa baina ya mapaja.

5. Saruni - hufungwa kiunoni na kuteremka hadi miguuni.

6. Kibwebwe/mahazamu -hufungwa kiunoni.

7. Masombo -Huviringwa na kufungwa kiunoni.

8. Gagulo - kirinda kidogo.

9. Kanchiri/sidiria - huvaliwa kifuani.

10. Kaniki -kanga ya kujifunga wakati wa kazi.

Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: marya.wangari@gmail.com

Marejeo

Kamusi ya Elezo Huru

White, L. 1949. Ya Sayansi ya Utamaduni: Utafiti wa mtu na ustaarabu. New York: Farrar, Straus na Giroux.