http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197893/-/1a5cdcz/-/wangari.jpg

 

Mbinu ya tafsiri katika uundaji wa msamiati katika Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  14:50

Kwa Muhtasari

Tafsiri ni mbinu ya kuunda maneno ambapo maneno au vifungu katika lugha chanzi hufasiriwa katika lugha lengwa.

 

KWA mujibu wa Matinde (2012), tafsiri ni mbinu ya kuunda maneno ambapo maneno au vifungu katika lugha chanzi hufasiriwa katika lugha lengwa.

Ni vyema kutilia maanani kwamba tafsiri huzingatia muundo wa lugha pokezi jinsi ilivyosawiriwa katika mifano ifuatayo:

Jinsi tunavyofahamu, kutafsiri ni kutoa mawazo kutoka lugha chanzi hadi lugha pokezi pasipo kwa njia inayoeleweka na hadhira lengwa pasipo kubadilisha maana.

Mbinu ya tafsiri katika uundaji wa msamiati huwa faafu mno katika mazingira yafuatayo:

  1. Hali ambapo hapana neno mwafaka linaloweza kutumiwa kuiafiki dhana fulani ambayo imeibuka kutokana na maendeleo ya teknolojia na sayansi au iliyochipuka katika katika mazingira mageni.
  2. Hali ambapo pana dharura ya kutafutia istilahi geni msamiati ili kukidhi haja ya mawasiliano. Kwa mfano ili vyombo vya habari viwezi kuwavutia zaidi wasikilizaji, watazamaji au wasomaji zaidi iwezekanabyo, ni sharti taarifa zake ziwe za papo kwa hapo au zinazochipuka kadri matukio yanavyotendeka.

 

Aidha kuna baadhi ya matukio ambayo wanajamii wanapaswa kujuzwa kwa dharura ili kuchukua hatua ya haraka kwa mfano: mikurupuko ya maradhi, ajali, uhalifu, migogoro, vita na matukio mengineyo.

Ili kujitwalia umaarufu, ni sharti vyombo vya habari vijitahidi kutoa taarifa muhimu kwa hadhira yake bila kuchelewa au kupitwa na wakati na matukio.Si ajabu basi kwamba vyombo vya habari hugeukia mbinu ya tafsiri ili kuunda msamiati na tafsiri katika jitihada za kukabiliana na dharura ya mawasiliano.

 

Kiingereza                                                                     Kiswahili

Running mate                                                                Mgombea mwenza

Ruling party                                                                  Chama tawala

Free market                                                                   Soko huria

 

Ubora wa Tafsiri katika uundaji wa msamiati

Mbinu ya tafsiri huzingatia kigezo cha maana zaidi kuliko muundo wa maneno yaliyotwaliwa kutoka lugha chanzi na kutafsiriwa na huafiki utamaduni wa lugha lengwa. Hali hii husaidia katika kuunda maneno yenye maana iliyo wazi na inayokubalika katika lugha lengwa.

 

 

Udhaifu wake

Aghalabu huwa vigumu kutafsiri baadhi ya maneno kutoka lugha chanzi kwa kufuata kigezo maana.

Kuna uwezekano wa kupata tafsiri ambazo hazina maana wala mantiki katika lugha lengwa.

Kwa mfano:

 

Pool party  -    Sherehe ya kidimbwi cha kuogelea.

Things fall apart  -   Vitu vyasambaratika na kutapakaa

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

 

Ndungo, C. & Mwai, W., (1991). Kiswahili: Historical Modern Development in Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press.

Mbaabu, I., (1996). Language Policy in East Africa: A Dependency Theory Perspective. Nairobi: Educational Research and Publications.

Masebo, J.A. & Nyangwine A. D. (2002). Nadharia ya Lugha: Kiswahili 1. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com