http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197893/-/1a5cdcz/-/wangari.jpg

 

Tathmini ya kina kuhusu mchakato wa uundaji istilahi za Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  14:00

Kwa Muhtasari

Mchakato wa uundaji istilahi unahusisha vipengele, mifumo na fasili za dhana, zinazopaswa kushughulikiwa na wataalamu wa uwanja husika wa maarifa.

 

KWA mujibu wa Infoterm (2005), mchakato wa uundaji istilahi unahusisha vipengele, mifumo na fasili za dhana, zinazopaswa kushughulikiwa na wataalamu wa uwanja husika wa maarifa.

Naye Massamba (1997), anasema, jukumu la msingi la wataalamu ni kukusanya istilahi za uwanja husika katika lugha chanzi na kufafanua kwa usahihi dhana ya kila istilahi iliyokusanywa, ambapo pia wanaweza kupendekeza visawe vya istilahi hizo katika lugha lengwa.

Kutozingatiwa kwa vipengele kwa masuala ya mifumo dhana na ufafanuzi wa dhana kunaashiria kutohusishwa kikamilifu kwa wataalamu wa nyanja mbalimbali za maarifa katika mchakato uundaji istilahi za BAKITA.

Tukitazama Istilahi za Kiswahili (2005), tunaona kwamba BAKITA huwashirikisha wataalamu katika ngazi ya usanifishaji wa istilahi, wakati mwingine, bila kuzingatia upekee wa fani husika. Kwa mfano, usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili (2005), ambazo ni za nyanja zaidi ya thelathini, ulifanywa kwa kutumia jopo moja tu.

Ni bayana kwamba mkabala na mbinu za uundaji istilahi za BAKITA, kwa kiasi kikubwa zinalandana na zile zilizotumiwa na wanaleksikografia wa jadi, hususani wa Kiingereza, ambao walikusanya maneno magumu ya Kilatini na kuyatafutia visawe vya Kingereza katika muundo wa faharasa.

Kama anavyosema Mdee (1992: 11), mnamo karne ya 15 faharasa za aina hiyo ziliwekwa pamoja na kuchapishwa kama kamusi ya maneno magumu. Istilahi za Kiswahili (2005), chapisho lililotokana na kuunganishwa kwa faharasa za vijitabu 6 vya Tafsiri Sanifu, ni mfano mzuri wa kazi za aina hiyo.

Uundaji wa istilahi kwa upande wa TUKI ulikuwa na lengo la kukiwezesha Kiswahili kitumike katika elimu ya sekondari na ya juu kama wanavyoeleza Mwansoko et al (1992)

Naye Massamba (katika Kamusi ya Biolojia, Fizikia na Kemia,1990) ajnafafanua kwamba uhudi za mwanzo za uundaji wa kamusi ya istilahi za Kiswahili zilianza mnamo mwaka 1970 kwa uundaji wa istilahi za Biolojia. Juhudi hizo zilifuatiwa na uundaji wa istilahi za Fizikia, za Kemia na za Lugha na Isimu katika miaka ya 80.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U., Thiong’o, D., (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com