Mchango wa NMG katika ukuzaji wa Kiswahili

Ngulamu Mwaviro

Mshindi wa Tuzo ya Ubunifu 2016 Ngulamu Mwaviro; OGW (kati) akabidhiwa hundi na Bw Joe Muganda (wa pili kushoto), Afisa Mkuu Mtendaji wa Nation Media Group, Simon Sossion (kushoto) ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa Matbaa ya Spotlight, Balozi wa Ufaransa nchini Kenya, Antoine Sivan na Mwenyekiti wa Jopo la Tuzo ya Ubunifu, Profesa Ken Walibora. Picha/DIANA NGILA  

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Friday, September 29  2017 at  08:16

Kwa Mukhtasari

Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ni kampuni mama ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Kiswahili ya Mwananchi na Mwanaspoti na la Kiingereza, The Citizen.

 

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) ni kampuni mama ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Kiswahili ya Mwananchi na Mwanaspoti na la Kiingereza, The Citizen nchini Tanzania.

Kampuni ya NMG inamiliki kampuni tanzu zilizoko nchini Tanzania, Uganda na Rwanda zinazojishughulisha na uchapishaji wa magazeti na utangazaji kwa kutumia redio na runinga.

Kwa upande wa Kiswahili Kampuni hii inachapisha magazeti ya Taifa Leo na Taifa Jumapili nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania yako magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti. Pia ziko redio na runinga ambazo hutangaza kwa Kiswahili.

2.0 Historia fupi

Kampuni ya NMG ilianzishwa Mwezi Mei, mwaka 1959 huko Nairobi, Kenya kwa lengo la kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii ya Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla.

NMG inasimamia shughuli za utangazaji kwa kutumia redio na runinga, kuchapisha magazeti ya Kiingereza na Kiswahili.

Nchini Tanzania yako magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti ambayo ni ya Kiswahili na The Citizen ambalo ni la Kiingereza.

Magazeti haya yako chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Francis Nanai, Mhariri Mtendaji Mkuu Bakari Machumu, Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Frank Sanga,

Gazeti la Mwananchi lilianzishwa Mei 1999 na Balozi Ferdinand Rutihinda na baada ya miaka miwili aliliuza kwa Kampuni ya Nation Media Group mwezi Aprili 2000.

Nakala ya kwanza ilitolewa na kuuzwa kwa TSh150.00 kwa nakala moja ikiwa na kurasa 15.

Wakati huo nchini Tanzania kulikuwa na magazeti matatu tu ya Kiswahili ambayo ni Uhuru, Mfanyakazi na Kiongozi.

Ni gazeti la Uhuru pekee ndilo ambalo bado liko hai wakati mengine mawili yameshakufa.

Gazeti la Mwanaspoti lilianzishwa tarehe 12/2/2001 likiwa na kurasa 12 na kuuzwa kwa Sh100.00.

The Citizen lilianzishwa tarehe 16/9/2004 likiwa ni la tano kwa lugha ya Kiingereza katika Afrika Mashariki.

Gazeti la Mwananchi mbali na kuchapisha taarifa mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa huchapisha pia nyongeza ambayo ni matoleo mahsusi kuhusu masuala ya michezo yanayojulikana kama Spoti Mikiki (Jumatatu), Maarifa (Jumanne), Siasa (Jumatano), Uchumi/Biashara (Alhamisi), Afya (Ijumaa), masuala ya kijamii na Starehe (Jumamosi) na Johari kama urembo, sherehe, mapishi, harusi, mavazi na kadhalika (Jumapili).

Wasomaji wengi hulitumia gazeti la Mwananchi kama chanzo cha elimu na maarifa na shuleni na katika jamii kwa jumla.

Hutumika pia kama makala za marejeo kwa ajili ya kufundishia darasani.

3.0 Kukiendeleza Kiswahili

Tangu mwanzo NMG ilipoanza kuchapisha gazeti la Taifa Leo na baadaye Taifa Jumapili kwa lengo la kuwapa wasomaji wa Kiswahili katika nchi za Afrika habari, burudani na elimu, mafanikio yamekuwa makubwa kiasi kwamba magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti yakaendelea kukiiimarisha Kiswahili na kufikia hatua ya kuwa ni chanzo cha taaluma ya Kiswahili katika fasihi na isimu ya Kiswahili.

Sasa hivi gazeti la Mwananchi ni chapisho linalotumika kama rejea kwa walimu na wanafunzi wa Kiswahili.

Katika kukiimarisha Kiswahili, gazeti la Mwananchi limejikita katika kutoa mafunzo kwa wanahabari (waandishi na watangazaji) kutumia lugha ya Kiswahili iliyo sanifu na fasaha.

Kwa mfano, yako makosa mbalimbali yanayojitokeza katika magazezi na redio ambayo yanasababishwa na uelewa finyu kwa wanahabari hasa wanaotoka vyuoni.

Makosa yanayojitokeza katika magazeti, redio na runinga hukusanywa na kutolewa ufafanuzi na baadaye kuchapishwa katika gazeti kila wiki.

Pia semina, mikutano na kongamano hutumika kutolea ufafanuzi kuhusu makosa yanajitokeza ya upotoshaji wa lugha ya Kiswahili katika tahajia, miundo, maumbo ya maneno na matamshi.

Hatua ya kupigiwa mfano ni uanzishwaji wa tovuti ya Kiswahili inayojulikana kama Swahilihub yaani Kitovu cha Kiswahili.

Huu ni mfumo wa kidijitali wa swahilihub.com na ukitaka kufungua tovuti hii tumia www.swahilihub.com

Mfumo huu wa kidijitali husambaza masuala ya lugha kama fasihi na isimu.

Kwa mfano mashairi, tenzi, insha, methali, nahau, semi huwasaidia wanafunzi wa Kiswahili wa ngazi mbalimbali kuanzia msingi, sekonari na elimu ya juu. Pia habari, burudani, elimu na hupakiwa katika tovuti hii na wasomaji duniani kote hupata maarifa yanayopakiwa katika tovuti hii.

Njia nyingine za kidijitali zinazotumika ni kwa kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Instagram.

Lengo ni kuhakikisha kuwa matukio kama ajali, hotuba za viongozi wa nchi, maafa na masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanasambazwa kwa kutumia tovuti na mitandao hii.

Kwa kuwa lugha ya Kiswahili inakua, inatakiwa kufanyiwa utafiti wa kusaidia kurekebisha na kusahihisha ya mara kwa mara makossa yanayojitokeza.

Katika kufanya hivyo tumegundua kuwa kuna maneno na misemo inayotumika kimakosa.

Kwa mfano kuna maneno, misemo na miundo inayokanganya na hutumiwa na wanahabari.

Mkanganyiko huu unatokana
na athari ya lugha za asili na wakati mwingine athari ya lugha za kigeni hasa Kiingereza na Kiarabu kwa wasomi. Kwa mfano maneno yanayosomeka au kusikika katika redio na runinga huwapotosha wale wanaojifunza Kiswahili.

Iko mifano kama adhima na azma, ajali na ajari, ghorofa na gorofa, jinsi na jinsia, kazi na makazi, mazishi na maziko, mahari na mahali, loga na roga, jizatiti na jidhatiti, king’amuzi na kisimbuzi, tegemea na tarajia, na kadhali. Orodha hii ndefu sana.

Vilevile, iko mifano mingine ambayo inaonekana katika magazeti ya Kiswahili.

Kwa mfano kuongeza kiambishi cha awali kama –ma- kwa baadhi ya maneno kama ma/husianao, ma/shirikiano, ma/kampuni, ma/hospitali, ma/hoteli, maa/uamuzi na mengine ambayo wanasiasa wanapenda sana kuyatumia na waandishi huyatumia bila kuwa na umakini wowote. Kiambishi -ma- kinatumika kimakosa.

Kuhusu miundo ya Kiswahili isiyo sahihi tunayo mifano kama:
i) Anayekwenda kwa jina la… badala ya anayefahamika kama…
ii) Akizungumza kwa njia ya simu badala ya akizungumza kwa simu.
iii) Suala hili linapelekea badala ya suala hili linasababisha…
iv) Kinyume cha sheria badala ya kinyume na sheria.
v) Kusafiri na ndege badala ya kusafiri kwa ndege.
vi) Majira ya saa… badala ya saa… na kadhalika.
Matumizi ya alama katika uandishi nayo inakosewa. Kwa mfano nukta, nuktamkato, nuktapacha, nukyakatishi, mkato, kiulizo, mshangao, mnukuo, kiungio, kinyota, nk.
Matumizi ya herufi kubwa.
Kwa kweli makosa ni mengi na hatuna budi kutumia kila juhudi kurekebisha makosa haya.
Mifano mingine inayokanganya wasomaji itatolewa katika makala zijazo.

Simu ya Kiganjani: 0754 861 664 au 0716 694 240 (Tanzania +255)