Mchango wa tamthilia ya Kiswahili kutunga historia

Na ERASTO DUWE

Imepakiwa - Tuesday, January 24  2017 at  16:29

Kwa Mukhtasari

Fasihi ni njia mojawapo iwezayo kumjuza mtu historia ya jamii bila kujali ni fasihi simulizi au fasihi andishi.

 

JAMII yoyote hupitia katika vipindi mbalimbali vya historia.

Aghalabu tunapotaka kuifahamu historia ya jamii huwa tunatumia njia mbalimbali kupata taarifa husika.

Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na masimulizi kutoka kwa waliowahi kuwapo katika kipindi husika na kusoma vitabu vya historia.

Fasihi ni njia mojawapo iwezayo kumjuza mtu historia ya jamii bila kujali ni fasihi simulizi au fasihi andishi.

Katika makala ya leo tutaangazia mchango wa tamthilia ya Kiswahili katika kutunga historia ya jamii ya Watanzania.

Tunaweza kuigawa historia ya jamii ya Watanzania katika vipindi mbalimbali ambavyo wanajamii wamepitia.

Vipindi hivyo ni pamoja na kipindi cha kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni, baada ya uhuru, kipindi cha kukata tamaa ambacho hujulikana kama kipindi cha giza na wakati wa kushamiri kwa utandawazi.

Katika vipindi hivi vya kihistoria kuna matukio mbalimbali yaliyojiri.

Matukio hayo huakisiwa vyema na kazi mbalimbali za kifasihi kupitia vipengele vyake.

Katika kuonyesha dhima hii ya fasihi, tutatumia utanzu wa tamthilia kudhihirisha inavyoakisi historia ya jamii.

Kabla ya ukoloni, jamii nyingi zilikuwa na mila na desturi zao.

Zilijishughulisha na kazi mbalimbali kwa lengo la uzalishaji mali na kuzienzi mila na desturi za kupitia mivigha, jando, unyago matambiko na kadhalika.

Tamthilia faraguzi ya wakati huo ilijikita katika kuakisi shughuli zilizokuwa zikifanywa na wanajamii.

Katika kipindi cha ukoloni (1885-1960) shughuli za kijamii hazikuweza kufanyika ipasavyo kwa kuwa jamii ilikuwa katika migogoro mbalimbali na Wakoloni, awali Wajerumani na baadaye Waingereza.

Kuburudisha Wakoloni

Hata hivyo tamthilia ya wakati huo ililenga katika kuliburudisha tabaka la watawala wa kikoloni.

Baada ya uhuru maudhui ya kazi ya fasihi yalibadili mwelekeo.

Katika kipindi hiki kulikuwa na wasomi wazawa walioandika.

Tamthilia za wakati huo zililenga katika kusherehekea uhuru uliopatikana, kuwakejeli wakoloni, kuwakejeli wasomi wazawa waliobeza utamaduni wao na kushadidia ule wa kikoloni.

Zililenga pia kuwakweza wapigania uhuru wa kizalendo ambao kati yao walijitoa hata kufa.

Tamthilia za Mkwawa wa Uhehe (M.M. Mulokozi), Kinjeketile (E. Hussein) na Mkwawa Mahinya (F. Mkwera) na Martin Kayamba (G. Uhinga) ni miongoni mwa kazi zilizoingia katika kundi hili. Kupitia kazi hizi mtu huweza kujua matukio mbalimbali yaliyojiri.
Wakati uhuru ukipatikana, watu walikuwa na matazamio makubwa sana kwamba maisha yangekuwa bora kwa kuwa wakoloni walikuwa wameondoka na wazawa kushika utawala.

Katika kipindi hiki (1971 – 1981) maisha yalikuwa magumu kuliko ilivyotarajiwa.

Tamthilia kama “Giza Limeingia” (E. Mbogo), Mashetani (E. Hussein) Kilio cha Haki (A. Mazrui) Bwana Mkubwa (J. Mbonde) na nyinginezo ziliandikwa kuakisi ubaya wa wakati huo.

Aidha, katika kipindi cha kushamiri kwa utandawazi (Miaka ya 1980) mpaka sasa kuna matukio mengi yaliyojitokeza.

Hayo ni kama vile kuwapo kwa mwingiliano mkubwa wa kijamii kushamiri kwa mfumo wa kibepari na mengineyo.

Hayo yanaakisiwa na tamthilia kama vile “Wakati Ukuta” (E. Hussein), “Kwenye Ukingo wa Thim” (E.Hussein) “Nguzo Mama (P. Mhando) “Mkutano wa pili wa Ndege” na nyinginezo.

Tamthilia hizi humwezsha mtu kujua matukio mbalimbali ya kihistoria akizisoma. Pamoja na kuandikwa kwa lugha ya kisanaa, matukio yaliyojadiliwa ni bayana.

Hivyo, msomaji huwea kujifunza au kujikumbusha mambo mengi yaliyotokea katika jamii.