Misingi ya lugha ya Kiswahili

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Thursday, September 28  2017 at  08:36

Kwa Mukhtasari

Mwandishi maarufu na bingwa wa Kiswahili nchini Kenya Profesa Ken Walibora katika moja ya makala zake aliwahi kuandika, "Chombo cha baharini hakiwezi kwenda bila ya dira inayomwelekeza nahodha. Dira inamsaidia nahodha si tu kujua uelekeo wa safari bali pia huchangia pakubwa kukiepusha chombo kwenda mrama au kuzama.”

 

MWANDISHI maarufu na bingwa wa Kiswahili nchini Kenya Profesa Ken Walibora katika moja ya makala zake aliwahi kuandika, "Chombo cha baharini hakiwezi kwenda bila ya dira inayomwelekeza nahodha. Dira inamsaidia nahodha si tu kujua uelekeo wa safari bali pia huchangia pakubwa kukiepusha chombo kwenda mrama au kuzama.”

Mwongozo kwa wanahabari uliotayarshwa unalenga kuwasaidia na kuwaimarisha wanahabari katika kukitumia Kiswahli na kukijenga kama wenzo wa kuwasaidia katika safari yao kubwa ya uanahabari.

Wanahabari wanaotumia Kiswahili kama wenzo wao wa kujieleza wanastahili kukiona Kiswahili kama chombo mahsusi cha kuwawezesha kuvuka bahari pana ya taaluma yao. Lengo ni kuwawezesha wanaokitumia Kiswahili kwenye vyombo mbalimbali kama magazeti, mtandao, redio, na runinga.

Lugha ya Kiswahili ndicho chombo cha kutumiwa katika safari hii ndefu ya kazi za uanahabari na wanapaswa kukiheshimu na kukitumia kwa uangalifu na umakini mkubwa ili kisiangamie.

Maangamizi ya Kiswahili yanapaswa kuepukwa kwa kuzingatia matumizi bora na kuacha kukishushia hadhi yake mbali na kuwashushia hadhi wanahabari wenyewe.

Ndiyo maana tumeandaa mwongozo huu uwe dira ya kuwasaidia wanahabari hao kuingia katika kina kirefu cha bahari ya kazi yao huku wanakitumia Kiswahili kwa njia mwafaka.

Matumizi bora ya Kiswahili ni kwa faida ya wanahabari wenyewe na hadhira yao yaani wasomaji, wasikilizaji na watumiaji ambao aghalabu huyaona matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari kama kielelezo cha kuigwa.

Mara kwa mara tumeshuhudia wanahabari wakisongoa Kiswahili ama katika maandishi yao hata kattka matamshi yao yasiyoridhisha yenye kuathriwa na lugha za asili au lugha za kigeni.

Baadhi yao huwa na mazoea ya kuchanganya ndimi kiholela kama kwamba wanachelea kuwa wasipoyatumia maneno mawili matatu ya Kiingereza katika maandishi au matamshi yao ni ishara ya kuwa hawakusoma.

Hii ni kasumba ambayo haina budi kupigwa vita.

Ipo haja kujizatiti kuzungumza na kuandika Kiswahili sahihi na sanifu, hata ingawa katika miktadha mingine maneno ya kigeni yanayoweza kutumika ili kunogesha maelezo.

Aidha, lipo tatizo kubwa la kufasiri sisisi nahau na misemo kutoka katika Kiingereza na kuilazimishia matumizi ya Kiswahili.

Mwongozo huu ulioandikwa utawaongoza walioko ndani ya uzio wa Kampuni za Nation Media Group ili wazingatie mtindo mmoja unaoepuka mazoea na matumizi mengine ya lugha ambayo labda yanakubalika na wengine nje ya uzio huo.

Suala la kuwa na mwongozo wa mtindo wa chombo fulani cha habari si geni katika fani hii.

Mashirika makubwa ya habari duniani huwa na vitabu vyao vya mtindo kuelekeza waajiriwa wao wapya na wa zamani kuhusu lugha na kanuni za taaluma.

Maelekezo yaliyomo humu ni matokeo ya uchunguzi mwafaka na mpana.

Kuwa na mtindo mmoja kwa ajili ya kampuni moja bila kubana na kudumaza ubunifu na mitindo binafsi ya wanahabari wetu ndilo lengo letu tangu mwanzo.

Dira ya utendaji

Waajiriwa wanatumia Kiswahili kujieleza katika magazeti kama vile Mwananchi, Mwanaspoti, Taifa Leo, Taifa Jumapili na chombo kingine chochote kitakachobuniwa baadaye.

Wanahabari wanatarajiwa kuusoma mwongozo huu na kuutumia kama dira ya utendaji wao wa kazi za kila siku.

Waajiriwa wapya pia wanatarajiwa kuupitia na kujifahamisha na yaliyomo kabla kujitosa kikamilifu katika bahari ya fani ya uanahabari. Aidha, mwongozo huu utakuwa ukisahihishwa na kurekebishwa mara kwa mara ili uendane na wakati.

Kutolewa kwa mwongozo huu ni ithibati ya jinsi Kiswahili ni lugha ambayo umuhimu na umaarufu wake unaendelea kuongezeka ndani na nje ya Afrika Mashariki na Kati. Nasi tuna dhima ya kuendelea kuchangia ukuaji wake.

Ni matumaini yangu kwamba mwongozo huu utatufaa sote na utavisaidia vyombo vyetu vya Kiswahili kukwea na kudumu kileleni katika kusambaza habari na kuwa vielelezo bora vya kuigwa katika matumizi ya lugha ya Kiswahili.

smaina1@tz.nationmedia.com
0754 861664; 0716 694240