http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Misingi ya Leksikografia na Teminografia katika uundaji wa istilahi

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  13:25

Kwa Muhtasari

Katika leksikografia swali la msingi ni ‘neno ni nini’ na katika teminografia ni ‘istilahi ni nini’.

 

UUNDAJI wa istilahi kwa kiasi kikubwa unasheheni msukumo wa kuingiza maarifa mapya katika lugha lengwa.

Mchakato wa kuunda istilahi huanza kwa ukusanyaji wa istilahi katika lugha chanzi na halafu kuunda visawe vyake katika lugha lengwa. Ni bayana kwamba uundaji wa istilahi unahusiana kwa kiasi fulani na kazi za teminografia.

Shughuli za leksikografia na teminografia huongozwa na misingi tofauti.

Katika leksikografia swali la msingi ni ‘neno ni nini’ na katika teminografia ni ‘istilahi ni nini’.

Aidha, katika leksikografia hakuna uundaji wa maneno kama ilivyo kwenye teminografia ambapo kuna uundaji wa visawe vya istilahi zilizokusanywa katika lugha chazi.

Vilevile fasili ya maana katika leksikografia hutegemea matumizi ya neno wakati ambapo katika teminografia fasili huhusiana moja kwa moja na dhana ya istilahi inayokubalika kwa wataalamu wa uwanja husika wa maarifa.

Licha ya hayo, ni vyema kufahamu kwamba sio wataalam wote wanaokubali kwamba leksikografia na teminografia ni taaluma mbili zinazotumia mbinu tofauti. Kwa mujibu wa Bergenholtz katika Humbley (1997: 13-115) leksikografia na teminografia ni sinonimi, hivyo ni kosa kuzichukulia kama taaluma zenye mbinu tofauti.

Bergenholtz anaamini kwamba utofautishaji huo umefanywa kwa makusudi na wanaistilahi kwa nia ya kujitenga na kuanzisha himaya yao nje ya leksikografia, na hilo, kwa maoni yake, pale wanaistilahi walipobainisha katika ISO 1087 kwamba teminografia inachukua nafasi ya leksikografia ya lugha ya kitaalamu.

Anajikita katika kauli tatu katika kubainisha ikiwa leksikografia na teminografia ni vitu viwili tofauti au ni ni vitu vinavyooana. Kauli hizi ni kama zifuatazo:

Kwanza, kwamba ni vitu viwili tofauti ambapo teminografia inahusu lugha ya kitaalamu na leksikografia inahusu lugha ya kawaida.

Pili, kwamba kwamba ni vitu tofauti kwa vile teminografia ni sehemu ya istilahi na leksikografia ya lugha ya kitaalamu ni sehemu ya leksikografia kwa jumla na kila kimoja kina taratibu na mbinu zake.

Tatu, kwamba leksikografia ya lugha ya kitaalamu na teminografia ni sinonimi na ni sehemu ya leksikografia kwa jumla na wala teminografia haihusiani na teminolojia kwani utekelezaji wa shughuli za teminolojia hufanywa na makampuni na kamati za istilahi za kitaifa na kimataifa.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1.Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine Publisher.

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers. 

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com