http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197893/-/1a5cdcz/-/wangari.jpg

 

Mkabala na mbinu mbalimbali za uundaji istilahi za Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  13:27

Kwa Muhtasari

Zubeida (1982) anaeleza kuwa mkabala wake wa kuunda istilahi ni ule wa kukusanya na kuorodhesha maneno ‘magumu’ ya Kiingereza kwa kuzingatia mahitaji mahususi ya Afisi na Idara za Serikali, na kuyatafutia visawe au tafsiri sanifu bila ya kutilia maanani swala zima la uzingatiaji wa dhana na mahusiano yake katika uwanja mahususi wa maarifa.

 

BAKITA ikiwa imekabidhiwa jukumu la kukiwezesha Kiswahili kitumike mahali pa Kiingereza, hasa katika ofisi na idara za Serikali, iliingia katika uundaji wa istilahi ikiwa na lengo la kutafuta visawe au tafsiri za maneno magumu ya Kiingereza kama yalivyohitajika kwa ajili ya matumizi mbalimbali, hasa ya Kiserikali.

Kulingana na Zubeida (1982) anaeleza kuwa mkabala wake wa kuunda istilahi ukawa ni ule wa kukusanya na kuorodhesha maneno ‘magumu’ ya Kiingereza kwa kuzingatia mahitaji mahususi ya Afisi na Idara za Serikali, na kuyatafutia visawe au tafsiri sanifu bila ya kutilia maanani swala zima la uzingatiaji wa dhana na mahusiano yake katika uwanja mahususi wa maarifa.

Kutokana na mazingira hayo, mbinu za BAKITA za uundaji istilahi zililenga moja kwa moja katika namna ya kupata visawe vya Kiswahili. Hili linadhihirishwa na misingi ya uundaji istilahi iliyopendekezwa na BAKITA kama anavyosema (1982).

Kwa mujibu wa ISO CD 704 (1997), misingi ya uundaji istilahi haina budi kuzingatia mambo matatu, ambayo ni:

i. mfumo wa dhana

ii. ufafanuzi wa dhana

iii. vitajo vya dhana au istilahi.

Mfumo wa dhana

Katika kitengo hiki, misingi hiyo izingatie kwamba istilahi za uwanja wowote wa maarifa sio mkusanyiko wa kiholela bali hutokana na mfumo makini wa uhusiano baina ya dhana katika uwanja husika wa maarifa.

Ufafanuzi wa dhana

Misingi hii izingatie namna ya upataji wa fasili za dhana ambazo ni sahihi na zinazokubalika katika uwanja husika wa maarifa.

Vitajo vya dhana

Kitengo hiki kinasema kwamba misingi ilenge katika upatikanaji wa istilahi zinazokubalika kwa misingi ya sarufi ya lugha, utaalamu katika uwanja husika wa maarifa na utamaduni wa watumiaji lugha.

Ni bayana kuwa misingi ya uundaji istilahi ya BAKITA inazingatia kipengele kimoja tu cha uundaji wa vitajo vya dhana katika mchakato mzima wa uundaji istilahi. Kutozingatiwa kwa kipengele cha mifumo dhana pamoja na cha fasili za dhana kunaweza kutajwa kama upungufu mkubwa katika mbinu za uundaji istilahi za BAKITA.

Marejeo

Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1.Dar-Es Salaam: Nyambari Nyangwine Publisher.

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers.