http://www.swahilihub.com/image/view/-/3463388/medRes/1496376/-/128k3d2z/-/IRI.jpg

 

PROF P.I IRIBEMWANGI: Msomi na mtaalamu wa Isimu katika Chuo Kikuu cha Nairobi

Prof P.I. Iribemwangi

Prof P.I. Iribemwangi - mwanaisimu, mwandishi na msomi anayejivunia tajriba pana katika ufundishaji wa taaluma za Kiswahili. PICHA/ CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 24  2016 at  15:34

Kwa Muhtasari

HAKUNA yeyote aliye na nguvu za kuizima kabisa ndoto yako isipokuwa wewe mwenyewe! Usikubali mtazamo wa mtu mwingine dhidi yako kukufanya kuona dunia kuwa pahali pachungu pasipofaa.

 

Usijiruhusu kukatishwa tamaa na wabinafsi wachache utakaokutana nao, maana nao wapo! Huwezi kabisa kuyafikia matarajio yako wala kujenga chochote bila ramani. Kumbuka wewe ni wa kipekee kutokana na jinsi ulivyo.

Unapoanza kujilinganisha au kuilinganisha kazi yako na za watu wengine; matokeo yake ni kwamba utaanza kujidharau, kujihukumu, kujiona hufai au asiyeweza kufanya jambo lolote la maana.

Kila mtu aliumbwa afanye kitu kilicho tofauti na mwingine na kwa njia zisizofanana. Sote tuna mtindo tofauti inayotutambulisha katika fani mbalimbali.
Kumbuka mafanikio ni zao la jitihada na nidhamu.

Thamini kile unachokifanya huku uki - jitahidi kuwa mbunifu na mvumilivu. Watu wanaopenda kufanikiwa mara zote hutafuta mbinuza kuzitimiza ndoto zao za kila siku.

Hivyo, unatakiwa kuota ndoto za mafanikio siku zote. Ndoto hizo hazina gharama yoyote; hutegemea tu jinsi unavyoupanga muda wako.

Huu ndio ushauri wa Prof P.I. Iribemwangi - mwanaisimu, mwandishi na msomi anayejivunia tajriba pana katika ufundishaji wa taaluma za Kiswahili.

“Acha kujidharau na kutazama ukubwa wa udhaifu na matatizo yako. Acha kujihurumia na kujiona mtu asiyeweza chochote.

Unapohitaji jambo kubwa kutokea maishani mwako, unatakiwa kuwa na maono mapya. Mafanikio hutegemea ukubwa wa shauku uliyonayo. Jifunze kwa wengine ili upunguze uwezekano wa kuyarudia makosa yao,” anasema mhadhiri huyu.

MAISHA YA AWALI
Iribemwangi alizaliwa miaka ya 70 katika eneo la Amboni, Mweiga, Kaunti ya Nyeri. Alisomea katikashule ya msingi ya Amboni hadi darasa la tatu kabla ya wazazi wake kuhamia Nyahururu mnamo 1977.

Baada ya kufanya mtihani wa CPE mwishoni mwa 1982 katika shule ya Salama, alijiunga na shule ya upili ya Mwenje iliyopo Ng’arua, Nyahururu kisha kuhitimu kisomo cha sekondari mnamo 1986.

“Mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili zilipandwa kwangu na marehemu babangu, John Mwangi ambaye aliwahi kuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi. Alitambua umuhimu wa lugha hiyo, akawa ananinunulia vitabu vya hadithi fupi na nakala za gazeti la Baraza.”

Ingawa hivyo, walimu Richard Chitambe na D. T. Mureithi ndio waliomchochea pakubwa Iribemwangi kuienzi Fasihi ya Kiswahili walipomtanguliza katika uchambuzi wa ushairi na vitabu vya ‘Kisima cha Giningi’, ‘Mkemwenza’ na ‘Ukame’ vilivyokuwa vikitahiniwa katika mtihani wa kitaifa.

Ilhamu na kariha zaidi katika Kiswahili ilichangiwa na Alex Ngure na Ashiruka, walimu waliotagusana na Iribemwangi katika kiwango cha A-Level baina ya 1987 na 1988 katika shule ya upili ya Koilel, Gilgil.

“Ilikuwa fahari kupokezwa malezi ya lugha shuleni Koilel, ngome ya wasomi na watalaamu mashuhuri wa Kiswahili wakiwamo Maprofesa Nathan Ogechi (Chuo Kikuu cha Moi) na Ken Walibora (Kampuni ya Nation Media Group).

USOMI NA UTAALAMU
Baada ya kuhitimu kisomo cha Kidato cha Sita mwishoni mwa 1988, Iribemwangi alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Kikuyu kusomea shahada ya Ualimu mnamo 1989.

Anakiri kwamba motisha ya kuzamia taaluma za Kiswahili chuoni humo ilitokana na ulazima wa kutangamana na wasomi maarufu wa lugha hiyo, akiwamo Profesa Said A. Mohamed kutoka Zanzibar.

“Mbali na ufahamisho wake, utunzi wa msomi huyo uliniathiri pakubwa nikiwa mwanafunzi wa A-Level hasa baada ya kuuchambua ushairi wake katika kitabu ‘Kina cha Maisha’.

Wengine walionihamasisha zaidi ni Maprofesa Kineene wa Mutiso, John Habwe, Rayya Timammy, Jay Kitsao (marehemu), Madaktari Evans Mbuthia na James Zaja Omboga.

Baada ya kufuzu chuoni mwishoni mwa 1992, Iribemwangi alipata kazi katika Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) na kutumwa kufundisha Kiswahili katika shule ya upili ya Mugumo iliyopo Kaunti ya Kirinyaga.

Mnamo 1995, haja ya kubadilisha mkondo wa maisha yake pamoja na msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ni mambo yaliyomlazimisha Iribemwangi kurejea katika Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya Uzamili katika hadi mwishoni mwa 1996.

Japo yalikuwa matamanio yake kusomea Uanahabari au kuzamia taaluma ya Elimu (M.Ed), anaungama kuwa ni Dkt Mbuthia ndiye alimshawishi kusomea Kiswahili katika Idara ya Isimu na Lugha za Kiafrika.

Waliomshajiisha hata zaidi ni waliokuwa wanafunzi wenzake, Obuchi Moseti na Mwangangi Musyoka ambao kwa sasa ni wahadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu vya Moi (Eldoret) na SEKU (Kitui) mtawalia.

“Ilinijuzu kuukatiza udhati wa tangu utotoni niliokuwa nao na Fasihi ya Kiswahili na kuazimia haja ya kuzamia kwa kina masuala ya Isimu, Tafsiri na Leksikografia.”

Mnamo Januari 1997, TSC ilimtuma Iribemwangi kufundisha Kiswahili katika shule ya upili ya Mutige, Kirinyaga na kupandishwa cheo kuwa Naibu Mwalimu Mkuu. Miezi minne baadaye, aliajiriwa kuwa Mhadhiri wa Muda katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Kikuyu.

Ilimbidi apangue baadhi ya vipindi vyake kwenye ratiba ya masomo shuleni Mutige ili awezeshwe kufika Nairobi kila Ijumaa kuhudhuria na kuendesha kozi za Kiswahili chuoni chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Idara, Dkt Omboga. Mnamo 1999, Iribemwangi alifanywa Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ilikuwa hadi 2002 ambapo alianza kuandaa pendekezo la utafiti kwa minajili ya shahada ya Uzamifu (phD) chuoni humo kwa matarajio ya kufuzu baada ya miaka minne.

Ingawa hivyo, kifo cha mama mzazi ambacho kilitokea mnamo Machi 2005 kiliyumbisha pakubwa ulimwengu wa Iribemwangi kiasi kwamba alichelewa kuyafikia malengo yake ya kiusomi kwa mwaka mmoja.

Tasnifu yake, “A Synchronic Segmental Morphophonology of Standard Kiswahili” ilikamilika Julai 2007 chini ya usimamizi wa Maprofesa Habwe, Kyallo Wadi Wamitila na Dkt Jane Oduor.

UANDISHI
Akisomea shahada ya kwanza chuoni Nairobi, Iribemwangi alijitosa katika utunzi wa kazi za kibunifu baada ya kusoma “Nyota ya Rehema” na “Kicheko cha Ushindi” za (Mohamed Suleiman Mohamed).

Baadhi ya mashairi yake yalichapishwa miaka 25 baadaye katika Diwani ya ‘Miali ya Ushairi’ (2015). Mnamo 2007, alichapishiwa hadithi mbili katika “Alidhani na Hadithi Nyingine” kabla ya mkoko kualika maua kwenye mikusanyiko ya Hadithi Fupi za “Kunani Marekani” na “Sina Zaidi”.

Mbali na kuandika miongozo ya “Utengano”, “Mstahiki Meya”, “Kidagaa Kimemwozea” na “Damu Nyeusi”, Iribemwangi pia alishirikiana na Dkt Ayub Mukhwana wa Chuo Kikuu cha Nairobi kuandika kitabu “Isimujamii” mnamo 2011 kabla ya kutunga “Fasihi: Andishi na Simulizi” kwa kuwashirikisha Kariuki Chege na Betty Kiruja mnamo 2016.

Akiwa mtaalamu wa masuala ya Isimu, Iribemwangi ana machapisho mengi katika vitabu na majarida ya kitaaluma baadhi yakiwa Structure of Kiswahili: Sounds, Sound Changes and Words (2010); “Mofofonolojia ya Kiswahili Sanifu: Matatizo katika Machapisho yake” katika Ukuzaji wa Kiswahili:

Dhima na Majukumu ya Asasi Mbalimbali (2014); “A Case for the Harmonization of Kikuyu, Kiembu and Kimbeere Phonology and Orthography” katika The Harmonization and Standardization of Kenyan Languages: Orthography and Other Aspects (2012) na “Kikuyu Phonology and Orthography” katika Culture in Aphasia: The Language Loss of the Indigenous (2016).

Hadi kufikia sasa, anajivunia zaidi ya machapisho 50 ya kibunifu, uhakiki, nadharia na kiada. Ingawa anakiri hatawahi kutunga riwaya, “Zingo la Bahari” na “Kwani Kunani” ni miongoni mwa hadithi zake zitakazochapishwa karibuni.

JIVUNIO
Tajriba ya Iribemwangi katika ufundishaji wa Kiswahili imempa fursa ya kujivunia wataalamu wengi katika ulingo wa Kiswahili, wakiwamo wanahabari Carol Nderi (KTN) na Yassin Juma aliyewahi kuhudumu katika Runinga ya NTV.

Wengine ni wanasiasa Sabina Chege na Mary Seneta ambao ni Wabunge Wawakilishi wa Wanawake katika Kaunti za Murang’a na Kajiado mtawalia.

“Hawa ni wachache tu miongoni mwa wasomi, wataalamu, wanahabari, wahariri, wanasiasa, walimu na wahadhiri chungu nzima ambao wamefaidi kutokana na maarifa tuliyochangiana madarasani,” anasema Mkurugenzi huyu wa Almasi Consultants, kampuni inayojishughulisha na masuala ya mawasiliano, tafsiri, uanahabari na uchapishaji.

Mbali na kuwa Mhadhiri Mkuu wa Isimu katika Idara ya Kiswahili, Iribemwangi pia husimamia na kuwaongoza wanafunzi wa Uzamili na Uzamifu katika Idara ya Isimu na Lugha hasa wanaotafiti kuhusu fonolojia za lugha mbalimbali.

Kwa sasa ndiye msimamizi wa masomo ya Uzamifu kwa wanafunzi wanaojisimamia wakati wa likizo katika Kitivo cha Sanaa, Chuo Kikuu cha Nairobi.