http://www.swahilihub.com/image/view/-/3806482/medRes/1558768/-/h4nmvk/-/mwa.jpg

 

Mwalimu mwenye umilisi wa kipekee wa Kiswahili na mwandishi

Justus Kyalo Muusya

Mwalimu mwenye umilisi wa kipekee wa Kiswahili na mwandishi, Bw Justus Kyalo Muusya. Picha/CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, February 9   2017 at  15:57

Kwa Mukhtasari

Ni vigumu kujitolea kwa jambo lolote lile maishani na Mola akose kabisa kukuneemesha kwalo, kwa mujibu wa Bw Justus Kyalo Muusya, mwandishi shupavu na mwalimu mahiri wa Kiswahili shuleni Kaluva, Kitui.

 

JITIHADA za mja na neema za Maulana ni pande mbili za sarafu moja. Ni vigumu kujitolea kwa jambo lolote lile maishani na Mola akose kabisa kukuneemesha kwalo. Aidha, Mwenyezi Mungu ataona vigumu kubariki pasipo na juhudi zozote kutoka kwa aliye katika uhitaji wa msaada wake. Ukijitolea kwa udi na uvumba kulimakinikia jambo lolote, hapana shaka kwamba utapokea baraka kubwa. 
Huu ndio ushauri wa Bw Justus Kyalo Muusya, mwandishi shupavu na mwalimu mahiri wa Kiswahili shuleni Kaluva, Kitui. 

Maisha ya Awali
Muusya alizaliwa katika kijiji cha Kangii, kata ya Kakeani katika Kaunti ya Kitui yapata miaka thelathini na mitano iliyopita. Wazazi wake ni Tabitha Muyali na mwendazake Muusya Mukuli. Ni mwana wa tatu katika familia ya watoto saba, wavulana watano na wasichana wawili. Alisomea katika shule ya msingi ya Kangii. Baada ya kuufanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mnamo 1998, jahazi lake la masomo lilikuwa linayumba si haba nusura kwenda mrama. Hii ni kwa sababu  alitoka katika familia yenye ufukara wa pangu pakavu, na katika ukoo ambao elimu ilikuwa ni 'mwiko’ kwa baadhi ya wanajamii.
Ingawa hivyo, aliibuka wa pili katika kata nzima ya Kakeani. Alituzwa katika sherehe zilizoandaliwa na chifu wa kata, Bw Charles Mbiti (mstaafu). Hafla hiyo ilikuwa kama daraja kwake. Iliweza kubainika wazi kuwa japo alifaulu mno katika mtihani wa darasa la nane, ilikuwa rahisi kwa ngamia kupitia kwenye tundu la sindano kuliko kijana huyu kuiona milango ya shule za upili. 
Baadhi ya wanakijiji walichangia elimu yake ya shule ya upili. Hawa walishirikishwa katika zoezi hili na Joseph Syuma ambaye kwa sasa ni Askofu Mkuu wa Kanisa la GFBC, Kenya. Akali ya fedha zilizochangwa zilimwezesha kujiunga na shule ya Kakeani mnamo Mei 17, 1999. Huu ulikuwa ni muhula wa pili kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili. Kilichoshangaza wengi ni kuwa Kyalo aliweza kuibuka wa pili katika mtihani wa mwisho wa muhula wa pili, na kuongoza katika mitihani mingine yote katika kidato cha kwanza na cha pili. 
Ukosefu wa karo ulimweka nyumbani kila muhula kipindi kirefu kuliko kile alichokuwa darasani. Walimu wake wa darasa, Bw Moses Wambua (kwa sasa Mwalimu Mkuu katika shule ya upili ya Kangii) aliweza kutambua uwezo na talanta ya mwanafunzi huyu na kujitolea kwa jino na ukucha kumfaa. 
Wambua alimsaidia kupata ufadhili wa masomo katika shule binafsi ya Likii Hill School viungani mwa mji wa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia. Kujiunga na shule hii kulichukuliwa kuwa utovu wa nidhamu kwa vile babake alikatalia mbali ufadhili huu akidai kuwa alikuwa hajapata kusikia shule isiyolipwa karo. Wakati huu, Bw Wambua alikuwa amekwishampulizia Justus mapenzi ya lugha ya Kiswahili. Aliupasi vyema mtihani wake wa Kidato cha Nne. 

Usomi na Taaluma
Japo watu wengi, akiwamo mwalimu Wambua walimshauri kujitosa katika taaluma tofauti, aliazimia kusomea Shahada ya Ualimu (Kiswahili na Historia) ili kufuata nyayo za mwalimu na mwandani wake huyo. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, bewa la Laikipia mnamo 2005 na kuhitimu mwishoni mwa 2008. Huko alipatana na wahadhiri waliochochea ari yake ya kubobea zaidi katika taaluma ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na maprofesa Onyango Ogolla na Nabea Wendo, kwa sasa wa Chuo Kikuu cha Laikipia. 

Alipata ajira ya muda kufundisha Kiswahili na Historia katika shule ya Wasichana ya Mua katika Kaunti ya Machakos mwaka huo wa 2008.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma kufundisha katika shule ya upili ya Kaluva, Kaunti ya Kitui mnamo 2010. 

Mwaka uliofuata aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Masomo na Mitihani shuleni humo. Mbinu zake za kipekee na juhudi chungu nzima zimeimarisha mtazamo wa somo la Kiswahili shuleni Kaluva.

Jambo hili lilichangia matokeo ya Kiswahili kuimarika mno kwa kipindi kifupi.

Wanafunzi wake wamekuwa wakichukulia somo hili kuwa taaluma. Wengi wao wamejiunga na vyuo vikuu mbalimbali kusomea Kiswahili. Wengine wamejiunga na taaluma ya Uanahabari. 

Muusya amekuwa mhakiki shupavu wa miswada.

Tangu 2013 amekuwa akihakiki miswada katika kampuni ya EAEP.

Hii hasa ni miswada inayohusu kazi za fasihi. Hii ni baada ya Mhariri Mkuu wa Kiswahili, Bw Job Mokaya kutambua umahiri wake katika jambo hili.

Ni katika kipindi hiki ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa masomo ya umahiri ambapo alifuzu 2012 baada ya kuwasilisha tasnifu, “Mandhari katika Hadithi Fupi za Kisasa: Mtazamo Linganishi” chini ya usimamizi wa Profesa Kitula King’ei na Mwalimu Kamunde. 

Chuoni humu, alitagusana na magwiji wengine kama vile Madaktari Richard Wafula, Pamela Ngugi, Edwin Masinde na Miriam Osore. Kutoka kwao aliweza kunoa makali ya usomi, ikiwa ni pamoja na ujuzi wa kuhakiki fasihi ya dhati. 

Kati ya kazi hizi za fasihi ya dhati zilikuwapo za Maprofesa Said A. Mohamed na Ken Walibora.

Tangu kuhitimu uzamili, amekuwa Mhadhiri wa Muda katika South Eastern Kenya University (SEKU), Kitui akifundisha kozi za Isimu na Fasihi.  
Mnamo 2013, alirejea katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa shahada ya Uzamifu (phD).

Hivi sasa yuko katika hatua za mwishomwisho za kuandaa tasnifu, “Maadili ya Kisiasa katika Riwaya za Kiswahili za Kisasa za Mohamed na Walibora” chini ya usimamizi wa Profesa King’ei na Dkt Masinde.

Familia

Justus ana familia. Mkewe Ann Kavuu ni tabibu katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Machakos.

Wawili hao wamebarikiwa na mvulana mmoja, Moses Mumo. 

Uandishi

Muusya ameweza kuchapisha vitabu kadha. Vingine vingi vitachapishwa hivi karibuni.

Kazi yake ya awali kuchapishwa ni riwaya ya Sinema Bila Malipo aliyoiandika akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika chuo kikuu mnamo 2005.

Hata hivyo, ilichukua miaka mitano kwenye matbaa kadha bila ya ripoti yoyote kuihusu kutolewa. Mwaka wa 2010 aliweza kuiondoa kwa matbaa hizi na kujichapishia. 

Mwaka wa 2012 akishirikiana na Profesa King’ei na Bi Leah Mwangi (wa Chuo Kikuu cha Karatina), walichapisha Mwongozo wa Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine (JKF) na Mwongozo wa Mstahiki Meya (Target Publishers, siku hizi ni Spotlight Publishers). Mwaka uliofuata, walishirikiana tena kuandaa Mwongozo wa Kidagaa Kimemwozea (EAEP). 

Mwaka wa 2015, Muusya alichapisha Mwongozo wa Msururu wa Usaliti (EAEP) na kushirikiana na King’ei kuandika Mwongozo wa Mwakilishi wa Watu (EAEP). Miongozo hii inatumiwa na wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita nchini Uganda. 

Aidha, ameshirikiana na Leah na King’ei kuandaa mswada wa mashairi, Sanaa ya Ushairi: Historia na Uchambuzi. Huu upo katika hatua za mwisho za kuchapishwa na kampuni ya Focus. Amechangia hadithi 'Kusisimua Misuli’ katika diwani Tutaonana Tena na Hadithi Nyingine iliyohaririwa na Stella Were na Edison Wanga. 

Vilevile, diwani ya hadithi fupi ambayo ameshirikiana na Profesa King’ei kuihariri, Kusukuma Kitu na Hadithi Nyingine itachapishwa na kampuni ya Phoenix hivi karibuni. Zaidi, Muusya ameshirikiana na Simon Ngige (wa shule ya Wavulana  ya Alliance) kuandaa kitabu cha kiada kwa wanafunzi wa Kidato cha Tatu nchini Rwanda, kitakachochapishwa na EAEP hivi. 

Miswada ya riwaya, tamthilia na hadithi fupi chungu nzima ni kati ya kazi zake bunilizi zitakazochapishwa karibuni.

La kujivunia

Msomi huyu ameweza kuasisi nadharia mpya ya uhakiki wa fasihi iitwayo Daindamano.

Daindamano ni istilahi iliyotokana na mawazo ya wanafalsafa ya daintolojia (tafsiri yake ya deontology) na umaandamano (tafsiri yake ya Consequentialism). 

Daintolojia na umaandamano ni falsafa za Immanuel Kant na Stuart Mill mtawalia. 

Sehemu ya dain kutoka kwa neno daintolojia na ile ya ndamano kutokana na neno umaandamano zikiunganishwa zinaunda neno daindamano.

Hii ni nadharia inayochunguza maadili ya viongozi katika utendakazi wao.

Nadharia yake hii ndio inaongoza utafiti wake wa shahada ya Uzamifu.

Mhimili wake mkuu ni kuwa kiongozi yeyote haruhusiwi kutenda kitendo kisichokubaliwa na wanajamii anaowaongoza, isipokuwa ikiwa kwa kutenda kitendo hicho matokeo yake yatanufaisha wengi, hata kama kitawaumiza wachache. 

Mawazo haya aliyawasilisha katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kwenye pendekezo la utafiti la Uzamifu na kukubaliwa na wataalamu wa fasihi chuoni humu.

Aidha, aliwasilisha mawazo haya ya kinadharia katika kongamano la CHAUKIDU (Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA) jijini Nairobi mnamo Desemba 2016.

Ana imani kubwa kuwa atakapochapisha na kusambaza mawazo haya kuanzia mwaka 2017, yatapata wafuasi na wachangiaji wengi kote ulimwenguni.